Na. Calvin Katera - Babati.
Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) imekutana na wadau wa utalii na uhifadhi ili kusuka mikakati itakayochagiza ongezeko la watalii na kuridhika kwa wageni watakaotembelea Hifadhi ya Taifa Tarangire. Mikakati hiyo imefanyika leo Juni 03, 2026 katika kikao cha pamoja kilichofanyika katika hifadhi hiyo inayosifika kwa tembo wengi na wakubwa nchini Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla.
Kikao hicho ni hatua ya maandalizi kuelekea msimu mpya wa utalii (High season) unaoanza mwezi Juni hadi mwishoni mwa mwezi Januari kila mwaka.
Katika kikao hicho Mkuu wa Kanda ya Kaskazini, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi Dkt. Beatrice Kessy alieleza kuwa wadau na wawekezaji kwa kushirikiana na hifadhi wanapaswa kutoa huduma bora zitakazoongeza hamasa na kuridhika kwa wageni ili waende kuisemea vizuri hifadhi na Taifa kwa ujumla. Kama inavyojulikana katika soko la utalii mgeni anaporidhika kwa huduma na mapokezi mazuri anaporudi nchini kwake huwa ni balozi mzuri kwa yale mema aliyofanyiwa.
Sambamba na hilo Kamanda Kessy aliongeza; “Hifadhi ya Taifa Tarangire imeboresha miundo mbinu ya barabara na malazi. Aidha, ikolojia imeendelea kuimarishwa ili wanyamapori wapate malisho ya kutosha na wanyama waonekane kwa urahisi, kwani malisho yanapokuwa mengi wanyamapori hawatembei umbali mrefu hivyo kuwawezesha watalii kuona wanyama wote waliowakusudia katika safari yao.
Kwa upande wake, Bw. Loseku Dorop kutoka Kampuni ya Conserve Safari alieleza kuwa wadau wa utalii wawekeze nguvu katika matumizi ya nishati safi, vitambulisho kwa watoa huduma wa makampuni ya kitalii na usafi wa mazingira kwa kuepuka kurusha taka, kwani taka huathiri mazingira na wanyamapori.
Kwa upande wake Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Tarangire Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Dkt. Tutindaga George alieleza kuwa licha ya hifadhi hiyo kushika nafasi ya tatu kwa mapato na wingi wa watalii, mikakati yao ni kuwa ya pili au ya kwanza kuzipiku Hifadhi za Taifa Serengeti na Kilimanjaro.
Kikao hicho mbali na kuweka mikakati kuelekea msimu mpya wa utalii pia ni utaratibu wa hifadhi hiyo kukumbushana kanuni na taratibu mbalimbali za uhifadhi na kuwahamasisha wadau hao kuendesha utalii endelelevu kwa maslahi yao binafsi na maslahi ya Taifa kwa ujumla.







No comments:
Post a Comment