ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, February 1, 2011

Januari kugharimia mawasiliano Bumbuli

Januari Makamba
Zulfa Msuya,aliyekuwa Tanga
MBUNGE wa Bumbuli,  Januari  Makamba,  amezindua  huduma ya mawasilino na wakazi wa jimbo lake ambao watakuwa wanatuma ujumbe mfupi katika simu zao na gharama za malipo zinakuwa chini yake.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Makamba alisema  mawasiliano ya simu ni muhimu  katika kuharakisha maendeleo.

Alisema kwa kuzingatia hilo , wananchi wa Bumbuli  lazima wawe miongoni mwa mamilioni ya Watanzania  wanaopaswa kuwa na  mawasiliano hayo,  ili nao wapige hatua za haraka maendeleo.
“Nimefanya mazungumzo na kampuni za simu,lengo ni kuleta mawasiliano karibu ili wananchi wangu waweze kunufaika na mpango huo. Nitafanya semina elekezi ya viongozi ili waweze kuwahamasisha wananchi wa Jimbo la Bumbuli kuhusu mpango huo,”alisema Makamba.


Mbunge huyo wa Bumbuli aliandaa semina ya viongozi wa kata, viti wa Serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa lengo la kupangiana majukumu ya kutekeleza Ilaani ya CCM.

Alisema kwa kipindi kirefu, wananchi wa jimbo hilo wamekuwa wakikabiliwa na changamoto mbalimbali za kimaendeleo na kwamba hadi sasa bado wako nyuma.

Alisema kwa msingi huo, kuna kila sababu za kubuni mikakati ya kujiletea maendeleo kwa haraka.
“Kwa miaka mingi sasa tumekabiliwa na tatizo la  kutafuta maendeleo  na bado hatujafanikiwa, lakini nadhani wakati umefika wa kutoka kwenye boksi na kufanya kazi kwa bidii  ili tupate maendeleo,”alibainisha.
Kwa mujibu wa Makamba, wajibu wake kutekeleza ahadi alizotoa kwa wananchi wa jimbo hilo, ambalo kabla ya uchaguzi wa Oktoba mwaka jana, lilikuwa linawakilishwa bungeni na Wiliam Shellukindo ambaye alishindwa katika kura za maoni ndani ya CCM.

Mbunge huyo wa sasa, aliwataka wananchi kushirikiana na viongozio wao, ili iwe rahisi kutekeleza mikakati ya kujiletea maendeleo katika nyanja mbalimbali.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Lushoto,  Sophia Mjema, aliwataka viongozi wote walioko madarakani, kutekeleza  ahadi zao kwa wakati.

Hali kadhalika aliwahimiza watendaji wa vijiji, kuwasomea wananchi mapato  na matumizi ya fedha wanazochanga, ili kusaidia utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Alisema kufanya hivyo, kutawafanya wananchi wawe na imani na viongozi hao.
Wakati huo huo, baadhi ya wananchi walitoa malalamiko yao kwa uongozi wa Jimbo hilo kuwa, baadhi ya watendaji wa kijiji wamekuwa wakiwatoza fedha katika kupata huduma mbalimbali.

Huduma hizo ni pamoja na kupigiwa mihuri, kuandikiwa barua na kadhalika.

Kuhusu hilo, Mkuu wa Wilaya alionya viongozi wa vijiji kuacha mara moja kuwatoza wananchi gharama za mihuri au kuandikiwa barua.

                                                                                 Chanzo:Mwananchi

No comments: