Sunday, February 7, 2010

Msolla atangaza makocha Taifa Stars


KOCHA wa zamani wa timu ya taifa, Taifa Stars Mshindo Msolla amewapigia chapuo kocha wa Simba Patrick Phiri na Yanga, Kostadin Papic kuwa wana sifa za kumrithi kocha wa sasa, Marcio Maximo.


Mbali na makocha hao, Msolla amerusha karata yake kwa aliyewai kuwa kocha wa Simba, James Siang'a kuwa pia ni kocha bora na kwamba makocha hao watatu wanafaa kuinoa Stars kutokana na uwezo wao mkubwa.


Akizungumza na Blog ya Vijimambo katika mahojiano maalum jana, Msolla alisema: "Maelezo ya Papic ya kwanza kabisa alipotua nchini na kusema mpira ni sanaa ni lazima ufurahishe watazamaji, niliamini kabisa kocha huyo ni kocha mzuri.


"Anachokazania ni timu icheze mpira sio kukimbiza mpira, na kwa kipindi kifupi alichofundisha Yanga imekuwa na mabadiliko," alisema kocha huyo aliyemwachia mikoba Maximo.


Kwa upande wa Phiri na Siang'a alisema ni makocha ambao kwanza ni wavumilivu na wanajua mazingira ya kiafrika na pia ni walimu ambao wameifundisha Simba kwa mafanikio makubwa.


"TFF ingewapa kipaumbele makocha hawa iwapo wataomba kuinoa Stars, naamini wataleta mafanikio makubwa kama watapewa ushirikiano mkubwa kama anavyopewa Maximo hivi sasa.


Msolla alielezea kushangazwa na mafanikio finyu na kusema fedha zilizotumika na kiwango cha soka alichoonyesha Maximo havilingani.


"Ukiangalia, zimetumika fedha nyingi sana tofauti na mafanikio yaliyopatikana."


Tayari Phiri alishatoa msimamo wake kamwe hatajitosa kuifundisha timu ya taifa, wakati kocha wa wapinzani wao Kosta Papic naye ameshaweka bayana msimamo wake wa kutaka kuinoa timu hiyo ya taifa.


Maximo ambaye mkataba wake unamalizika mwishoni mwa Juni, ameshaweka wazi kuwa hana mpango tena wa kuinoa timu hiyo inayopewa sapoti kubwa na makampuni mbali mbali na kuungwa mkono na rais Jakaya Kikwete.


Mbali na Papic pia kocha wa Ivory Coast, Vahid Halilhodzic ambaye yupo visiwani Zanzibar akifundisha soka visiwani humo kwa muda wa miezi miwili ametangaza nia yake ya kutaka kibarua cha Taifa Stars baada ya Fainali za Kombe la Dunia.


Akimzungumzia kocha huyo, Msolla alisema: "Ni kocha mzuri, hata kama ni yeye atapewa kipaumbele kuinoa Stars si mbaya.


"Kwenye fainali za Angola aliangushwa na wachezaji wake ambao ni mastaa kama akina Didier Drogba waliokuwa wakicheza kwa tahadhari wakihofia kuumizwa, hali hiyo pia imemkumba kocha wa Nigeria Shaibu Amodu," alisema.


Hata hivyo, Amodu tayari ameshapigwa chini kuifundisha timu hiyo

No comments: