Fidelis Butahe na Neema Myovela
MZIMU wa Chadema umeonekana kuendelea kukitesa CCM kufuatia viongozi wakuu wa chama hicho kutumia muda mwingi kuzungumzia hofu dhidi ya chama hicho cha upinzani kuelekea katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, katika uzinduzi wa maadhimisho ya miaka 34 ya chama hicho tawala.
Viongozi hao walionyesha wasiwasi wao dhidi ya Chadema wakati wakizungumza katika mkutano wa ufunguzi wa maadhimisho ya miaka 34 ya kuzaliwa kwa CCM, yaliyofanyika jana katika viwanja vya Biafra, Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Viongozi hao ni pamoja na Rais Mstaafu wa Zanzibar ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa CCM visiwani humo, Aman Abeid Karume, Katibu Mkuu wa CCM, Yusuph Makamba, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, John Guninita pamoja na katibu wake, Kilumbe Ng’enda.
Hatua hiyo ya CCM kutumia muda mwingi kuzungumzia Chadema badala ya mafanikio ya uwepo wake nchini kwa miaka 34, unachukuliwa na wachunguzi wa masuala ya kisiasa kama dalili ya kuumizwa na wapinzani hao ambao walizoa majimbo 23 ya ubunge hasa katika miji mikubwa nchini.
Miongoni mwa majibo hayo ni Kawe na Ubungo jijini Dar es Salaam, Ilemela na Nyamagana jijini Mwanza, Arusha Mjini, Iringa Mjini, Moshi Mjini, Musoma Mjini na Mbeya Mjini.
Akizungumza katika mkutano huo, Karume alisema majimbo mawili yaliyochukuliwa na Chadema mkoani Dar es Salaam kuwa ni kama wamewakopeshwa.
“Wapizani walikamia sana uchaguzi hasa hapa Dar es Salaam, lakini matokeo ndio hayo kati ya majimbo nane tumechukua sita, hayo mawili tumewakopesha tu,”alisema Karume.
Katika mkutano huo, Karume alitumia dakika 16 kuzungumza na wananachi huku wanaCCM waliohuduria mkutano huo wakionekana wanyonge ambapo alisema kuwa viongozi wa CCM wanatakiwa kutembea kifua mbele kwa kuwa hata huo ushindi walioupata ni mkubwa na kwamba zipo njia nyingi za kukiondoa Chadema.
“Njia ni nyingi za kuwaondoa, kama hawataki kutoka basi tunawafuata huko huko, uwezo, sababu na nia ya kurejesha majimbo yetu tunao, wakae chonjo 2015 tunachukua wenyewe au sio Guninita,”alisema Karume akimuuliza Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Dar es Salaam.
Alisema CCM ndio iliyoruhusu upinzani nchini mwaka 1992 ili wawasikilize wapinzani na kwamba kwa kuwa chama hicho kina uzoefu kinatakiwa kutumia uzoefu huo kuwasomesha wapinzani.
“Wana CCM wote wasisahau dhamana hiyo, tukiwachoka watatupeleka sehemu isiyo sahihi, mtambue kuwa kuna tofauti kubwa sana kati ya mwalimu na mwanafunzi,”alisema Karume na kuongeza:
“Msikubali kudanganywa na propaganda za wapinzani katika magazeti, CCM ina itikadi na sera zake, tujiandae na uchaguzi wa chama mwaka 2012 ili tuchague viongozi bora kwa ajili ya kushinda mwaka 2015”.
Awali kabla ya Karume kuzungumza, Katibu Mkuu wa CCM, Makamba alisema ushindi iliopata chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka 2010 sio mdogo.
Alisema kuwa ushindi wa Rais Jakaya Kikwete wa kura milioni 5 huku mpinzani wake, Dk Willibrod Slaa akiambulia kura milioni 2 sio wa kubeza na kwamba kwa matokeo hayo, Dk Slaa ni mpangaji ndani ya nyumba ya rais Kikwete.
“Dk Slaa atambue kuwa kashindwa, ndio kashindwa…., hivi mpangaji unaweza kumfungia mlango mwenye nyumba,”alihoji Makamba na kuwafanya wanachama wa chama hicho kuangua kicheko.
“Kikwete ndio baba mwenye nyumba bwana, hao wapinzani ni wapangaji tu, Guninita usisikitike sana, hata hao wabunge wa upinzani huko katika majimbo yao chumvi, binzari wanapata kutoka kwa CCM, hizo ni kelele za wapangaji tu, tujipange kwa uchaguzi mwingine,”alisema Makamba.
