MEYA wa Manispaa ya Sumbawanga, Samweli Kisabwiti kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) ametangaza rasmi kujiuzulu nafasi hiyo kwa madai ya kulinda heshima yake binafsi na ya chama chake.
Akizungumza nyumbani kwake jana mjini hapa, Kisabwiti alisema amefikia uamuzi huo baada ya kutambua kwamba meya ni mtu muhimu sana katika kufanya kazi kwa ufanisi na anahitaji muda wa kutosha ili ajifunze.
‘’Kwa hiyo nimeona nipate muda wa kujifunza na kupata uzoefu kupitia nafasi yangu ya udiwani wa Kata ya Katandala na kupitia vikao mbalimbali.
“Nimeona ni vema nikaachia ngazi ili kutoa nafasi kwa wengine wenye uzoefu kwani nafasi hiyo ni nyeti sana na inahitaji uzoefu na elimu ya kutosha,’’ alisema.
Kwa mujibu wa Meya huyo ambaye ana elimu ya darasa la saba, tayari ameandika barua kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbawanga kumueleza nia yake ya kujiuzulu na imepokewa rasmi Januari 28 mwaka huu.
Alisema pia amepeleka nakala ya barua hiyo kwa taarifa kwa Katibu wa CCM wa Taifa, Katibu wa CCM wa Mkoa wa Rukwa na Katibu wa CCM wa Wilaya ya Sumbawanga. Kisabwiti alisema kuwa amefikia uamuzi huo kwa hiari yake mwenyewe bila shinikizo lolote kutoka sehemu yoyote.
Hata hivyo alisema alipopata udiwani alikubalika lakini baada ya kugombea na kushinda umeya wa Manispaa, yalianza kuibuka maneno na tuhuma kwamba yeye hana elimu ya kumwezesha kushika nafasi hiyo.
Pamoja na kusema hakushinikizwa, lakini alikiri kuwa kutokana na maneno hayo, aliona siyo rahisi kuendelea kuliongoza Baraza la Madiwani ambalo nalo kuna baadhi ya madiwani hawamkubali.
Kwa mujibu wa Kisabwiti, kutokubalika kwake kunatokana na ukweli kwamba hajasoma na hivyo ameona bora aachie ili apatikane msomi wa kuwaongoza tofauti na yeye ambaye ana elimu ya darasa la saba.
“Awali ya yote kusudio langu kubwa lilikuwa kujiuzulu kuanzia nafasi ya udiwani hadi umeya lakini rafiki zangu wa karibu na wanachama wa chama changu walinisihi nijiuzulu nafasi ya umeya tu kwani kama ningejiuzulu na udiwani, ingelazimu uchaguzi mdogo ufanyike kitendo ambacho huenda CCM ingepoteza kata hiyo, “ alisisitiza.
Meya huyo ambaye anamiliki maduka manne ya kuuza nyama mjini hapa alikiri kuwa nafasi hii sio tu ni nyeti bali pia ni dhahabu na kwamba kama angekuwa hana pengine pa kushikia, asingejiuzulu.
Kutokana na uamuzi huo, amedhamiria kujikita zaidi katika biashara zake hizo alizosema zilianza kudorora tangu ajiingize katika siasa.
Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya ya Sumbawanga Mjini, Charles Kabanga alidai hawajaipata rasmi taarifa hiyo ya kujiuzulu lakini alisema Kisabwiti ana hiari ya kufanya hivyo.
Alisema CCM itafuata utaratibu na atapatikana Meya mwingine kuziba pengo hilo.
Aliongeza kusema kuwa kujiuzulu kwa Meya huyo hakutakiathiri chama kisiasa kwa sababu kama kiongozi unaona nafasi imemshinda au umeshindwa kuimudu, ni bora awajibike ili kutoa fursa kwa wengine wenye uwezo kuliko kuendelea na hatimaye kuharibu .
Meya huyo amedumu katika nafasi hiyo kwa mwezi mmoja na nusu, alichaguliwa kushika nafasi hiyo Desemba 17 , mwaka jana ambapo alikuwa mgombea pekee baada ya mgombea wa Chadema kujitoa.
Alipata kura za ndiyo 12 na tisa zilimkataa. Halmashauri hiyo ina jumla ya madiwani 21 kati ya hao 16 ni wa CCM , wanne wa Chadema na mmoja ni diwani kupitia tiketi ya DP.
Chanzo:Habari Leo
No comments:
Post a Comment