Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam limewakamata watu 31 kwa tuhuma za kujihusisha na matukio ya uporaji baada ya kuvunja nyumba, kujeruhi na kuiba vitu mbalimbali vya nyumbani.
Akizungumza Mei 7, 2022 Kamanda wa Polisi Maalum, Muliro Jumanne amesema, watu hao wamekamatwa katika operesheni maalum ya msako wa mtaa kwa mtaa dhidi ya vijana wanaojihusisha na vitendo vya kihalifu maarufu Panya Road.
Amesema operesheni hiyo ambayo ni endelevu ilianza Aprili 27, 2022 imefanikiwa kuwakamata wahalifu hao ambao wengi wao ni vijana wenye umri kati ya miaka 13-20 na wakati wanafanya uhalifu hutumia mapanga, visu, nondo, na mikasi mikubwa.
“Jeshi la Polisi Kanda Maalum linaendelea kushirikiana na raia wema, kwa kupokea taarifa mbalimbali za wahalifu na linaahidi kuzifanyia kazi, ikiwa ni pamoja na kuwakamata kabla ya kutenda uhalifu,” amesema Muliro
Amebainisha katika mahojiano ya kina kati ya Jeshi la Polisi na watuhumiwa hao wameonyesha baadhi ya vitu walivyoiba zikiwemo runinga 12 na simu za mkononi 4.
“Jeshi la Polisi linatoa onyo na halitasita kuwakamata watu ambao wamekuwa wakipokea mali mbalimbali za wizi, zinazotokana na matukio ya kihalifu, pia halitasita kuwafikisha kwenye vyombo vingine vya kisheria,”amesema
Katika hatua nyingine, Jeshi hilo limefanikiwa kumkamata Fakhi Hamisi (30), mkazi wa Ununio na wenzake 33 wakiwa na madawa ya kulevya aina ya bahangi gunia 10 zenye uzito wa kilogramu 180, kete 497 pamoja na puli 48.
Watuhumiwa hao walikamatwa maeneo ya Kinondoni baada ya kupata taarifa fiche za kihalifu,ambapo walikutwa na sare za Jeshi la Wananchi (JWTZ), darubini, kisu, blaketi na viatu mbalimbali vya Jeshi, pikipiki 6, bajaji 1 vitu ambavyo ni matokeo ya kazi za kihalifu.
No comments:
Post a Comment