Alisema wanachotakiwa kufanya CCM ni kuzika tofauti zilizopo, kama kupanda kwa gharama za bei ya umeme na kuongeza kuwa upandaji wa gharama hizo ni jambo la kawaida.
“Hapa sio peponi, Mungu anasema kwa jasho lako utakula, ni wakati wa kuwapa nafasi mawaziri wetu wafanye kazi, tusifanye maandamano kama wao wasitutoe katika ajenda zetu, sisi tuna kazi za kufanya,”alisema Makamba.
Kwa msimamo huo, Makamba anapingana na Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), ambao wametishia kuitisha maandamano nchi nzima iwapo Serikali haitachukua hatua za haraka kutatua matatizo ambayo yanawakabili wananfunzi katika vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu nchini.
UVCCM katika siku za karibini wamekuwa wakitoa matamshi makali dhidi ya viongozi wa chama chao na Serikali, hali ambayo inaashiria kuwepo kwa mgawanyiko ndani ya chama hicho.
Kwa uapnde wake akitoa salamu za CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Katibu wa chama hicho mkoani humo, Kilumbe Ng’enda alisema kuwa dharau ndio zimekiponza chama hicho na kwamba zimesababisha baadhi ya majimbo washinde wabunge wa upinzani ambao hawana sifa.
“Majimbo tuliyoyapoteza tutayarudisha, tulidharau siasa zao za chuki, ushabiki, upandikizi na uchochezi, lakini ndio zilizotuponza, tumevumilia mengi, lakini tukajikuta tumepoteza majimbo kwa propaganda na uchochezi wa wapinzani, "alisema Ng’enda.
Alisema kuwa wanachama wa CCM itafikia wakati watachoka na siasa zinazofanywa na wapinzani na kwamba wanaweza kufikia wakati wakachukua hatua.
“Ukicheka na nyani utavuna mabua, umefikia wakati wa kuchukua hatua, yaliyotokea mkoani Arusha ni uchochezi na ushabiki tu, ni mambo ambayo yanaweza kuleta vurugu na amani kuwa mashakani,” alisema Ng’enda.
Alifafanua kwamba tabia ya baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani kuwachochea vijana kufanya vurugu kutalipeleka taifa katika hatua mbaya.
Akizungumza kwa ukali alisema, “Wana CCM wa Dar es Salaam tunasema hivi, ‘tumechoka’, uvumilivu unatosha, Serikali isimame kama Serikali kwa sababu hivi sasa uchaguzi umekwisha”.
Kuhusu katiba mpya, Ng’enda alisema mapendekezo yaliyotolewa na Rais Jakaya Kikwete yanatakiwa kufuatwa na wananchi.
“Asiye na hoja ya katiba akae pembeni, wapo wanaozungumzia suala la katiba ili wapate umaarufu tu, tufuate yale yaliyozungumzwa na Rais ili tuweze kufikia muafaka ulio bora,”alisema.
Kauli ya Ng’enda iliungwa mkono na Guninita ambaye alisema kuwa yaliyozungumzwa na Katibu wake ndio kauli ya CCM Mkoa wa Dar es Salaam.
“Kazi yangu kubwa ilikuwa kumkaribisha Katibu wa CCM, lakini acha niseme machache, Dar es Salaam waliojiandikisha kupiga kura ni watu 2.4 milioni, lakini waliopiga kura ni watu 700,000 tu, hili si tatizo la CCM bali ni jukumu letu sote,”alisema Guninita.
Huku akizungumza kwa upole, Guninita alifafanua kwamba wanachama wa CCM hawatakiwi kuwa na huzuni yoyote kwa kuwa kati ya majimbo nane ya jijini humo ni mawili tu ndio yaliyokwenda kwa wapinzani .
“Ubunge tumepoteza majimbo mawili kati ya nane, Kata tumepoteza 16 tu kati ya 90, lakini mkumbuke kuwa katika uchaguzi wa mwaka 1995 Dar es Salaam tulipoteza majimbo matatu na tukafanikiwa kuyarejesha tena kwetu,” alisema Guninita. Hata hivyo, wakati huo Guninita alikuwa kiongozi wa Chadema.
Huku akizungumza kwa jazba, Guninita alisema kuwa hata Uchaguzi Mkuu ukirudiwa kesho (leo) CCM ina uhakika wa kuyachukua majimbo iliyoyapoteza kwa kuwa imeshajua kosa lake.
Chanzo:Mwananchi
No comments:
Post a Comment