Saturday, February 13, 2010

Wanamuziki walia JK amnusuru Babu Seya

WATOTO WAKE NGUZA, FRANCIS WAINGIA MTAANI WANENA
SIKU moja baada ya mwanamuziki wa Mahakama ya Rufaa kukatisha ndoto za kutoka gerezani kwa mwanamuziki wa Kikongo, Nguza Vikings ( Babu Seya), wanamuziki nchini wamepeleka kilio chao kwa Rais Jakaya Kikwete afikirie na akiona kuna umuhimu awasamehe wanamuziki hao afanye bila shinikizo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wanamuziki hao walisema kuwa wanaamini kuwa Rais Kikwete ni msikivu, mwerevu na mwenye huruma hivyo aachwe afanye maamuzi yake baada ya kufikiria kwa kutumia mamlaka yake na si vinginevyo.

Akizungumza na gazeti hili jijini Dar es Salaam jana, Kikumbi Mwanzampango, maarufu kama King Kikii, mzee wa Kitambaa cheupe, alisema anamfahamu Rais Kikwete ni mtu mwenye kupenda kusikiliza wananchi wengi wanavyotaka katika baadhi ya mambo, ndiyo maana hana wasiwasi naye katika kufanya maamuzi.

"Rais wetu ni mwenye huruma sana, anasikiliza watu wa kila rika kwa maana ya rika zote yeye anaweza mwenyewe kufanya maamuzi bila kusukumwa, kwa hiyo sioni haja kwa watu kuanza kumtaka awape msahamaha," alifafanua Kinkiki baada ya kulizwa kama alikuwa na ombi lolote kwa Rais.

Kuhusu kuachiwa kwa watoto hao wawili, alisema hiyo ni mipango ya Mungu kwani hakuna aliyejua hilo lingeweza kutokea kutokana na adhabu ya kifungo cha maisha walichokuwa wakitumikia.

Huku akionyesha hisia nzito, King Kikii alisema:, "Unajua mimi si mwanasheria wala sijui mipango ya mahakama; lakini kwanza, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa uwezo wake.

"Ukiangalia, hawa watu walikuwa wamefungwa maisha na tayari hawa walikwishatumikia miaka sita, lakini kwa uwezo wa Mungu wameachiwa huru, ni hatua nzuri."

King Kiki aliongeza: "Nakwambia sisi ni binadamu kila kitu kina mipango yake kwani hata wana wa Israel walikaa Misri miaka nenda rudi kwa mateso, lakini baadaye walijikuta wakiwa wamekombolewa."

Aliweka bayana kwamba, jambo la msingi kwa sasa hivi ni Watanzania kuendelea kuomba dua kwa Mungu ili hata akina Babu Seya na Papii waweze kuachiwa huru siku za usoni.

Kuhusu namna ya kuwasaidia vijana hao waliotoka (Nguza Mbangu na Francis Nguza kwa ajili ya kuendeleza vipaji, alisema kipaji cha mtu hakiwezi kuzimwa, hata kama hakitaibuka leo kinaweza kuibuka miaka kumi ijayo.

"Hata akina Nguza ambao wako gerezani kwa mfano wakitoka wanaweza kufanya mambo makubwa zaidi kuliko ilivyokuwa awali, kwa hiyo hata hawa watoto kama wana vipaji hakuna mtu ataweza kuvizuia,"aliongeza.

Naye kiongozi wa bendi ya FM Academia Njoshi El Sadat alisema mahakama haikuwatendea haki Nguza Vicking (Babu Seya )na Jonson Nguza (Papii Kocha) kutokana na kuwatia hatiani.

"Haiwezekani Mahakama iliwatia hatiani watuhumiwa wote wanne kwa kosa moja la ubakaji, lakini leo wametolewa wawili na wawili wamehukumiwa kifungo cha maisha,"alisema.

El Sadat alisema hajisikii faraja kwani watoto waliotoka hususani Francis Nguza ambaye alikuwa akisoma kaathirika kimasomo.

Jana watoto wake walisema bado wanaamini baba na kaka yao wananafasi ya kuachiwa huru. Watoto hao walioachiwa huru juzi na mahakama hiyo walitoka gerezani rasmi jana baada ya kukamilisha taratibu za magereza.

Akizungumza na Mwananchi, jana Geofrey Gondwe ambaye anakaa na watoto hao hivi sasa alisema Nguza na Francis wako katika hali nzuri kiafya.

Gondwe alisema kwa sasa watoto hao wa wanapumzika ili waweze kurejea katika hali nzuri kisaikolojia.

"Wametoka leo baada ya kukamilisha taratibu, lakini kwa leo hawataweza kuzungumza na wewe wanapumzika kwanza ili warejee katika hali nzuri kisaikolojia, wewe watu wametoka leo baada ya kukaa gerezani kwa miaka mitano halafu baba yao na ndugu yao bado wapo gerezani, unadhani wataweza kuzungumza kweli? alihoji Gondwe na Kuongeza:

"Wakishakuwa vizuri tutazungumza na wakili wao ili tuweke utaratibu wa kufanya ‘press conference’ (mkutano na waandishi wa habari), lakini kimsingi wamesema bado wana ‘hope’ (tumaini) kuwa baba na kaka yao wana nafasi ya kutoka kwasababu hukumu ile siyo ya mwisho".

Baada ya hukumu iliyotolewa juzi na jopo la majaji wa tatu, bado wananafasi ya kukata rufaa katika Mahakama hiyo hiyo ambapo kesi hiyo itasikilizwa na majaji watano.

Na endapo watashindwa katika kesi hiyo bado watakuwa na nafasi ya kurusha kete yao ya mwisho kwa kumuandikia Rais barua ya kuomba msamaha.

Babu Seya na wanaye, Johnson Nguza maarufu kama Papi Kocha, Nguza Mbangu na Francis Nguza walihukumiwa kifungo cha maisha mwaka 2004 baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Addy Lyamuya kuwatia hatiani kwa makosa ya kuwabaka na kuwalawiti watoto wa kike 10 waliokuwa wanafunzi wa shule ya msingi Mashujaa jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo, walikata rufaa Mahakama Kuu ambako Jaji Thomas Mihayo (mstaafu kwa sasa), aliwatia hatiani na kuunga mkono hukumu ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kisha wakakata rufaa katika Mahakama ya Rufaa.

Katika hukumu ya Mahakama ya Rufaa, ilitolewa na Jopo la Majaji watatu, Salum Massati , Mbarouk Mbarouk, wakiongozwa na Jaji Nathalia Kimaro waliosikiliza rufaa hiyo, iliyosomwa jana na Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufaa (DRCA), Neema Chusi, Babu Seya na mwanaye Papi Kocha walitiwa hatiani huku Nguza Mbangu na Francis Nguza wakiachiwa huru.

No comments: