Na Heckton Chuwa, Moshi
MADIWANI wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro jana waliweka pingamizi kwa Msajili wa Mahakama ya Ardhi kuzuia
ubadilishaji au uendelezaji wa viwanja na nyumba ambavyo vinamilikiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Moshi Mjini na jumuiya yake ya Umoja wa Vijana (UVCCM) mkoani hapa.
Akitoa tamko kuhusiana na uamuzi huo kwa niaba ya meya wa halmashauri hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Mipango Miji na Mazingira wa Halmashauri hiyo, Abdrahman Sharif, alisema madiwani wa halmashauri hiyo wameamua kuchukua hatua hiyo kutokana na taarifa za kiintelejinsia zinazoonyesha kuwa CCM wanahaha kubadili umiliki wa mali hizo.
“Tumefanya uchunguzi wa kina kwa kuzingatia sheria zote na kubaini kuwa mali hizo ni mali halali za halmashauri ya manispaa ya Moshi,†alisema Diwani Sharif ambaye pia ni katibu wa madiwani wa CHADEMA katika Baraza la Madiwani wa halmashauri hiyo.
Akitolea mfano wa uchunguzi huo, Bw. Sharif alisema kuwa viwanja na jengo linalotumiwa na UVCCM vyenye ukubwa wa ekari 2.7 vina hati miliki nambari 15686 na kwamba imemilikishwa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi kwa miaka 33.
“Kufuatia uhalali huu, CCM ilitakiwa iwe inailipa halmashauri sh. milioni 20 kwa mwaka na kiwanja na jengo ambalo CCM wilaya Moshi Mjini imefanya kuwa ofisi zake vina ukubwa wa square futi 18,790 na vimesajiliwa kwa hati nambari 056038/94,†alisema.
Aliongeza kusema kuwa hatua walizochukua ni muhimu na zenye manufaa kwa umma na kwamba hazilengi kumkomoa mtu au taasisi yoyote zaidi ya kuzikomboa na kuzilinda mali za halmashauri hiyo.
“Mchezo huu wa CCM umekuwa ukiidhulumu halmashauri ya manispaa ya Moshi zaidi ya sh. milioni 100 kwa mwaka na tunachotaka ni fedha hizi zitumike kwa ajili ya maendeleo ya watu wa Moshi,†alisema.
Akijibu maswali kuhusiana na swala hilo, Bw. Sharif alisema uamuzi huo ni wa madiwani wa halmashauri hiyo na kwamba pamoja na kuwashirikisha madiwani wenzano wa CCM madiwani hao wa chama tawala hawakujitokeza wakati wa kutolewa kwa tamko hilo.
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Moshi Mjini, Bw. Godfrey Mwangamilo alisema swala hilo linafuatiliwa na Katibu wa CCM wilaya ya Moshi Mjini na kwamba chama hicho kina uhalali kuhusiana na mali hizo, hivyo madiwani hao wamekurupuka.
Chanzo:Majira
No comments:
Post a Comment