ANGALIA LIVE NEWS

Friday, December 3, 2010

Umuhimu gani wa kuwa na mwenzi wa maisha? - 2

NI Ijumaa nyingine tena tunakutana katika ukurasa wetu ambao kwa hakika umekuwa ukiboresha maisha yetu ya uhusiano. Sina shaka wasomaji wangu wote mtakuwa wazima wa afya njema na mpo tayari kabisa kusoma kitu nilichowaandalia juma hili.

Nazungumzia juu ya umuhimu wa kuwa na mwenzi wa maisha. Kila mtu anaweza kuwa na mawazo yake, akafikiria kivyake; lakini bado kuna ukweli kwamba zipo sababu muhimu zaidi ambazo zinaweza kuwakutanisha wanandoa na kuwa kitu kimoja!
Imekuwa mada yenye changamoto sana kwa wasomaji, wengi wamenitumia ujumbe kutoa dukuduku lao au kuuliza zaidi ya jambo hili. 

Wewe unafikiriaje? Kuna ambao hudhani kwamba wanakutana kwa ajili ya kujifurahisha katika ngono. Huu ni mtazamo mbaya…mtazamo hasi, kwani kama mwenzi wako akiwa na matatizo katika suala hilo, basi ndoa inaweza kuwa si imara tena!

Niliokuwa nao wiki jana, watakumbuka kwamba, nilianza na vipengele vitatu vya awali ambavyo ni kusaidiana mawazo, nikafafanua pia suala la kukutana kimwili na muda muafaka kwa ajili ya tendo hilo, hasa kwa wale ambao bado ni wachumba tu! Hebu twende tukaone katika vipengele vingine, lakini kabla sijaingia kwenye shina la mada yenyewe, tuone kama kuna ubaya wowote kwa wapenzi (ambao hawajaoana) kukutana faragha na kufanya mapenzi. 

Ni sahihi kufanya ngono kabla ya ndoa?
Tafiti mbalimbali za Wataalamu wa Mambo ya Uhusiano, zinaonyesha kuwa wengi walio katika uhusiano huwa hawawezi kuvumilia kuendelea kuwepo katika uhusiano bila kufanya mapenzi. Hata hivyo, tafiti hizo za uhakika zinaeleza kuwa baada ya wapenzi kufanya ngono, ile hamu ya kuendelea kuwa na uhusiano hupungua taratibu na pengine kuisha kabisa. 

Kitakachobakia hapo ni mazoea tu! Hiyo husababishwa na dharau za kimaumbile, na kujihakikishia kuwa hakuna kitu asichokijua kwa patina wake. Wengi hulia baada ya kujikuta akiingia katika mkumbo huu. 

Hebu jiulize, kama anakupenda, kwanini anang’ang’ania kufanya mapenzi na wewe haraka?
Wewe ni wake na huenda mna ndoto za kuishi pamoja siku moja, kwanini asivumilie mpaka wakati huo? Akitaka anaweza kuvumulia na kufaidi mambo hayo mkiwa katika ndoa halali yenye baraka zote.

Siyo wote ambao baada ya kufanya ngono huwachoka wenzi wao, kwakuwa katika hilo inawezekana pia mkaweka ratiba nzuri ambayo itawafanya kila mmoja kuwa na hamu na mwenzake kila wakati.

Kwa maana hiyo, naweza kusema kuwa, ngono siyo nzuri katika uhusiano wa kawaida, lakini inaweza kuwa na manufaa ikiwa mtafanya kwa nia ya kufurahisha nafsi zenu na siyo kuonyeshana mapenzi ya dhati. Kumbuka NGONO na MAPENZI ni vitu viwili tofauti! Upo hapo?

…kama inasaidia fulani hivi!
Inaelezwa kwamba kwa namna moja ama nyingine, wapenzi kujuana kimwiili mapema, inasaidia kujua udhaifu mapema. Wakati mwingine, unamfanya mpenzi wako asifikirie kukusaliti kwa wengine huko nje, maana ukweli ni kwamba vijana huwa na mihemko mikali zaidi!

Unajua kitakachotokea hapo? Kwamba kila mmoja anajifanya anasubiria ndoa na mwenzake, anajifanya mwaminifu, lakini anaiba nje akiamini mwenzake hajui, kumbe naye anaiba; kinachokuja kutokea hapo ni ngoma droo! Kila mmoja katoka nje.

Mila, dini zinaweza kusaidia
Lakini kama wapenzi wakakutana wakiwa wanaabudu katika imani moja au ni kabila moja, walio na misingi ya kifamilia na makuzi, inaweza kuwa mwongozo wao mzuri kwenye suala la ngono. Mafundisho ya dini zote yanakataza ngono kabla ya ndoa, kwa maana hiyo ni rahisi kila mmoja kumsihi mwenzake kufuata maagizo ya imani wanayoiamini!

Kumbuka kwamba hapa, kila mmoja atakuwa mwaminifu maana hawa si waumini bali ni waamini, ambao wana misimamo na wameshika sawasawa imani yao. Kadhalika katika mila za kabila, kama ni moja, inaweza kuwasaidia, kwani wana malezi/mafundisho/makuzi yanayofanana!

Mathalani, kijijini kwetu, mwanamke akipata mimba akiwa nyumbani kwao anatengwa na familia na wasichana wenzake kwa ujumla! Kwahiyo kwa kutambua hilo, vijana wanaogopa sana ngono wakiwa na hofu ya kutengwa, kinachotokea vijana hujitokeza hadharani na kutangaza nia ya kuoana kabla ya ndoa ya kimila kufungwa! Tupo pamoja?!

kutunziana siri / kufarijiana
Mwenzi wako wa maisha ana nafasi kubwa sana ya kujua mambo yako mengi, hata yale ambayo huwezi kumwambia rafiki yako wa karibu ofisini kwako. Siri zako za moyoni unazihifadhi kwake, hata ukiumwa ni yeye ndiye atayeweza kukuogesha, kukubadilisha nguo, kukupaka mafuta na hata kukutoa nje upumzike kwenye upepo!

Hata ukiwa na matatizo makubwa kama kufukuzwa kazi, kutimuliwa kwenye nyumba ya kupanga, kufiwa, madeni n.k ni yeye ndiye atakayeshika nafasi ya kukufariji na kukufanya ujione mwenye thamani tena. Si suala la ngono pekee, kwani ngono haiwezi kushika nafasi ya mapenzi.

kujenga familia imara
Kupata mke/mume mwema (bora) ni kujijengea nafasi ya kujenga familia bora. Mtapanga idadi na aina ya watoto mnaowataka ambao kwa hakika baadaye watakuwa na manufaa makubwa kwenu. Kikubwa zaidi katika maisha ya ndoa ni kusikilizana na kila mmoja kumpa mwenzake nafasi ya kwanza. Hapo maisha yatakuwa bora na maana ya ndoa yenu mtaiona.

Imani yangu kubwa ni kwamba, mada hii itakuwa imekufungua vya kutosha na kukufanya uwe mpya kabisa katika mtazamo wa suala zima la mapenzi na ndoa. Nisikuchoshe sana, yafanyie kazi haya, wiki ijayo tena nitashuka na mada nyingine ambayo bila shaka utaikubali. Ahsante sana na week end njema!
Chao!!!

Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi ambaye anaandikia magazeti ya Global Publishers, ameandika vitabu vya True Love na Secret Love.

No comments: