ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, February 1, 2011

Hoseah abanwa kuhusu Dowans

Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk Edward Hoseah
Ramadhan Semtawa na Sadick Mtulya

MZIMU wa mkataba tata wa Kampuni ya Richmond kisha Dowans, umezidi kumtafuna Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk Edward Hoseah, baada ya wabunge kumbana wakimtaka afafanue tena usahihi wa taarifa yake ya awali iliyosafisha mkataba huo ambao umeibua utata kwa Kampuni ya Dowans.

Takukuru iliwahi kufanya uchunguzi wa mkataba huo wa Richmond uliosaniwa Juni 23, 2006, ikitumia Sheria ya  Rushwa ya mwaka 1971 na kutoa ripoti iliyobainisha ulikuwa halali, lakini uchunguzi wa Kamati Teule ya Bunge ulibaini ulikuwa wa kifisadi.

Ikiwa sasa ni miaka karibu minne tangu Takukuru kutoa ripoti hiyo huku kukiwa na mjadala mzito kuhusu malipo ya Sh94 bilioni kwa Dowans , baadhi ya wabunge jana wameamua kugusa majeraha hayo wakimtaka Dk Hoseah ataje wamiliki wa Richmond anaowafahamu ili kufungua njia kuwabaini wamiliki halali wa Dowans.

Vyanzo vya kuaminika kutoka ndani ya kikao cha semina ya siku 10 kwa wabunge kinachoendelea jijini Dar es Salaam, kilifafanua kwamba Dk Hoseah alitakiwa afafanue ilikuaje aisafishe Richmond ambayo sasa inaletea nchi matatizo kupitia Dowans.

Kwa mujibu wa vyanzo hivyo vya habari, Dk Hoseah alirushiwa makombora hayo wakati akipokea maoni kutoka kwa wabunge mbalimbali kuhusu mada yake aliyoiwasilisha, na wakati wa majumuisho ndipo alipogeuka mbogo na kujibu mapigo kwa jazba.   

"Hosea kabanwa kaambiwa yeye aliisafisha Richmond ambayo baadaye ilirithi mkataba wa Dowans, vipi sasa mkataba huo unaonekana kuitesa Serikali... ndipo alipoanza kujibu kwa ukali," alifafanua mbunge mmoja ambaye aliomba kuhifadhiwa jina.

"Amegoma kuwataja wamiliki na amekuwa mkali kweli kweli na kwambia..., amesema kabisa siwezi kuwataja. Aliulizwa kama Richmond haina matatizo mbona Dowans ina matatizo wakati mkataba ndiyo huo iliorithi?" 

Hata hivyo, baada ya kubanwa sana, Dk Hoseah alijitetea akisema atakuwa tayari kuwataja wamiliki wa Dowans na hata wale wa Richmond endapo akiitwa katika kamati za Bunge na si katika semina hiyo.

Mkataba wa Richmond uliangusha Baraza la Mawaziri la kwanza la Serikali ya Awamu ya Nne baada ya Edward Lowassa kujiuzulu uwaziri mkuu Februari mwaka 2008, kufuatia kashfa hiyo.

Hata hivyo, badaye akiwa nje kwa mapumziko ya mlo wa mchana, Dk Hoseah ambaye awali aliwasilisha mada yenye kichwa cha habari, "Nafasi ya Bunge Katika Mapambano Dhidi ya Rushwa Nchini Tanzania," alipoulizwa yaliyojiri ndani, alijibu, "Ndiyo, nimesema siwezi kujibu kwasababu suala hilo liko bungeni na katika vyombo vya sheria."

"Nyie wenyewe mnajua na wao wabunge wanajua suala hilo angeulizwa spika liko bungeni, lakini pia liko mahakamani sasa nianze kuingilia taratibu za kisheria, siwezi. Lakini, hawa wabunge wanajuana wenyewe pia."

Pamoja na kubanwa huko, Dk Hoseah aliwatahadharisha wabunge kuacha vitendo vya rushwa na akawasisitizia kuwa bado anaendelea kuwachunguza kuhusiana na  vitendo vya rushwa vilivyoajiri katika Uchaguzi Mkuu uliopita.

“Bado ninaendelea na mchakato wa kuchunguza wabunge waliotuhumiwa kujihusisha na vitendo vya rushwa na nikikamilisha uchunguzi, watafikishwa mahakamani,’’ kilisema chanzo chetu.
 
Kutokana na majibu hayo, wabunge wa CCM walimjia juu Dk Hoseah na kumhoji ni kwa nini aliwachunguza wagombea wa CCM pekee na kuwaacha wa upinzani.

“Dk Hoseah alijibu, ata wagombea wa upinzani aliwafuatilia nyendo zao na pia wapo ambao anakamilisha uchunguzi  ili awafikishe mahakamani,  lakini aliweka mkazo kwa wagombea wa CCM kutokana na kwamba kama angefanya hivyo kwa wapinzani, angeeleweka kuwa ametumwa na CCM kusambaratisha upinzani,’’ kilisema chanzo kingine.

Chanzo hicho kilisema, Dk Hoseah alijitetea kuwa, Takukuru haipaswi kulaumiwa pekee katika kufikisha kesi mahakamani na kwamba hatua hiyo hutakiwa kufanywa na ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Serikali (DPP), baada ya kukamilika kwa taratibu zote. 


Katika mada yake ya awali, Dk Hoseah alilipa Bunge changamoto kuisimamia Serikali na kuongeza, "Msisitizo mkubwa katika kuhakikisha rushwa inadhibitiwa ni kwa Serikali kuwa wazi (Transparency) na kuwajibika katika maamuzi yake (Accountability)."

Mkuu huyo wa taasisi yenye dhamana ya kuzuia na kupambana na rushwa nchini ambaye mara kwa mara mada yake ilipingwa na baadhi ya wabunge waliokuwa wakiguna, "mmm," alifafanua kwamba, uwazi na uwajibakaji wa Serikali unapaswa kuwahikikishia Watanzania  maamuzi yake yanazingatia maslahi ya nchi.

"Na Bunge linawajibu huu wa kikatiba kuona kuwa uwazi na uwajibikaji unazingatiwa wakati wote na kuwa ni sehemu ya utamaduni wa utawala bora," alisisitiza Dk Hoseah ambaye hivi karibuni alinukuliwa na mtandao wa Wikileaks akimtuhumu Rais Jakaya Kikwete, akidai hana dhamira ya dhati kupambana na rushwa kubwa.

Kuhusu nafasi ya Bunge na mapambano dhidi ya rushwa, Dk Hoseah aliupongeza mhimili huo wa dola wa kutunga sheria, lakini akautahadharisha, "msisitizo mijadala hii isitawaliwe na chuki, hasira na kukomoana bali izingatie ushahidi na ukweli."

....Ikifanyika hivyo haki itatendeka na mitafaruku kati ya mtu na mtu au vikundi na vikundi haitatawala taswira ya Bunge linalojali maslahi ya Watanzania kwasababu ukweli utabaki na ukweli hauwezi kubadilishwa kwa kutupiana lawama au kuwekeana chuki baina ya mtu au kikundi kimoja dhidi ya kingine."

Katika angalizo lake ambalo liliongeza mguno kwa wabunge, Dk Hoseah alisema, umefika wakati sasa tuhuma zozote  za rushwa zijadiliwe kwa kuangalia ushahidi unaothibitika na si hisia, kitu alichokiita hakitaweza kuleta tija katika mapambano dhidi ya rushwa.

Huku akinukuu tafiti mbalimbali duniani, Dk Hoseah alisema rushwa inachangiwa na sababu mbalimbali zikiwemo utumiaji wa madaraka vibaya, tamaa na uroho wa mali, migongano ya maslahi, kujuana katika kutoa ajira na zabuni mbalimbali, mmomonyoko wa maadili na kukosekana kwa uwazi na uwajibikaji.

Dk Hoseah aliwalipua wabunge akiwataka kuacha kutumia rushwa katika kupata nafasi ya uwakilishi kwa kutumia njia za rushwa wakati wa Uchaguzi Mkuu.

Hoseah tangu kuibuka sakata la Richmond, amejikuta akiwa katika vita pana na wabunge hasa wapambanaji wa ufisadi mvutano ambao ulikorezwa zaidi na uamuzi wake wa kuchunguza kile alichokiita ni posho mbili.

No comments: