DODOMA. Serikali imeendelea kuimarisha udhibiti wa ununuzi wa umma kwa kuhakikisha michakato ya ununuzi inafanyika kupitia mifumo ya kielektroniki, hatua inayolenga kuongeza uwazi, uzingatiaji wa sheria za ununuzi wa umma, uwajibikaji na thamani ya fedha za umma.
Akizungumza leo, Jumanne, Septemba 15, 2026, katika programu ya kuwaelekeza watumishi wapya wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) jijini Dodoma, Kamishna Msaidizi Mwandamizi na Meneja wa Kitengo cha Usimamizi wa Ununuzi na Ugavi, SACC Fridolin Matembo, alisema matumizi ya mifumo ya kidijitali yameendelea kubadilisha usimamizi wa michakato ya ununuzi serikalini ili kuendana na mabadiliko ya sheria, miongozo na maelekezo ya Serikali.
Matembo alisema Mfumo wa Kitaifa wa Ununuzi wa Kielektroniki (NeST) umewekwa ili kuhakikisha michakato ya ununuzi inafanyika ndani ya mfumo huo, kuanzia hatua za awali za kuandaa mpango wa ununuzi hadi utekelezaji wa mikataba, hatua inayopunguza utegemezi wa nyaraka za kawaida na kuongeza uwezo wa kufuatilia michakato ya ununuzi.
Alisema mfumo huo pia unaongeza uwajibikaji kwa watendaji kwa kuwa michakato inayofanyika kupitia mfumo inaweza kufuatiliwa na kukaguliwa, hivyo kuwataka watumishi kuzingatia sheria, taratibu na maadili ya utumishi katika kutekeleza majukumu yao.
Kwa upande wa TFS, Matembo alisema ununuzi ni shughuli mtambuka inayogusa maeneo mbalimbali ya utekelezaji wa majukumu ya taasisi, ikiwemo shughuli za uhifadhi na upandaji miti, zinazohitaji upatikanaji wa bidhaa na huduma mbalimbali kupitia michakato halali ya ununuzi.
Alisema kutokana na ukubwa wa TFS na uwepo wake katika maeneo mbalimbali nchini, matumizi ya mifumo thabiti ya ununuzi ni muhimu katika kuhakikisha taasisi inapata thamani ya fedha, inatekeleza mipango yake na kutumia rasilimali kwa kuzingatia malengo ya Serikali.
Matembo pia aliwataka watumishi wapya kuendelea kujifunza na kushirikiana na wataalamu wa ununuzi katika vituo watakavyopangiwa, huku wakihakikisha michakato ya ununuzi inaanzishwa kwa wakati na kuendana na bajeti pamoja na mipango kazi iliyoidhinishwa.




No comments:
Post a Comment