MWANAFUNZI Wema Eliakunda ambaye alishindwa kujiunga na kidato cha kwanza baada ya kukosa ada, amepongeza Kampuni ya Mwananchi Communication Limited (MCL) kwa kumsaidia kumtafutia mfadhili.
MCL ndio wachapishaji wa magazeti la Mwananchi, Mwananchi Jumapili, The Citizen na gazeti la michezo na Burudani la Mwanaspoti.
Eliakunda alitoa shukrani hizo jana kwenye ofisi za MCL mjini Moshi wakati akikabidhiwa Sh300,000 zilizotolewa kama msaada na Mbunge wa Viti Maalumu(Chadema), Grace Kiwelu, ili mwanafunzi huyo aweze kwenda shule.
“Namshukuru sana mheshimiwa Kiwelu japo simfahamu kwa namna alivyoguswa na tatizo langu na kunisaidia, Mungu ambariki na amzidishie, lakini kubwa naishukuru MCL kwa sababu bila wao tatizo langi lisingejulikana,” alisema Eliakunda.
Mwanafunzi huyo ambaye alikabidhiwa fedha hizo na Mwandishi Mwakilishi wa MCL Mkoa Kilimanjaro, Daniel Mjema, alisema shukrani zake kwa MCL na Kiwelu atazionyesha kwa kufanya vizuri kwenye masomo.
Akiwa ofisini hapo, mwanafunzi huyo aliunganishwa kwa njia ya simu na mbunge huyo na kumshukuru kwa msaada huo na kwamba, fadhila hiyo atailipa kwa kufanya vizuri.
Eliakunda aliliambia Mwananchi baadaye kuwa, katika mazungumzo yake na mbunge kwenye simu, Kiwelu alimsisitiza kuhakikisha anasoma kwa bidii na nidhamu kwa walimu na wanafunzi wenzake, ili awe kielelezo cha shuleni.
Wiki iliyopita, Eliakunda aliyemaliza Shule ya Msingi Benjamin iliyopo Mabogini Wilaya ya Moshi Vijijini na kuchaguliwa kujiunga na Sekondari Mpirani, alifika ofisi za Mwananchi Moshi akiomba gazeti kumsaidia kutafuta mfadhili wa kumsomesha.
Lakini jana baada ya kusoma habari za msichana huyo kupitia gazeti la Mwananchi la Jumamosi iliyopita, Kiwelu alikuwa wa kwanza kuguswa na tatizo la msichana huyo na kuahidi kutoa kiasi hicho cha fedha.
Lakini jana baada ya kusoma habari za msichana huyo kupitia gazeti la Mwananchi la Jumamosi iliyopita, Kiwelu alikuwa wa kwanza kuguswa na tatizo la msichana huyo na kuahidi kutoa kiasi hicho cha fedha.
“Kwa kweli niliposoma habari ya msichana yule ilinigusa sana, hasa ikizingatiwa na mimi ni mwanamke…nilijiuliza maswali mengi kuhusu hatma ya maisha ya msichana huyu ambaye ana nia ya dhati ya kusoma,” alisema Kiwelu.
Mbunge huyo alisema tatizo ni serikali kuona elimu ni fadhila au huruma ya watawala na kufafanua kuwa, rasilimali ambazo Tanzania inazo, isingestahili atokee mwanafunzi ambaye amefaulu na kushindwa kuendelea na masomo.
Kiwelu alisema Watanzania hivi sasa wanakabiliwa na changamoto kubwa ya elimu, ili waweze kushindana na mataifa wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), hivyo serikali inapaswa kuwekeza kwenye rasilimali watu.
Mbunge huyo alilipongeza Mwananchi kwa kutoa nafasi kwa mwanafunzi huyo kutoa kilio chake, huku akisema gazeti hilo limeonyesha jinsi lilivyojitoa kupigania haki ya watoto wa kike kusoma na makundi mengine ya jamii.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment