Makala ya tatu ya tamasha la mitindo na sanaa barani Afrika yamefanyika katika mbuga ya wanyama ya Nairobi jijini Nairobi na kumalizika kwa maonyesho ya wanamitindo kupita mbele ya umati uliokusanyika.
Miongoni mwa umati huu walikuwa wageni waalikwa na wasio aliakwa wakiwemo jamii ya twiga wote wakiwa wamevalia mavazi ya kupendeza. Wageni walitumbuizwa kwa maonyesho mazuri ya ubunifu na rangi mbali kutoka kwa wasanii wabunifu waliobobea na wale wapya ambao wamejiunga na fani hii hivi karibuni kutoka kote barani Afrika
Tamasha hili lilianzishwa mwaka 2008 na mbunifu wa mitindo wa Kenya maarufu, Anne McCreath ambaye ni mwasisi wa kampuni ya mitindo ya KikoRomeo. Wakati huo Kenya ilikuwa inakabiliana na athari za machafuko ya baada ya uchaguzi mkuu uliozozaniwa wa mwaka 2007.
McCreath ameiambia BBC: "sisi sio wanasiasa lakini baado tuna mengi ya kuchangia katika jamii zetu."
Msanii Alphadi kutoka Niger na ambaye ni mwenyekiti wa tamasha la kimataifa la mitindo ya Afrika, FIMA anamuunga mkono kwa kusema kuwa: " Kuweza kuonyesha haiba hata wakati wa machafuko ni ujumbe muhimu sana. Hatutaki kujulikana tu kwa ghasia, tunataka kutambulika pia kwa mambo mazuri kama tamasha hili.
No comments:
Post a Comment