Tuesday, February 9, 2010

Rufaa ya Babu Seya keshokutwa

MAHAKAMA ya Rufaa Tanzania keshokutwa inatarajiwa kuisoma rufaa ya mwanamuziki maarufu wa dansi, Nguza Viking na wanawe watatu.

Nguza maarufu kwa jina la Babu Seya na wanawe wapo jela wakitumikia kifungo cha maisha baada ya kupatikana na hatia ya kubaka na kulawiti.

Kwa mujibu wa notisi waliyopatiwa leo mawakili wa serikali na wa walalamikaji, majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa Tanzania, Nathalia Kimaro, Mbarouk Mbarouk,na Salum Massati,wataisoma rufaa namba 59 ya mwaka 2005. Watu wengi wakiwemo mashabiki wa wasanii hao wanasubiri matokeo ya rufaa hiyo.

Juni 25, 2004 Hakimu Mkuu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kusutu, Dar es Salaam, Addy Lyamuya, aliwatia hatiani Babu Seya na wanawe Papii Nguza ‘Papii Kocha’, Nguza Mbangu na Francis Nguza.

Wasanii hao walituhumiwa kutenda makosa kumi ya kubaka watoto wa wenye umri kati ya miaka sita na minane na makosa mengine 11 ya kulawiti watoto wa kike wenye umri huo huo kati ya April na Oktoba 2003 katika maeneo ya Sinza kwa Remmy, Dar es Salaam.

Wakili wao, Mabere Marando, amedai kuwa, Hakimu Lyamuya, aliingiza maslahi yake binafsi na hakuwa akizingatia ushahidi uliokuwa ukitolewa na upande wa washitakiwa.

Marando amedai kuwa, hakimu huyo alitoa kipaumbele kwa mashahidi wa upande wa Jamuhuri na kupuuza mashahidi wa upande wa washitakiwa hivyo kuwanyima haki.

Kwa mujibu wa Marando, watoto wote waliokwenda mahakamani kuthibitisha kwamba walibakwa au kulawitiwa na washitakiwa walitoa ushahidi bila kiapo isipokuwa mmoja kati ya 10 waliotoa ushahidi.

Amedai kwamba, watoto hao pia hawakurekodiwa ushahidi wao kabla ya kutoa ushahidi mahakamani jambo ambalo linakiuka sheria.

Marando amedai kuwa, baadhi ya watoto waliotoa ushahidi walikiri kutomtambua Babu Seya na washitakiwa wengine na kwamba, ripoti ya Daktari ilionyesha kwamba miongoni mwa watoto hao walikuwa ni bikira hivyo kumaanisha kwamba walikuwa hawakufanya kitendo chochote kilichohusiana na mashitaka hayo.

No comments: