Sunday, October 13, 2024

MHE OTHMAN AKUTANA NA UJUMBE WA BODI YA WAKURUGENZI YA BARAZA LA TAIFA LA HIFADHI NA USIMAMIZI WA MAZINGIRA (NEMC)


Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman, amesema kwamba Zanzibar inatatizo kubwa la uharibifu wa mazingira linalohitaji jitihada za pamoja kati ya wadau, wahisani na washirika mbali mbali ili kuweza kulikabili ipasavyo na kupunguza athari zitokanazo na changamoto hiyo.

Mhe. Othman ameyasema hayo huko nyumbani kwake Chukwani Zanzibar alipofanya mazungunzo na Ujumbe kutoka Bodi ya Wakurugenzi ya Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), ulioongozwa na Mwenyekiti wake Profesa Esnati Osinde Chaggu.

Mhe. Othman amesema kwamba changamoto hiyo inayotokana na athari za mabadiliko ya tabia nchi ni vita kubwa ya kimazingira na ni jambo ambalo haliwezi kushughulikiwa ipasavyo pasipo jitihada za pamoja kati ya wadau, wahisani pamoja na wataalamu sambamba na kupatikana rasilimali za aina mbali mbali.
Amefahamisha kwamba maeneo mengi yameharibika na kwamba ni vigumu kwa Zanzibar pekee kwa nguvu za waliopewa dhamana ya usimamizi wa mazingira kuweza kuyarejeshea hali yake ya uasili pasipo na jitihada za pamoja kutoka ndani na nje ya nchi.

Mhe. Othman ameutaka uongozi wa Bodi hiyo kuhakikisha wanalichukua suala la changamoto ya uharibifu wa mazingira kwamba ni la wote hasa kwavile katika mtazamo wa kimataifa Tanzania ndio mlango wa wakutambuliwa.

Amesema kwamba hivi sasa zaidi ya maeneo 145 hapa Zanzibar yamehakabiliwa na changamoto kubwa ya kuharibika kimazingira ambapo jitihada za pamoja ndio njia nyepesi ya kusaidia kukabiliana na hali hiyo.

Akizungunzia tisho la uhaba wa maji kunakotokana na athari hizo, Mhe. Othman amesema kwamba Zanzibar kwa asilimia 100 inategemea vyanzo vya maji kutoka aridhini na kwamba hali hiyo kama haikuchukuliwa tahathari mapema upo uwezekano wa changamoto hiyo kuongezeka.

Amesema kwamba hali hiyo inaweza kuathiri pia sekta ya utalii ikizingatiwa kwamba Zanzibar hivi sasa inahoteli zaidi ya 600 za daraja tofauti ambapo mahitaji ya sekta hiyo , pasipo na hifadhi bora ya mazingira nayo inaweza kuathirika na pia idadi ya wageni wanaotembelea nchi inaweza kupungua iwapo mazingira hayaridhishi.

Ameishauri Bodi hiyo kwamba suala la mazingira ni fursa muhimu ya kuwezesha kufanya kazi pamoja kwa taasisi zilizopewa jukumu la usimamizi wa mazingira kati ya bara na Zanzibar ili juhudi hizo ziweze kufanikiwa.

Akizngunzia suala la ardhi , amesema kwamba sehemu kubwa ya ardhi inayohitajika kwa kilimo imepo Magharib mwa visiwa vya Unguja na pemba na kwamba tayari imeshatumika kwa shughuli za makazi ya binaadamu na kwamba ni masuala yanayoongeza changamoto ya athari za kimazingira Zanzibar.

Naye Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Profesa Isnati Osinde Chaggu , amesema kwamba chombo hiyo kimepewa jukumu na Mamlaka ya kutafiti , kufuatilia pamoja na mambo mengine kuhakikisha kwamba masuala yote ya mazingira nchini Tanzania yanasimamiwa kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa.

Amesema kwamba mabadiliko ya taibia nchi yanahitaji kila juhudi katika kuhakikisha kwamba athari zinazotokana na tatizo hilo haziongezeki hasa kwa vile masuala ya tabia nchi hayana mipaka zaidi ya kukabiliwa kwa juhudi za pamoja.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Bodi hiyo Immaculate Sware Semesi, amesema kwamba suala la uchumi wa bluu, mafuta na gesi asilia linalohusisha masuala ya sera ya uchumi wa matumizi ya rasilimali ya bahari kwa wananchi na taifa kwa jumla halina mipaka kutoka pande zote za muungano na kwamba linahitaji kusimamiwa kwa juhudi za pande zote mbili.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira Zanzibar Sheha Mjaja Juma, amesema kwamba ofisi yake inaendelea kujenga mashirikiano na wenzao wa Tanzania Bara katika kuhakikisha kwamba suala la mazingira linasimamiwa ipasavyo nan chi inaendelea kuwa salama.




Imetolewa na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar kupitia ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar leo Jumamosi tarehe 12. Oktoba 2024.

No comments: