Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imefanikisha zoezi kubwa la kuteketeza dawa za kulevya zenye uzito wa jumla ya kilo 4,402.02. Zoezi hilo limefanyika Oktoba 3, 2025, katika kiwanda cha saruji cha Twiga kilichopo Wazo, jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa ya DCEA iliyosomwa na Kamishna Jenerali Aretas Lyimo, dawa zilizoteketezwa ni pamoja na kilo 2,168.18 za methamphetamine, kilo 1,064.29 za heroin, gramu 326.95 za cocaine, kilo 515.48 za bangi na kilo 653.74 za mirungi. Zote zilikuwa sehemu ya vielelezo vya mashauri mbalimbali yaliyopo mahakamani; baadhi yakiwa tayari yametolewa hukumu na mengine yakiendelea kusikilizwa.
Miongoni mwa mashauri yanayohusiana na dawa zilizoteketezwa ni kesi ya Najim Abdallah Mohamed iliyohusisha heroin kilogramu 882.71 na methamphetamine kilogramu 2,167.29. Aidha, mashauri yaliyotolewa hukumu ni Pamoja na ya Hassan Azizi aliyepatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo cha maisha, Salum Shaaban Mpangula aliyehukumiwa kifungo cha maisha, Hemed Juma Mrisho maarufu kwa jina la “Hororo” aliyehukumiwa kifungo cha maisha, Ramadhan Shaban Gumbo aliyehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela, Irene Dickson Mseluka aliyehukumiwa miaka mitano jela na Gema Victor Mmasy aliyehukumiwa miaka mitatu jela.
Akizungumza wakati wa tukio hilo, Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, alisema mamlaka itaendelea kushirikiana na wadau wote kuhakikisha vita dhidi ya dawa za kulevya inafanikiwa. Aidha, alisisitiza kuwa DCEA haitabaki katika hatua za kisheria pekee, bali pia itatoa nafasi kwa wale wanaojihusisha na biashara hiyo kuachana nayo kwa hiari.
“Tunatoa msamaha kwa wauzaji wa dawa za kulevya watakaoamua kukiri na kuacha. Hatutachukua hatua yoyote dhidi yao, bali tutashirikiana nao ili kufichua mbinu zinazotumika kuficha na kusambaza dawa hizi,” alisema Lyimo.
Kutokomeza zaidi ya tani nne za dawa za kulevya ni hatua kubwa katika kupunguza athari zinazotokana na biashara haramu ya dawa za kulevya nchini. Tukio hili linadhihirisha dhamira ya DCEA kuhakikisha jamii inalindwa dhidi ya madhara ya dawa hizo ambazo zimekuwa zikiathiri afya, uchumi na usalama wa taifa.
No comments:
Post a Comment