ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, June 6, 2026

TFS YAELIMISHA WAVUNAJI RUFIJI, YASISITIZA UVUNAJI HALALI WA MAZAO YA MISITU



Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Kanda ya Mashariki umeendelea kuimarisha usimamizi wa rasilimali za misitu kwa kutoa elimu kwa wavunaji na wafanyabiashara wa mazao ya misitu katika Wilaya ya Rufiji, huku wadau wa sekta hiyo wakiomba kuboreshwa kwa mfumo wa usajili ili kurahisisha shughuli zao za biashara.


Akizungumza katika kikao cha elimu kwa wadau hao Juni 03,2026, Mhifadhi Mkuu wa TFS Kanda ya Mashariki, Mkama Kusaga, alisema mafunzo hayo yanalenga kuongeza uelewa wa sheria, kanuni na taratibu za uvunaji na biashara ya mazao ya misitu ili kuhakikisha shughuli hizo zinafanyika kwa kuzingatia misingi ya matumizi endelevu ya rasilimali za misitu.

Alisema kabla ya kuanza uvunaji, wafanyabiashara na wavunaji wanapaswa kuwasilisha maombi katika vijiji husika, kupata idhini kutoka mamlaka zinazotambulika na kuhakikisha wanamiliki vibali vyote vinavyotakiwa kisheria.

“Tunataka wadau wote wafahamu na kuzingatia taratibu zilizowekwa ili rasilimali za misitu ziendelee kunufaisha wananchi na Taifa kwa ujumla bila kuhatarisha uendelevu wake,” alisema Kusaga.

Aliongeza kuwa uzingatiaji wa sheria na kanuni za misitu utasaidia kupunguza migogoro, kudhibiti uvunaji haramu na kuimarisha uhifadhi wa mazingira.

Wakichangia mjadala katika kikao hicho, baadhi ya wafanyabiashara walieleza kuridhishwa na elimu iliyotolewa na TFS, wakisema imewapa uelewa mpana wa wajibu wao katika kulinda rasilimali za misitu wakati wa kutekeleza shughuli za biashara.

Hata hivyo, waliomba serikali kuangalia uwezekano wa kuwa na mfumo wa usajili unaowaruhusu kujisajili mara moja katika ngazi ya wilaya badala ya kufanya usajili katika kila kijiji wanachofanyia biashara, wakidai hatua hiyo itapunguza urasimu na gharama za uendeshaji wa shughuli zao.

Akizungumza kwa niaba ya wafanyabiashara hao, Mussa Maganga alisema pamoja na kupongeza juhudi za TFS za kutoa elimu, bado kuna haja ya kuimarisha ushirikiano kati ya wafanyabiashara na watumishi wa serikali ili kurahisisha utekelezaji wa shughuli zinazofanyika kwa mujibu wa sheria.

“Tunathamini elimu hii kwa sababu imetupa mwanga kuhusu taratibu za sekta ya misitu. Tunatarajia kuona maboresho zaidi katika usajili na kuendelea kujenga ushirikiano mzuri na TFS,” alisema.

TFS imeendelea kusisitiza kuwa ushiriki wa wadau katika kuzingatia sheria na kanuni za misitu ni muhimu katika kulinda rasilimali za Taifa na kuhakikisha sekta hiyo inaendelea kuchangia ukuaji wa uchumi na ustawi wa jamii kwa vizazi vya sasa na vijavyo.









No comments: