ANGALIA LIVE NEWS

Friday, June 5, 2026

FURSA ZA KIUCHUMI TANZANIA NA URUSI, AIR TANZANIA KUANZA SAFARI ZA MOJA KWA MOJA DAR/ZANZIBAR -MOSCOW



RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ambaye yupo nchini Urusi kwa ziara maalum, amebainisha kuwa, kuanzia Julai 2026, Kampuni ya Ndege ya Tanzania (ATCL) itaanza safari za moja kwa moja kati ya Dar es Salaam, Zanzibar na Moscow. 

Ambapo amesema hatua hio muhimu itaimarisha zaidi utalii, biashara na uwekezaji, na kufungua ukurasa mpya katika historia ya uhusiano na ushirikiano kati ya Tanzania na Urusi.

Amesema:

"Nikihitimisha ziara yangu ya Kitaifa katika Shirikisho la Urusi, leo pamoja na mambo mengine nimepata fursa ya kuhutubia Jukwaa la Biashara kati ya Tanzania na Urusi pamoja na Jukwaa la 29 la Kimataifa la Uchumi la St. Petersburg (SPIEF), ambayo yamekutanisha viongozi, wataalamu wafanyabiashara na wawekezaji kutoka mataifa mbalimbali.

Nimewahakikishia wawekezaji kuwa Tanzania ni sehemu salama na bora kwa mitaji yao, tukijivunia mazingira wezeshi ya kisheria, amani na utulivu, miundombinu bora, ukuaji imara wa uchumi, uwepo wa nguvu kazi na fursa ya kufikia soko la zaidi ya watu milioni 500 ukanda wa Mashariki na Kusini mwa Afrika.

Pia, nimebainisha sekta za kimkakati ambazo ni kipaumbele katika uwekezaji zikijumuisha madini, kilimo, nishati safi, mafuta na gesi, afya pamoja na usafiri na usafirishaji." Amesema.





No comments: