CHAMA Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema kuwa hakiwezi kushirikiana na vyama vingine vya upinzani bungeni kwa kuwa vyama hivyo vimeungana na CUF ambayo 'imefunga ndoa' na CCM na kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar.
Hayo yalisemwa jana na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Willibrod Slaa alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Hayo yalisemwa jana na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Willibrod Slaa alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Dk Slaa alisema Kamati Kuu ya Chadema imeona kuwa chama hicho hakiwezi kuwa na ushirikiano wenye tija na vyama hivyo bungeni, hivyo imemwagiza kiongozi wa kambi ya upinzani kuunda baraza kivuli la mawaziri kwa kuwahusisha wabunge wa Chadema pekee.
"Kamati Kuu imeendelea kuzingatia umuhimu wa vyama vya siasa kushirikiana katika kuimarisha nguvu ya upinzani hapa nchini. Hata hivyo, Kamati Kuu imezingatia kuwa CUF na CCM wamejiunga kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar na kwa kuwa sheria inayoruhusu uwepo wa vyama vya siasa inahusu pande zote za Muungano, inaamini kuwa CCM na CUF ni wamoja hata huko, (Bara),"alisema Dk Slaa.
Dk Slaa alisema hayo alipokuwa akieleza maazimio ya Kamati ya Chadema iliyokutana hivi karibuni jijini Dar es Salaam.
Kuhusu mchakato wa upatikanaji wa katiba mpya, Dk Slaa alisema kamati hiyo ilipinga utaratibu uliotangzwa na Rais Jakaya Kikwete wa kuunda tume kwa kuwa hiyo siyo njia sahihi ya kutungwa kwa katiba mpya.
Alisema njia sahihi ambayo kamati hiyo iliona ni ile itakayowashirikisha wananchi kikamilifu na kwa dhati bila kujali tofauti zao za kisiasa, dini, kabila, umri, elimu,wala jinsia.
"Kamati Kuu imejadili na kutafakari kwa kina maoni ya wadau mbalimbali juu ya mchakato unaofaa katika kupata katiba mpya na kuzingatia kuwa njia sahihi ni ile itakayowashirikisha wananchi,"alisema Dk Slaa na kuongeza:
"Aidha, Kamati Kuu imezingatia kwamba kuunda tume ya rais siyo njia sahihi itakayowezesha upatikanaji wa katiba mpya yenye kuzingatia utashi, matakwa na mahitaji ya wananchi wa Tanzania."
Alisema kutokana na hali hiyo, kamati hiyo iliunga mkono utaratibu wa kutumia Bunge katika kutengeneza na kusimamia mchakato wa upatikanaji wa katiba hiyo huku ikipongeza uamuzi wa sekretariati yake kwa kumuagiza Mbunge wa Jimbo la Ubungo, John Mnyika kuwasilisha hoja binafsi bungeni kuhusu katiba.
Dk Slaa alitoa wito kwa wabunge wote kuunga mkono hoja hiyo ili iweze kupita na kuruhusu mabadiliko yatakayowezesha kulifikisha taifa kwenye katiba mpya na bora kwa maslahi ya umma.
…yamtoa lawama vurugu za Arusha
Akizungumzia suala la vurugu za Arusha, Dk Slaa alisema Kamati Kuu ilipokea kwa masikitiko vifo vya raia watatu waliouawa kwa kupigwa risasi na polisi katika juhudi za kuzuia maandamano halali yaliyoandaliwa na chama hicho.
Alisema kamati ilimtupia lawama Mkurugenzi wa Halmashauri ya Arusha kwa kuvuruga uchaguzi wa Meya wa Jiji la Arusha na inaamini mkurugenzi huyo alifanya hivyo kwa maelekezo ya CCM.
Dk Slaa alisema kamati iliwapa pole familia za wafiwa wote na kumpongeza mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Mbunge wa Arusha, Godbles Lema kushiriki na wafiwa wakati wote wa maombolezo ya msiba huo.
Alisema kamati hiyo imewaagiza madiwani wa Chadema wa Halmashauri ya Jiji la Arusha kuendelea kuhudhuria vikao vya baraza la madiwani na kuwawakilisha wananchi waliowachagua na pia kuhakikisha wanatumia nafasi yao kufanikisha uchaguzi wa meya unafanyika.
Maandamano kupinga malipo Dowans
Kuhusu Dowans, Dk Slaa alisema kamati ilielezea masikitiko yake ya kupanda kwa gharama za umeme na nishati za gesi nchini na kusisitiza kuwa maandamano yaliyoandaliwa na chama hicho nchi nzima yako paleple na yataanza Februari 24 katika Jiji la Mwanza.
Alisema pamoja na mambo mengine, maandamano hayo yanapinga malipo ya fidia kwa kampuni ya Dowans ambayo tayari CCM imeridhia.
"Kamati Kuu imesikitishwa na kufadhaishwa na uamuzi wa CCM na Serikali yake wa kuridhia kuilipa Kampuni hewa ya Dowans fedha za walipa kodi Sh94 bilioni pamoja na kwamba kampuni hii Ilishaharamishwa na Bunge kwa niaba ya Watanzania.
Kamati Kuu imetambua kuwa sakata la Dowans ni mwenendelezo wa vitendo vya kifisadi ndani ya CCM na Serikali yake ambavyo vimelighalimu taifa,"alisema Dk Slaa.
Alisema kamati hiyo iliwahimiza wabunge wa Chadema na wananchi wote kuendelea kupinga malipo ya Dowans na kuwataka wabunge hao kuendelea kuwahamisha wananchi kupinga malipo hayo kwa njia ya kisiasa na kisheria.
Aidha, Dk Slaa alitaka Serikali ya CCM kuchota sera nzuri za Chadema zinazohusu uboreshaji wa nishati ya umeme na kuzitumia kwa masilahi ya Taifa.
Matokeo ya Kidato cha Nne janga la taifa
Katika hatua nyingine, Chadema imetangaza matokeo ya kidato cha nne kuwa ni janga la kitaifa.
"Kamati Kuu imezingatia na kusikitishwa kuona kuwa ni asilimia 11.5 tu ya wanafunzi waliofanya mtihani wa Kidato cha Nne ndio waliofauli. Ndio kusema karibu asilimia 90 ya vijana waliomaliza kidato cha nne mwaka 2010 hawawezi kuendelea na masomo ya elimu ya juu na itakuwa vigumu kwa vijana hawa kupata ajira yoyote ya uhakika,"alisema.
Kuhusu suala la udini, katibu huyo alisema Kamati Kuu Ilipokea taarifa hiyo kwa masikitiko na kwamba hoja hiyo ya propaganda Iliyolenga kuwarubuni Watanzania na kuwaonda kwenye mchakato wa kuajdili hoja za msingi za kitaifa.
"Kamati Kuu imezingatia kuwa viongozi wa juu wa CCM wameamua kuficha udhaifu wao wa kioungozi kwenye kivuli chini ya zulia la udini ili wananchi waache kujadili mambo yamsingi ya Taifa ikiwemo kushindwa kwa CCM kutekeleza ahadi ilizoahaidi kwa wananchi wake,"alisema Slaa.
No comments:
Post a Comment