Wednesday, June 26, 2024

WAZIRI MKUU AZINDUA VITABU VYA HISTORIA YA BUNGE


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikata utepe wakati alipozindua vitabu vya Historia ya Bunge kwenye ukumbi wa Msekwa, bungeni jijini Dodoma, Juni 26, 2024. Wa pili kulia ni Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson, kushoto ni Naibu Spika Mussa Azzan Zungu na kulia ni Katibu wa Bunge, Nenelwa Mwihambi.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson wakionesha nakala za vitabu baada ya Waziri Mkuu kuzindua vitabu vya Historia ya Bunge kwenye ukumbi wa Msekwa, bungeni jijini Dodoma, Juni 26, 2024. Wa pili kushoto ni Naibu Spika wa Bunge, Mussa Azzan Zungu, kushoto ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maktaba ya Bunge, Mhandisi Stella Manyanya na kulia ni Katibu wa Bunge, Nenelwa Mwihambi.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea nakala za vitabu kutoka kwa Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson baada ya kuzindua vitabu vya Historia ya Bunge kwenye ukumbi wa Msekwa, bungeni jijini Dodoma
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza kabla ya kuzindua vitabu vya Historia ya Bunge kwenye ukumbi wa Msekwa, bungeni jijini Dodoma, Juni 26, 2024. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amezindua vitabu vya historia ya Bunge ambavyo vitasaidia kuhamasisha tafiti na kujua zaidi kuhusu mchango wa Bunge katika maendeleo ya jamii nchini.

Amesema kuwa vitabu hivyo pia vitakuwa kielelezo cha mafanikio na changamoto ilizopitia Bunge la Tanzania katika kudumisha demokrasia na utawala wa sheria. “Historia yetu ni sehemu ya mchango wetu kwa jumuiya ya kimataifa katika kukuza amani, utulivu na maendeleo.”

Amesema hayo leo (Jumatano, Juni 26, 2024) wakati wa uzinduzi wa vitabu viwili vya historia ya bunge katika ukumbi wa Pius Msekwa, Jijini Dodoma.Vitabu vilivyozinduliwa ni Kitabu cha Historia ya Bunge kutoka 1926-2024 na Wabunge wa Tanzania na nafasi zao kuanzia mwaka 1965-2023

“Kumbukumbu za historia ya Bunge zinaweza kuchochea utafiti wa kitaaluma na maendeleo ya nadharia za kisiasa na utawala. Watafiti wanaweza kutumia taarifa hizi kujenga ufahamu mpya na kupendekeza mifumo bora ya kisiasa.”

Kwa upande wake Spika wa Bunge Dkt. Tulia Ackson amepongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa sehemu ya maono ya bunge ikiwemo kuridhia kulikabidhi bunge maeneo yote yanayozunguka jengo la bunge.

“Tunatarajia kujenga makumbusho ya bunge ambayo yatakuwa ni makubwa kwa nchi nzima ili mtu anapokuja bungeni apate historia ambayo tumeipitia kama nchi lakini pia historia ya bunge letu”

No comments: