ANGALIA LIVE NEWS

Friday, June 5, 2026

NI TANAPA TENA: YANG’ARA KITAIFA, YABEBA TUZO YA UBORA WA HUDUMA ZA UMMA



Na. Catherine Mbena - Dar es Salaam.


Ubora wa huduma, utekelezaji wa *ISO 9001:2015* na kuridhika kwa wateja vyaiwezesha TANAPA kushika nafasi ya pili kitaifa katika Tuzo za Ubora wa Taifa (National Quality Award 2025/2026).

*DAR ES SALAAM*: Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) limeandika historia nyingine mjarabu baada ya kutunukiwa Cheti cha Ushindi wa Pili (First Runner-Up) katika Tuzo za Ubora wa Taifa 2025/2026, tuzo zinazoratibiwa na kutolewa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kwa lengo la kutambua taasisi zinazofanya vizuri katika utoaji wa huduma na kuzingatia viwango vya ubora.

Tuzo hiyo iliyotolewa leo juni 5, 2026 katika Jukwaa la Biashara la Viwango (Standards Business Forum) lililofanyika jijini Dar es Salaam katika Ukumbi wa Mlimani City, ambapo TANAPA iling’ara katika kipengele cha “Mtoa Huduma Bora wa Umma wa Mwaka”, ikiibuka mshindi wa pili miongoni mwa taasisi zilizofanya vizuri zaidi nchini katika utoaji wa huduma kwa watalii na wageni mbalimbali wanaotembelea maeneo yao yenye tunu za Taifa.

Mafanikio hayo yanaonesha hatua kubwa iliyofikiwa na TANAPA katika kuimarisha ubora wa huduma, kuongeza ufanisi wa utendaji kazi na kuhakikisha wateja wake ambao ni watalii, wanapata huduma zinazokidhi viwango vya kitaifa na  kimataifa. 

Tangu mwaka 2022, TANAPA imekuwa ikitekeleza Mfumo wa Usimamizi wa Ubora wa ISO 9001:2015, ambao umechangia kuimarisha usimamizi wa shughuli zake, kuongeza uwajibikaji na kujenga utamaduni wa maboresho endelevu kwa kila huduma inayotoa ndani ya Hifadhi za Taifa 21 inayozisimamia.

Akizungumza kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi TANAPA baada ya kupokea tuzo hiyo, Afisa Mhifadhi Mkuu Eunice Msangi, alisema kuwa ushindi huo ni matokeo ya juhudi za pamoja za Menejimenti na watumishi wa TANAPA katika kuhakikisha huduma zinazotolewa zinakizi matarajio na matamanio ya wateja na wadau wake.

Aidha, Mhifadhi huyo aliongeza; “Ushirikiano mkubwa kutoka kwa wadau wa sekta ya Uhifadhi na Utalii pia wamechangia kwa kiasi kikubwa mafanikio hayo. Tuwaahidi wateja wetu na wadau mbalimbali TANAPA itaendelea kuboresha huduma zake ili kuongeza uzoefu mzuri kwa wageni na kuchochea ukuaji wa sekta ya utalii nchini”.

Ushindi huo unaongeza hadhi ya TANAPA kama taasisi ya umma iliyojizatiti kutoa huduma bora na kuendeleza dhamira yake ya kusimamia kwa weledi rasilimali za Taifa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.







No comments: