Advertisements

Saturday, June 29, 2024

KAZI ZA UJENZI ZIFANYIKE KWA UBORA NA UZALENDO - DKT. BITEKO


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewataka Makandarasi nchini kutekeleza miradi ya ujenzi kwa ubora na uzalendo mkubwa ili wainue uchumi wa nchi na kuhakikisha unashikiliwa na Makandarasi wazawa.

Dkt. Biteko ameyasema hayo tarehe 28 Juni, 2024 alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kufunga Kongamano la Makandarasi na Watoa Huduma Shirikishi lililoandaliwa na Chama cha Umoja wa Makandarasi na Watoa Huduma Shirikishi Tanzania (TUCASA) jijini Dar es Salaam.
Vile vile, amewataka kuheshimu matumizi ya fedha za miradi, kwa kufanyia shughuli za ujenzi, na faida watakayoipata kuiwekeza na kutunza kampuni zao.

Aidha, ameielekeza Wizara ya Ujenzi kuweka mkakati wa kuwainua makandarasi nchini na kuhakikisha unatekelezwa ipasavyo kuanzia ngazi ya Wizara ya Ujenzi yenyewe pamoja na Wizara ya Fedha kisha kuendelea na mazungumzo na mabenki ili kuja na mpango mzuri wa kuwawezesha makandarasi kimtaji.

Amesema Ofisi ya Waziri Mkuu itaelekeza sekta zingine zikiwemo Nishati, Maji, Uchukuzi, kuhakikisha zina wabeba wakandarasi wazawa; pamoja na kuziwekea malengo ambayo kila mwaka kwenye mkutano wa makandarasi unapima utekelezaji wa malengo hayo.

Aidha, amewataka kuiga mfano kutoka Wizara ya Kilimo ya BBT, Wizara ya Ujenzi iwasaidie vijana kuanzisha makampuni na kuwapatia kazi ndogo ndogo ili kuwajengea uzoefu.
Dkt. Biteko pia amesisitiza kuwa, Serikali imeendelea kuwachukulia hatua watumishi wote wa umma wanaobainika kujihusisha na vitendo vya rushwa.

Dkt. Biteko amesema, katika mpango mkakati wa kukuza makandarasi wa ndani, kumewekwa kipangele cha kuhakikisha kuwa miradi yote inayotekelezwa kwa fedha za mikopo kutoka kwa wadau wa maendeleo kunatengwa asilimia isiyopungua 20 kwa ajili ya makandarasi wa ndani.

Dhamira ya Mhe Rais ni kuwajengea uwezo makandarasi wazawa na ametoa maelekezo kwa viongozi wote wa Serikali pamoja na watumishi wa ngazi zote kuhahakikisha wanatekeleza agizo lake la kuwakuza na kuwajengea uwezo wakandarasi wa ndani ili waweze kutekeleza miradi mikubwa.
Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameeleza Wizara kupitia Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB)imefanikiwa kuanzisha mpango mahsusi wa kuwashirikisha Mahandisi vijana kupitia miradi ya ujenzi ili kuwajengea uwezo zaidi katika miradi inayoendelea ya ujenzi ambapo hadi sasa, vijana waliopitia program ya SEAP ni 12,772 na wanao endelea nayo ni 3,317.

Amebainisha kuwa katika mwaka wa fedha 2024/2025 Wizara imetenga miradi ya Ujenzi wa barabara zenye urefu wa kilometa 120 za lami ambazo zitashindanishwa kwa Makandarasi wa ndani pekee pamoja na kutoa kipaumbele kwa Makandarasi wanawake ambapo imetenga kilometa 20.
Naye, Mwenyekiti wa TUCASA Samwel Marwa, ameiomba Serikali iwe mlezi kwa TUCASA ili kuwajengea uwezo wa kufanya kazi na kusimama wenyewe. Pia ameiomba Serikali kuendelea kupambana na rushwa ili kuifanya TUCASA kufanya kazi kwa weledi na kupata faida katika majukumu yao.

No comments: