Saturday, February 13, 2010

Mafisadi wa elimu waitwa kukaguliwa vyeti

Mawaziri wanaodaiwa kughushi vyeti vya taaluma (mafisadi wa elimu) na wengine wanaotiliwa shaka wamepewa nafasi ya kuwasilisha vyeti vyao kwenye Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) ili kuthibitishwa na kuondoa utata katika jamii juu ya uhalali wa shahada zao, hasa walizozipata nje ya nchi.

Tamko hilo la (TCU) linakuja siku moja baada ya Spika wa Bunge, Bw. Samuel Sitta kumtakasa Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Dkt. David Mathayo kuwa elimu yake haina utata, hivyo watu waache kumzongazonga, lakini hakugusia vigogo wengine wanaodaiwa kuwa na ama vyeti feki au kusoma kwenye vyuo visivyotambulika.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Katibu Mtendaji wa TCU, Prof. Mayunga Nkunya alisema kuwasilisha vyeti TCU ndio njia itakayosaidia kuondoa minong'ono miongoni mwa jamii.

"Tume ingependa kusisitiza kuwa ili kuondoa utata katika jamii (juu) ya uhalali wa shahada za digrii alizonazo Mtanzania yeyote, hasa kutoka nje ya nchi, ni vizuri wahusika wakaleta vyeti vyao kwenye Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania ili viweze kuthibitishwa uhalali wake na hivyo kuondoa minong'ono miongoni mwa jamii," alisema Profesa Nkunya.

Aliongeza kuwa iwapo TCU italetewa vyeti vyenye utata, itavifanyia tathmini kubaini uhalali wake au uhalali wa taaluma husika, kulingana na taratibu za kisheria zilizopo.

Pia tume hiyo imewashauri Watanzania kuendelea kutaka ushauri kutoka kwake endapo wana nia ya kujiunga na masomo kwenye vyuo nje ya nchi...ili kuepusha wasijiunge na vyuo batili au bandia ambavyo havitambuliwi kiithibati, na hivyo kupata vyeti na taaluma zisizotambuliwa.

Wakati huo huo, TCU imekana kupokea taarifa zinazohusiana na vyeti vya Dkt. Mathayo ili kutambua uhalali au ubatili wake na kuwa maamuzi ya Spika Sitta kumtangaza ndani ya bunge kuwa ana elimu isiyo na mashaka ni kuingiliwa kwa madaraka yake.

Hatua hiyo imekuja kutokana na kitendo cha mwanaharakati wa 'Ufisadi wa Elimu', Bw. Kainerugaba Msemakweli kuwataja baadhi ya mawaziri wa serikali ya awamu ya nne, ambacho kimeelezwa na TCU kuwa pia ni ukiukaji wa sheria.

Akizungumzia kitendo hicho, Profesa Nkunya alisema kuwa mtu au chombo kingine mbali na TCU kutangaza uhalali, ubatili au vinginevyo kwa stashahada ya mtu mwingine ni kuhodhi madaraka ya tume, na hivyo ni kukiuka sheria za nchi.

Alisema kuwa kitendo kilichofanywa na Bw. Msemakweli na Bw. Sitta ni ukiukwaji wa sheria huku akisisitiza kuwa TCU ndio chombo pekee nchini kinachotambulika kisheria kutambua na kubatilisha ngazi mbalimbali za shahada kupitia Sheria ya Vyuo Vikuu Namba 7 ya mwaka 2005 katika kifungu Namba 5-(1) (n)

Prof. Nkunya alisema kitendo kilichofanywa na Bw. Msemakweli hakikuwa cha kiungwana kwani hana mamlaka hayo.

"Hata kama vyeti hivyo vingeletwa kwa kutathminiwa, taratibu wa tume ni kuwafahamisha matokeo ya tathmini wahusika wenyewe binafsi au waajiri wao na sio kuwatoa taarifa zao kwenye vijitabu, vyombo vya habari au vinginevyo," alisema.

Alisema kuwa tume hiyo inalaani uchapishaji na usambazaji wa majina ya raia wa Tanzania kama alivyofanya Bw. Msemakweli na kusema kuwa vitendo hivyo ni ukiukwaji wa haki za binadamu hivyo, hana ruhusa hiyo na ni vitendo vya ukiukwaji wa utawala wa sheria

1 comment:

Anonymous said...

Hawa kina Kihiyo bado wapo tu?