Advertisements

Wednesday, June 26, 2024

RUTO AKUBALI YAISHE AONDOA MSWADA WAFEDHA ULIOZUA MAANDAMANO NCHINI KENYA


Rais William Ruto amesema hatotia saini Mswada wa Fedha wa 2024 kuwa sheria .

Katika kikao na waandishi wa habari siku moja baada ya maandamano makubwa kushuhudiwa nchini kupinga mswada huo ,Ruto pia ametangaza hatua mbalimbali za kupunguza mgao wa fedha za matumizi katika Ofisi ya Rais na idara nyingine za serikali ikiwemo bunge .

Ruto amesema serikali italazimika kuanza upya mchakato wa kutoa mapendekezo ya kukusanya fedha utakaohusisha wadau kutoka sekta mbali mbali .Katika kikao hicho rais Ruto alianza kwa kutaja baadhi ya hatua ambazo serikali imechukua tangu ilipotwa usukani kupunguza gharama ya maisha ikiwemo kupunguza bei ya unga,mbolea na mafuta ya kupikia .

Takriban watu 22 waliuawa katika maandamano ya Jumanne, kulingana na Tume ya Kitaifa ya Haki za Kibinadamu ya Kenya (KNHRC) inayofadhiliwa na serikali.

Bw Ruto alisema sasa ataingia kwenye mazungumzo na vijana hao ambao walikuwa mstari wa mbele katika maandamano makubwa zaidi kuwahi kutokea nchini tangu achaguliwe mwaka wa 2022.

"Baada ya kutafakari juu ya mazungumzo yanayoendelea kuhusu mswada wa fedha wa 2024 na kusikiliza kwa makini watu wa Kenya, ambao wamesema kwa sauti kubwa kwamba hawataki chochote kuhusiana na na mswada wa fedha wa 2024, nakubali na kwa hivyo sitatia saini mswada wa fedha wa 2024 na utaondolewa baadaye. Wananchi wamezungumza.” Alisema rais Ruto

Ghadhabu kuhusu mapendekezo ya serikali ya kukusanya kodi yalizua maandamano makali miongoni mwa Wakenya hasa vijana ambayo yalisababisha baadhi yao kufika bungeni na kuteketeza sehemu ya majengo ya bunge .Walikuwa pia wamehamakishw ana hatua ya wabunge ,wengi wao kutoka muungano unaotawala kupitisha mswada huo kwa hatua baada ya nyingine katika jitihada za kuufanya kuwa sheria .

No comments: