ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, June 23, 2026

TEMBO: MHANDISI WA ASILI ANAYEWAWEZESHA WENGINE KUISHI


📍Je, akitoweka nani ataendeleza kazi yake?


Na. Beatus Maganja,

+255 676 475 541.

Tembo ni mnyama wa aina gani?! Je mnyama huyu ana faida gani katika sayari hii tuliyomo?!  Kwanini Tanzania inajivunia kuwa na tembo?!  Kwanini mikataba ya kimataifa inamlinda tembo?!! Kwanini tembo, kwanini? Nauliza kwanini ?!!

Haya ni maswali, maswali yanayosumbua fikra za binadamu, ambapo  Kwa wengi wetu tukimtazama tembo, tunamwona ni mnyama mkubwa mwenye nguvu nyingi, anayepita porini aking'oa miti na wakati mwingine kuingia mashambani kusababisha uharibifu na hata kuleta madhara kwa binadamu. Lakini kuna swali ambalo wengi wetu hatujawahi kujiuliza, kwamba Je, nyuma ya ukubwa wake huo, athari zake kuna kazi gani kubwa anayoifanya kwa manufaa ya viumbe wengine na hata binadamu? 

Ukweli ni kwamba tembo si mnyama wa kawaida. Ni mnyama mwenye maajabu mengi ambayo watafiti walitumia miongo kadha wa kadha kuvumbua . Hivi umewahi kujua  kuwa tembo ni mhandishi kwa asili yake?!! Naam, tembo ni mhandisi wa mazingira ambaye kazi zake zinawezesha maisha ya maelfu ya viumbe kuendelea kuwepo kila siku katika sayari ya dunia.

Fikiria msitu mkubwa uliokauka wakati wa kiangazi. Mito imepungukiwa  maji, mabwawa yamekauka na viumbe wengi wako katika hatari ya kufa kwa kiu. Katika mazingira hayo magumu, anaibuka mnyama tembo ambaye kwa kutumia meno na miguu yake anachimba maeneo yenye unyevunyevu hadi maji yatoke ardhini. Anapomaliza kunywa na kuondoka, swala, pundamilia, nyani, ndege na viumbe wengine wengi huja kutumia maji hayo. Bila kujua, tembo huwa ameokoa maisha ya mamia ya viumbe ambao hawana uwezo wa kufanya kazi hiyo.

Si hivyo tu. Tembo anapotembea mamia ya kilomita kutafuta chakula, hubeba mbegu za miti mingi kupitia kinyesi chake na kuzisambaza maeneo mbalimbali. Mbegu hizo huota na kuwa miti mipya. Miaka inapopita, miti hiyo hugeuka kuwa misitu inayovutia mvua, kuhifadhi maji na kutoa hewa safi tunayovuta kila siku. Kwa lugha rahisi, tembo ni mpandaji miti wa asili ambaye hafanyi kampeni wala kutafuta sifa wala kutambuliwa, lakini matokeo ya kazi yake yanaonekana kwa vizazi vingi.

Katika misitu minene, tembo amekuwa akifungua njia kwa kuvunja matawi na kusafisha mapito. Njia hizo hutumiwa na wanyama wengine kutafuta chakula, maji na maeneo salama ya kuishi. Hata mbegu zinazoota ardhini hupata nafasi ya kukua kwa sababu mwanga wa jua hupenya kwenye maeneo aliyopita. Hivyo, tembo si mnufaika wa mazingira pekee; bali ni mmoja wa watengenezaji wakuu wa mazingira hayo.

Jambo ambalo wengi hatulioni ni kwamba faida za tembo hazibaki porini tu. Maelfu ya watalii kutoka duniani kote huja Tanzania kushuhudia uzuri wake. Wageni hao huacha fedha zinazochangia uchumi wa Taifa, kuongeza ajira kwa vijana na kusaidia ukuaji wa biashara mbalimbali katika jamii zinazozunguka maeneo ya hifadhi. Kwa namna hiyo, tembo anageuka kuwa daraja linalounganisha uhifadhi wa mazingira na maendeleo ya wananchi.

Sasa, hebu tufikirie kwa undani zaidi. Kama tembo wote wangetoweka leo, nani angechimba visima vya asili wakati wa ukame? Nani angesambaza mbegu za maelfu ya miti kwa umbali mkubwa kiasi hicho? Nani angeendelea kufungua njia za asili zinazotumiwa na viumbe wengine porini? Ukweli ni kwamba baadhi ya kazi anazozifanya tembo haziwezi kufanywa kwa ufanisi uleule na mnyama mwingine yeyote.

Ndiyo maana tunapomtazama tembo, tusione ukubwa wake pekee wala tusikumbuke madhara yake pekee. Tumuone kama mhandisi wa mazingira/ikolojia, mzalishaji wa misitu, mtoa maji kwa viumbe wengine na mshirika muhimu wa maisha duniani. Kadiri tunavyozidi kumwelewa, ndivyo tutakavyogundua kuwa tembo si mzigo wa mazingira, bali ni moja ya zawadi kubwa ambazo asili imeikabidhi Tanzania, na Mungu ameitunuku  dunia kwa ujumla wake 

Endelea kubaki katika kurasa za TAWA  ujifunze mengi kuhusu wanyamapori na faida zao kwetu. Tchao!!

#tawatzanzania #tumerithishwa #tuwarithishe

No comments: