Advertisements

Thursday, June 27, 2024

IDARA YA UCHUMI NA UZALISHAJI NI MUHIMU KWA MAENDELEO YA TAIFA




Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Bw. Herman Tesha akifungua kikao kazi cha Makatibu Tawala Wasaidizi wa Sehemu ya Uchumi na Uzalishaji (hawapo pichani) kilicholenga kuandaa Mpango Mkakati wa pamoja wa mikoa wa utekelezaji wa shughuli za uchumi mahalia, kilichofanyika mkoani Morogoro.

Makatibu Tawala Wasaidizi wa Sehemu ya Uchumi na Uzalishaji wakimsikiliza Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Bw. Herman Tesha (hayupo pichani) wakati akifungua kikao kazi chao cha kuandaa Mpango Mkakati wa pamoja wa mikoa wa utekelezaji wa shughuli za uchumi mahalia, kilichofanyika mkoani Morogoro.

Mwenyekiti wa Makatibu Tawala Wasaidizi Sekta za Uchumi, Bi. Aziza Mumba akieleza namna walivyojipanga kuandaa Mpango Mkakati wa pamoja wa mikoa wa utekelezaji wa shughuli za uchumi mahalia mara baada ya Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Bw. Herman Tesha kufungua kikao kazi chao.

Mkurugenzi Msaidizi, Idara ya Tawala za Mikoa, Sehemu ya Uchumi na Uratibu wa Sekta za Uzalishaji Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhandisi Enock Nyanda akieleza lengo la kuandaa mpango mkakati utakaowezesha kutekeleza mipango mbalimbali inayohusu uchumi mahalia.









Na James Mwanamyoto, OR-TAMISEMI
Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Bw. Herman Tesha amesema, Idara ya Uchumi na Uzalishaji katika Sekretarieti za Mikoa ni muhimu sana katika kuchagiza na kuleta maendeleo ya taifa.

Bw. Tesha amesema hayo leo kwa niaba ya Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-TAMISEMI Bw. Sospeter Mtwale, wakati akifungua kikao kazi cha Makatibu Tawala Wasaidizi wa Sehemu ya Uchumi na Uzalishaji kilicholenga kuandaa Mpango Mkakati wa pamoja wa mikoa wa utekelezaji wa shughuli za uchumi mahalia.

“Kazi ya msingi (core function) ya Sekretarieti za mikoa hivi sasa iko chini ya Idara ya Uchumi na Uzalishaji, hivyo ni idara muhimu yenye mchango mkubwa katika kuleta maendeleo na kukuza uchumi wa taifa letu,” Bw. Tesha amesisitiza.

Bw. Tesha amewataka Makatibu Tawala Wasaidizi hao wanaoziongoza Idara za Uchumi na Uzalishaji katika Sekretarieti za Mikoa, kutumia weledi na kuwa wabunifu ili waache alama ya utendaji kazi wao pindi watakapo ondoka katika maeneo waliyopewa dhamana ya kuyasimamia.

“Jitahidini sana kutumia weledi wenu katika maeneo mnayoyasimamia kwani Serikali haina mashaka na uwezo wenu na ndio maana imewaamini na kuwapatia jukumu la usimamizi wa Idara ya Uchumi na Uzalishaji,” Bw. Tesha amehimiza.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Makatibu Tawala Wasaidizi Sekta za Uchumi, Bi. Aziza Mumba amesema wako tayari kupata mafunzo na kwenda kuandaa mipango ya uchumi mahalia, ikiwa ni pamoja na kushirikiana na Ofisi ya Rais-TAMISEMI kuleta ufanisi na mabadiliko ya kiutendaji katika Idara wanazozisimamia.

“Idara za Uchumi na Uzalishaji zinapaswa kuimarika na si kudumaa kiutendaji, zikidumaa maana yake na sekta za kijamii haziwezi kukua kwani bila uchumi imara taifa litawezaje kujenga miundombinu bora ya shule, afya na barabara,” Bi. Mumba ametoa angalizo.

Naye, Mkurugenzi Msaidizi, Idara ya Tawala za Mikoa, Sehemu ya Uchumi na Uratibu wa Sekta za Uzalishaji Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhandisi Enock Nyanda, amesema Makatibu Tawala Wasaidizi hao wamekutana kwa lengo la kuandaa mpango utakaowezesha kwenda kutekeleza mipango mbalimbali inayohusu uchumi mahalia.

Akizungumzia uchumi mahalia, Mhandisi Nyanda amesema ni nadharia mpya ambayo inalenga kuanisha nani ana rasilimali gani na afanye nini na mwingine na rasilimali ipi na aitumie vipi katika suala zima la kutengeneza fursa za ajira na kipato zilizopo katika mnyororo wa rasilimali zinazomzunguka.

Uandaaji wa mpango mkakati wa pamoja wa mikoa wa utekelezaji wa shughuli za uchumi mahalia ni moja ya afua katika utekelezaji wa Program ya Uimarishaji wa Tawala za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa (RLGSP) ambayo Juni 27, 2024 itazinguliwa rasmi na Ofisi ya Rais-TAMISEMI jijini Dodoma kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na wanashirikishwa kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na maendeleo katika maeneo yao.





No comments: