Na. Mwandishi Wetu, Dar.
Mgeni Rasmi, Waziri Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Prof. Riziki Shemdoe (Mb);
Pamoja n wageni wengine: Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Michezo na Utamaduni Mhe. Husna Sekiboko, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Daniel Mushi;
Walimu; Wanafunzi; Wageni waalikwa;
Mabibi na Mabwana.
"Jamhuri ya Muungano wa Tanzania!
"Ufundishaji bora________ Taifa imara"
Aidha, kwa niaba ya Menejimenti ya Taasisi ya Elimu Tanzania ambayo ndiyo mwendeshaji wa shindano hili na mwandazi wa hafla hii ninawakaribisha nyote katika Duru ya Nne ya hafla ya Utoaji wa Zawadi kwa washindi wa shindano la Taifa la Nne la Stadi za Ufundishaji kwa walimu wa Elimu ya Awali na Msingi na Duru ya pili ya Utoaji wa Zawadi kwa washindi wa shindano la Taifa la Pili kwa walimu wa Sekondari.
Pili, kipekee kabisa nakushukuru sana wewe binafsi Mhe. Mgeni Rasmi kwa kukubali kuwa Mgeni Rasmi wa hafla hii muhimu ya Utoaji wa Zawadi kwa Washindi wa Shindano la Taifa la Stadi za Ufundishaji kwa Walimu wa Elimu ya Awali, Msingi na Sekondari.
Ninawashukuru sana wafadhili na wadau mbalimbali waliowezesha kufanikisha shindano hili. Kwa Heshima ninaomba niwatambue na niwatambulishe kwako kama ifuatavyo:
Kwanza Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia nchini Tanzania, Ndugu Firas Raad, pamoja na wawakilishi wengine kutoka Benki ya Dunia. Tunawashukuru sana kwa kuwezesha shindano hili.
Pili, Shirika la Educate; kwa kuiwezesha TET kuwa na mfumo mahususi wa kidijitali kwa ajili ya kuendesha shindano hili (National Teaching Skills Competitionb System Skills), pamoja na mchango wenu katika kufanikisha ufundishaji na ujifunzaji wa Somo loa Elimu ya Biashara, uendeshaji wa shindano hili kwa walimu wa Somo la Elimu ya Biashara na na utoaji wa Zawadi kwa washindi wote wa Somo la Elimu ya Biashara.
Shirika la Enabel kwa kuwezesha upatikanaji wa zawadi za kompyuta Mpakato Tisa kwa washindi wa elimu ya Sekondari katika masomo ya STEM. Mchango wenu utaendelea kuhamasisha matumizi ya TEHAMA na ubunifu katika elimu.
Project Zawadi kwa kutoa zawadi za kompyuta mpakato Tisa. Mchango wenu ni chachu muhimu katika kukuza ari ya ushiriki na ubunifu wa walimu katika ufundishaji Shuleni.
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa ukarimu na ushirikiano wenu na kwa kufadhili hafla hii kwa kupunguza bei halisi ya ukumbi huu ambayo imekuwa ni sehemu ya uthamini wa shindano hili.
Shindano la taifa la Stadi za Ufundishaji kwa Mwaka 2026 ni la nne kwa walimu wa Elimu ya Awali na Msingi, na la pili kwa walimu wa Elimu ya Sekondari na limejumuisha halmashauri zote 184 za Tanzania Bara.
Kwa ngazi ya Elimu ya Awali, shindano hili limejikita katika kuimarisha umahiri wa stadi za awali za kusoma, hususan ufundishaji wa sauti za herufi ambazo zimekuwa zikileta changamoto kwa wanafunzi katika kuzitamka kwa usahihi pamoja na kuzitumia katika kuunda silabi na maneno sahihi.
Kwa ngazi ya Elimu ya Awali, lengo la shindano ni kutatua changamoto za ufundishaji na ujifunzaji wa stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK), ili kuhakikisha wanafunzi wanamudu stadi hizo muhimu wanapofikia Darasa la Tatu.
Eneo hili la ushindani iinaunga mkono maono na mikakati ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuhakikisha kuwa watoto wote wanapata wanaweza kusoma kwa ufasaha wanapofikia Darasa la Tatu.
Katika Elimu ya Msingi, shindano hili lilijikita katika Darasa la Kwanza kupitia umahiri wa somo la Kiingereza wa “Demonstrate mastery of basic English language skills”, Umahiri huu uliteuliwa kwa makusudi ili kuendelea kutatua changamoto zinazojitokeza katika ufundishaji na ujifunzaji za stadi za awali za lugha ya Kiingereza, hususan katika matamshi sahihi ya sauti za konsonanti na irabu.
Kwa upande wa Elimu ya Sekondari, shindano lilihusisha masomo yafuatayo:
Somo la ‘Physics’ limehusisha shughuli mahususi ya Describe the concept of motion under gravity; Somo la ‘Mathematics’, shughuli mahususi ya Recognising the point of intersection of two linear equations;
Somo la ‘Computer Science’ shughuli mahususi ya Create an algorithm for a familiar real-life problem; na
Somo la ‘Business Studies’ katika shughuli mahususi ya explain how to establish a startup, specifically a sole proprietorship.
Maandalizi ya shindano hili yalianza kwa wakuza mitaala wa TET kubainisha maeneo ya ushindani kwa kutumia taarifa za uchambuzi wa majibu ya watahiniwa inayotolewa na Baraza la Mitihani Tanzania (CIRA) pamoja na kubainisha maeneo ambayo ni mapya klatika mtaala. Baada ya maeneo haya kubainisha tangazo rasmi la shindano liliandaliwa na kusambazwa kupitia OWM TAMISEMI. Tangazo liliwataka walimu kuandaa andalio la somo la kipindi na kujirekodi akifundisha katika kipindi chenye urefu wa kati ya dakika 10-15. Kisha mwalimu alipaswa kujisajili katika mfumo wa kidijitali unaoitwa National Teaching Skills Competition System na kisha kupakia andalio la somo na video.
Mfumo huu ulimpa mrejesho mwalimu iwapo video yake imepokelewa na katika ngazi zote za tathimini kuanzia ngazi ya halmashauri hadi taifa.
Kupitia mfumo huu Jumla ya walimu 3,153 walijisajili lakini waliofanikiwa kupakia video kwa ajili ya tathimini ngazi ya halmashauri/wilaya walikuwa ni 1,263 sawa na asilimia 40. Baada ya video kupokelewa tathmini ilifanyika katika ngazi tatu: ngazi ya halmashauri, mkoa na Taifa kupitia mfumo kwa kuzingatia vigezo vya ushindani vilivyoandaliwa awali na majaji. Majaji walitakiwa kujisajili katika mfumo na kufanya tathimini katika ngazi husika, na kila jaji aliweza kuona video katika ngazi anayotathimini tu. Vigezo vya tathimini vilikuwa ni pamoja na maudhui kuakisi umahiri lengwa, mtiririko wa somo, matumizi ya mbinu shirikishi, matumizi ya TEHAMA, matumizi ya zana, ukuzaji wa stadi za karne ya 21 sanjari na matumizi ya upimaji endelevu katika mchakato wa ufundishaji na ujifunzaji.
Katika ngazi ya halmashauri, video 1,263 zilifanyiwa tathimini na kati ya hizo video 751 ndiyo zilichaguliwa kuendelea na mchakato wa shindano katika ngazi ya mkoa. Kati ya Video 751 zilizowasilishwa katika ngazi ya mkoa video 232 ziliteuliwa kuendelea na shindano katika ngazi ya Taifa. Aidha, kati ya Video 232 zilizowasilishwa, video 35 ndizo zilizoshinda katika tathmini ya Taifa na hivyo washiriki 35 ndio walioshinda ngazi ya Taifa na hawa walifanya ufundishaji wa ana kwa ana mbele ya majaji wa ngazi ya taifa kwa ajili ya tathmini ya mwisho ili kupata mshindi wa kwanza hadi wa tano kwa kila eneo.
Washindi hao watano kwa kila umahiri ndio tunaowatunukia zawadi katika hafla ya leo Juni 6, 2026.
Majaji katika shindano hili walikuwa ni wahadhiri wa vyuo vikuu, wakufunzi wa vyuo vya ualimu, wathibiti ubora wa shule na wakuza mitaala wa TET. Kwa nafasi hii ninawashukuru sana majaji wote wa shindano hili kuanzia ngazi ya halmashauri mpaka taifa kwa kufanya kazi kwa weledi mkubwa hatimaye kupata washindi bora wa shindano letu.
Hakika, mchakato wa tathmini ulifanyika kwa weledi na umakini mkubwa katika kuhakikisha kuwa kila mwalimu anatendewa haki.
Uzingativu vigezo vya tathimini na matumizi ya mfumo wa kijigidital katika tathmini hii vinathibitisha uhalali na uthabiti wa matokeo ya washindi wa shindano hili kwa mwaka 2026.
Washindi watapewa zawadi kulingana na nafasi zao za ushindi kama ifuatavyo:
(a) Mshindi wa kwanza kwa kila nyanja atapata fedha taslimu Tsh 2,500,000/=, Cheti cha Pongezi, Cheti cha Ushindi na Kompyuta Mpakato moja. Shule anayofundisha itapata Projekta.
Vilevile, shule zilizotoa mshindi wa kwanza katika maeneo ya Kusoma kwa Darasa la Awali, Kiingereza kwa Darasa la Kwanza, Ufaraguzi wa Zana kwa Darasa la Pili zitapata vibao vya kielektroniki (Electronic Pad) 100 vyenye thamani ya Shilingi 5,000,000/=.
Aidha, video zote za washindi wa nafasi ya kwanza zitarekodiwa upya katika studio za TET na kupakiwa kwenye Mfumo wa Elimu wa Kidijitali (LMS) pamoja na kurushwa kupitia TET Soma Kwanza TV ili kuwapa nafasi walimu wote nchini kujifunza.
(b) Mshindi wa Pili- atapata Shilingi 2,000,000/=, Cheti cha Pongezi, Cheti cha Ushindi na Kompyuta Mpakato na Shule anayofundisha itapata Projekta.
(c) Mshindi wa Tatu- Shilingi 1,500,000/=, Cheti cha Pongezi, Cheti cha Ushindi na Kompyuta Mpakato na Shule anayofundisha itapata Projekta.
(d) Mshindi wa Nne- Kompyuta Mpakato na Cheti cha Pongezi.
(e) Mshindi wa Tano - Kompyuta Mpakato na Cheti cha Pongezi.
Shindano hili lina nafasi muhimu katika kuimarisha Mafunzo Endelevu ya Walimu Kazini (MEWAKA) kwa kuwa linatoa fursa kwa walimu kujifunza kwa vitendo, kuonesha umahiri, kubadilishana uzoefu, na kuendelea kujiendeleza kitaaluma wakiwa kazini. Kupitia shindano hili, walimu hujifunza kutoka kwa wenzao, huibua mbinu bunifu za ufundishaji, na kuimarisha matumizi ya mbinu shirikishi, upimaji, TEHAMA pamoja na matumizi ya zana za kufundishia na kujifunzia.
Aidha, shindano hili linaifanya MEWAKA kuwa ya vitendo zaidi kwa kuwa maarifa, uzoefu na bunifu zinazozalishwa kupitia shindano hili hurekodiwa, kuhifadhiwa na kusambazwa kupitia majukwaa ya kujifunzia kama MUK/LMS na TET Soma Kwanza TV, hivyo kuwafikia walimu wengi zaidi nchini. Kwa msingi huo, shindano hili limeendelea kuwa chachu muhimu ya kujenga utamaduni wa kujifunza endelevu, kuimarisha umahiri wa walimu, na kuinua ubora wa ufundishaji na ujifunzaji nchini.”
Nimalizie kwa kuwapongeza walimu wote walioshiriki katika shindano hili kwa mwaka huu 2026. Aidha, Ninawashukuru sana vongozi wote wa wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI kwa miongozo na usimamizi katika kutekeleza afua za TET kupitia ya miradi wa BOOST na SEQUIP.
Ninawashukuru pia waratibu wote wa mradi wa BOOST na SEQUIP kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI na TET kwa kuratibu utekelezaji wa afua hii ya shindano kupitia miradi hii. Kwa namna ya pekee Ninakushukuru sana wewe Mgeni Rasmi kwa kutenga muda wa kuja kuwa mgeni rasmi katika hafla hii muhimu." Dkt. Aneth Komba.














No comments:
Post a Comment