Monday, January 31, 2011

CUF, CCM kuandamana nchi nzima

MAANDAMANO ya amani yanaandaliwa na vyama vya siasa, ambapo Chama cha Wananchi (CUF), wamejipanga kufanya hivyo Jumatatu ijayo.

Chama Cha Mapinduzi (CCM), kupitia Umoja wa Vijana (UVCCM), kinaandaa maandamano ya nchi nzima ya vijana wa kuanzia shule za sekondari hadi vyuo vikuu.


CUF wataandamana kushinikiza Serikali kutolipa Sh bilioni 94 zinazodaiwa na Kampuni ya kufua umeme ya Dowans, ingawa suala hilo tayari liko mahakamani na kuna hoja inayotarajiwa kuwasilishwa leo, ili lijadiliwe bungeni.

Wiki iliyopita kampuni hiyo iliwasilisha maombi Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kutaka ilipwe deni hilo na maombi hayo yakasajiliwa na kupangiwa Jaji wakati Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi) anatarajiwa kuwasilisha hoja binafsi leo kutaka sakata la deni hilo likajadiliwe bungeni.

Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Julius Mtatiro huku akifahamu hatua hizo za kisheria na kisiasa zikiwa zimeshachukuliwa, alisema jana Dar es Salaam kuwa CUF itachukua hatua nyingine ya kisiasa kupinga malipo hayo.

Hatua hiyo ni maandamano yatakayoongozwa na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba na yataanza saa 3:00 asubuhi katika eneo la Buguruni Malapa kulipo makao makuu ya chama hicho na kuishia Viwanja vya Kidongo Chekundu.

CUF, katika kutimiza azma yao, wameitaarifu Polisi mapema kupitia barua yenye kumbukumbu namba CUF/AK/DSM/NKM/B/A2/2011/08 ya Januari 28 na wamesema hawatatarajia maandamano hayo ya amani yazuiwe kutokana na kinachoitwa taarifa za Polisi za kiintelijensia za kila mara.

Mtatiro aliwataka polisi kutokuwa mashabiki kwa kuwa fedha hizo zinaweza kuwaongezea mishahara.

Lakini pia kimewaalika wanaoitwa wanaharakati na washiriki kutoka mashirika mbalimbali ya kijamii na kupanga wakifika Kidongo Chekundu, viongozi wa kitaifa wa chama hicho watahutubia waandamanaji hao ambao kwa mujibu wa Mtatiro idadi yao itafikia maelfu.

Tofauti na CUF ambao wanapinga malipo ya Dowans na maandamano yatakuwa Dar es Salaam tu, maandamano ya UVCCM yatakuwa nchi nzima kushinikiza Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) ivunjwe.

Hatua hiyo inatokana na tamko la Kamati ya Utekelezaji ya Baraza Kuu la UVCCM ambalo lilitolewa takribani wiki mbili zilizopita, pamoja na mambo mengine wakipinga malipo kwa Dowans, pia walitaka HESLB ivunjwe na kuundwa upya.

Katika tamko hilo lililotolewa takribani wiki mbili zilizopita, pia walitishia kuitisha maandamano nchi nzima, lakini haikuwa kushinikiza HESLB ivunjwe bali kushinikiza baadhi ya mawaziri na wajumbe wa Kamati Kuu ya CCM (CC) na wa Halmashauri Kuu ya chama hicho (NEC) kuheshimu utaratibu, kanuni na Katiba ya chama hicho.

Safari hii waliotoa wazo au ombi la kuandamana si Kamati hiyo, ila taasisi nyingine ya kisiasa, Shirikisho la Vijana wa CCM Vyuo Vikuu, lakini wakati wa kutamkwa kwa wazo hilo, uongozi wa juu wa UVCCM ukiongozwa na Kaimu Mwenyekiti wa umoja huo, Beno Malisa na Katibu Mkuu wa Umoja huo, Martine Shigella ulikuwepo.

Mbali na uongozi huo, pia alikuwepo Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige ambaye alisema alikwenda kama kijana wa umoja huo hatua inayoonesha kwa upande mwingine nguvu ya azma ya maandamano hayo.

Katibu wa Shirikisho hilo, Salum Hapi, alisema matatizo ya Bodi hiyo ya mikopo kwa sasa ni janga na msiba wa kitaifa hivyo ni vyema ivunjwe na kuundwa nyingine mpya itakayowajali wanafunzi.

“Iwapo Serikali haitochukua hatua madhubuti za kuipindua Bodi hii, sisi vijana wa CCM, wasomi wa elimu ya juu na wazalendo wa Taifa hili tutautaka uongozi wa UVCCM uandae maandamano makubwa nchi nzima yatakayojumuisha wanafunzi wa sekondari ambao ni wahanga watarajiwa wa Bodi hii kushinikiza ivunjwe,” alisema Hapi.

Hapi alisema tangu Januari hadi sasa tayari vyuo vikuu 12 vimegoma kutokana na matatizo ya mikopo. “Bodi hii imegeuka taasisi ya kuwanyanyasa Watanzania na chanzo cha migogoro vyuoni, kwani hii Bodi ni mnyama gani? Tunaitaka Serikali iivunje.”

Mwenyekiti wa Shirikisho hilo, Christopher Ngubiagawe, aliyataja matatizo ya Bodi hiyo kuwa ni uwezo mdogo wa kuhakiki taarifa za waombaji wa mikopo akitolea mfano mgawanyo wa madaraja ya mikopo ambao wamedai hauzingatii hali halisi ya uchumi wa muombaji.

Alisema pia Bodi hiyo imekuwa na utaratibu mbovu wa utunzaji kumbukumbu za waombaji wa mikopo. “Mara kwa mara na bila aibu, Bodi kupitia maofisa wake imekuwa ikisumbua wanafunzi kwa kuwaomba taarifa za aina moja mara nyingi, hii inaonesha Bodi haina utaratibu mzuri wa utunzaji kumbukumbu.”

HELB pia imedaiwa kuwa na utaratibu mbovu wa kupeleka fedha za wanafunzi katika akaunti za vyuo badala ya akaunti za wanafunzi zilizoandikwa kwenye fomu.

Pia imelalamikiwa kuwa mfumo wa utendaji wa Bodi hiyo hauendani na teknolojia ya kisasa na badala yake wanafunzi wamekuwa wakisafiri kutoka maeneo mbalimbali nchini kuja kujaza fedha za maombi ya mikopo.

Lakini kudhihirisha nguvu ya azma hiyo, mara baada ya kutolewa wazo hilo, Malisa alisema umoja huo umekubali ombi hilo la maandamano iwapo Serikali haitochukua hatua ya kuivunja Bodi hiyo.

“Pamoja na ombi hili lakini tunawataka viongozi wa Bodi waondoke wenyewe kwa heshima bila kushinikizwa, bila hivyo nawaahidi kuwa tutafanya maandamano makubwa nchi nzima ya kushinikiza waondolewe,” alisema bila kujali tamko la Bodi hiyo kwamba hawahusiki ila wa kulaumiwa ni menejimenti za vyuo na Tume ya Vyuo Vikuu (TCU). Bodi pia iliwataka UVCCM waache kukurupuka.

Shigella naye alisema tamko hilo la shirikisho hilo linaendana na tamko la UVCCM lililotolewa takribani wiki mbili zilizopita.

Naye Maige, ingawa alikwenda kama kijana wa UVCCM, alivaa uwakilishi wa Serikali na kusema ameyasikia yote na atayawasilisha serikalini ili hatua sahihi zichukuliwe kwa manufaa ya taifa.

Chanzo:Habari Leo

No comments: