Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kajubi Mukajanga, akizungumza wakati wa kuwaapisha majaji wa Tuzo za Umahili wa Uandishi wa Habari Tanzania (EJAT 2021).
Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili Baraza la Habari Tanzania (MCT) Jaji mstaafu Robert Makaramba, akizungumza wakati wa kuwaapisha majaji wa Tuzo za Umahili wa Uandishi wa Habari Tanzania (EJAT 2021).
Nguli wa Habari, Mkubwa Ally, akiapa kuwa Jaji wa Tuzo za Umahili katika Uandishi wa Habari (EJAT 2021) mbele ya Jaji mstaafu Robert Makaramba. Katikati ni Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kajubi Mukajanga. (Na Mpiga picha Wetu).
Mwandishi wa Habari Mkongwe, Mbaraka Islam, akiapa kuwa Jaji wa Tuzo za Umahili katika Uandishi wa Habari (EJAT 2021) mbele ya Jaji mstaafu Robert Makaramba. Katikati ni Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kajubi Mukajanga.
Mwanzo Millinga akiapa kuwa Jaji wa Tuzo za Umahili katika Uandishi wa Habari (EJAT 2021) mbele ya Jaji mstaafu Robert Makaramba.
Beatice Bandawe akiapa kuwa Jaji wa Tuzo za Umahili katika Uandishi wa Habari (EJAT 2021) mbele ya Jaji mstaafu Robert Makaramba.
Aboubakar Famau akiapa kuwa Jaji wa Tuzo za Umahili katika Uandishi wa Habari (EJAT 2021) mbele ya Jaji mstaafu Robert Makaramba. Katikati ni Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kajubi Mukajanga.
Majaji walioapishwa leo katika picha ya pamoja na uongozi wa MCT. Waliokaa katikati ni Jaji Robert Makaramba, ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya MCT, kushoto niKatibu Mtendaji wa MCT, Kajubi Mukajanga nakulia ni Rais wa MCT Jaji Juxton Mlay.
Dar es Salaam, Tanzania
Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla ya utoaji wa Tuzo za Umahili wa Uandishi wa Habari Tanzania (EJAT 2021).
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kutangaza mchakato wa kuwapata washindi hao Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kajubi Mukajanga alisema "Rais Samia Suluhu Hassan atakuwa mgeni rasmi katika shughuli za utoaji Tuzo na ndiye atakaye mkabidhi Tuzo mshindi wa jumla pamoja na mshindi wa Tuzo ya Maisha ya Mafanikio Katika Uandishi wa Habari – Lifetime Achievement in Journalism Award (LAJA) 2022, hii itakuwa ni mara ya pili kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano aliyeko madarakani kuwa mgeni rasmi katika Tuzo hizo".
Hii itakuwa ni mara ya 13 kuwatuza waandishi waliofanya vizuri katika kazi zao za kiandishi katika mwaka uliotangulia ambapo kazi 598 zimepokelewa ili kushindanishwa katika makundi 20 ya Tuzo za Umahiri wa Uandishi wa Habari Tanzania (EJAT) 2021. Kazi za mwaka huu zimeongezeka kutoka 396 zilizopokelewa kwa ajili ya EJAT 2020.
Kati ya kazi hizo 598 zilizowasilishwa, waandishi wa mkoa wa Dar es Salaam wanaongoza kwa kuwasilisha kazi 250 wakifuatiwa na mkoa wa M wanza ambao wamewasilisha kazi 63, Zanzibar imeshika nafasi ya tatu kwa kuwa na kazi 59, Arusha ipo nafasi ya nne wakiwa na kazi 33, huku Tanga ikishika nafasi ya tano kwa kuwa na kazi 17. Kazi hizo zimewasilishwa na waandishi kutoka vyombo vya habari 73.
Katika Tuzo za mwaka huu, waandishi vijana wamejitokeza sana kushindanisha kazi zao, ikiwa ni pamoja na waandishi wa habari kutoka The Chanzo, Nukta Habari, Website Paradigm Initiative, Shamba FM, Furaha Radio, Mviwata Radio, Leo TV, online TIFO TV, Kagera Community Radio, Storm FM na Kings FM.
Pia katika mashindano ya mwaka huu, kuna mwandishi mmoja ambaye ameshiriki kwa miaka 12 mfululizo, wakati waandishi wapya wakiwa 206 wanaoshiriki kwa mara ya kwanza.
Vile vile makundi ya kushindaniwa yameongezeka kutoka makundi 18 mwaka 2020 hadi kufikia 20 kwa EJAT 2021, ambapo makundi ya Utawala Bora na Uwajibikaji pamoja na kundi la Habari za Ushirika, yaliongezwa.
Jopo la Majaji wa Tuzo za Umahiri wa Uandishi wa Habari Tanzania (EJAT) 2021 wameapishwa leo ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kuanza kupitia kazi zilizowasilishwa kushindanishwa ili kupata kazi zilizo bora katika uandishi na kuzitambua.
Washindi wa EJAT 2021 na wa Tuzo ya Mafanikio Katika Maisha ya Uandishi wa Habari 2022, watakabidhiwa tuzo zao katika kilele cha Tuzo za mwaka 2021 mnamo Mei 28, 2022, litakalofanyika Dar es Salaam katika Hoteli ya Serena.
Jopo la Majaji litaongozwa na mwandishi mzoefu Mkumbwa Ally. Majaji wengine ni Mwanzo Millinga, Imane Duwe, Rose Haji, Aboubakar Famau, Beatrice Bandawe na Mbaraka Islam. Jopo hilo la majaji limeapishwa na Jaji Mstaafu, Robert Makaramba, ambaye pia ni mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya MCT.
Baada ya kuapishwa, Jopo la Majaji litakutana kwa muda mfupi ili kujadiliana juu ya utaratibu wa mchakato wa kupitia kazi za kushindaniwa na kisha kuahirisha kikao hicho hadi Mei 7, 2022 watakapokutana tena kuanza kazi ya kupitia kazi za EJAT 2021 kwa siku nane mfululizo.
Mchakato wa kumtafuta mshindi wa Tuzo ya Maisha ya Mafanikio Katika Uandishi wa Habari (LAJA) 2022 umeshaanza. Tuzo hii humtambua mwandishi ambaye katika maisha yake ametoa mchango mkubwa katika kuiendeleza tasnia ya habari. Utaratibu wa kutafuta Mshindi wa Tuzo ya Maisha ya Mafanikio Katika Uandishi wa Habari ni tofauti na ule wa EJAT ambapo washindi wanatokana na makundi mbalimbali ya kushindaniwa.
Hii itakuwa ni mara ya sita Tuzo ya Maisha inatolewa. Washindi waliopata Tuzo hiyo huko nyuma ni Fili Karashani mwaka 2012, Hamza Kassongo mwaka 2013 na Mariam Hamdan mwaka 2014. Wengine ni Jenerali Ulimwengu mwaka 2015 na Rose Haji Mwalimu mwaka 2016.
Taasisi zinaounda Kamati ya Maandalizi ni Baraza la Habari Tanzania (MCT), Wakfu wa Vyombo vya Habari (TMF), Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), Jukwaa la Wahariri’ (TEF), HakiElimu, Agriculture Non-State Actors Forum (ANSAF), Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) na Twaweza.
No comments:
Post a Comment