Boniface Meena
SAKATA la malipo ya Sh94 bilioni kwa Kampuni ya Dowans jana lilichukua sura mpya kufuatia baadhi ya wasomi na wanasiasa kuhoji sababu za mawakili walioiwakilisha Tanesco kwenye shauri hilo kutotoa utetezi unaobainisha kuwapo kwa mazingira ya rushwa katika mkataba huo.
Kadhalika, wamebashiri kuwa wakati sakata la Dowans likiendelea, huenda kuna sakata jingine linakuja kufuatia kampuni ya Richmond pia kuishtaki Tanesco.
Wasomi na wanasiasa hao walisema hayo jana katika mjadala kuhusu sakata la Dowans ulioandaliwa na Jumuiya ya Wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udasa), chini ya uenyekiti wa Dk Azaveli Lwaitama.
Akizungumza katika mjadala huo, Dk James Jesse alisema kuwa iwapo Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kibiashara (ICC), ingeelezwa mapema kuwa mkataba wa Dowans ulikuwa na mazingira ya rushwa basi Mahakama hiyo isingehangaika kushughulika kesi hiyo.
"Mkataba wa Dowans hauna tofauti na 'bogus treaty' (Mikataba ya udanganyifu) ya Sultan Mangungo wa Msovero, na tusubiri tukio jingine la Richmond dhidi ya Tanesco kwa kuwa tayari imeshaishtaki,"alisema Dk Jesse.
Dk Jesse aliyeuchambua mkataba wa Dowans kwa undani kabla ya kutoa maoni yake, alisema kuwa mpaka sasa kitu pekee ambacho Kituo cha Sheria na Haki za Binaadamu(LHRC), kinachoweza kufanya katika pingamizi lao mahakamani ni kutoa hoja ya kuwepo kwa mazingira ya rushwa katika mkataba huo.
"Kama mahakama itakubali hilo, tuangalie nini kitatokea,"alisema.
Kwa upande wake, mbunge wa Singida Mashariki kuptia Chadema, Tundu Lissu alisema kuwa ameshangazwa na wanasheria wa Tanzania waliokuwa wanasimamia kesi hiyo kwa kushindwa kuieleza ICC tangu mwanzoni kuwa mkataba huo ulikuwa na mazingira ya rushwa.
"Kwenye ushahidi walieleza hilo, lakini tatizo inakuwa ni kwamba halikuwa jambo la msingi kwa kuwa haikuwa moja ya mambo yaliyowekwa kwenye kesi ya msingi kabla ya kuanza,"alisema Lissu na kuongeza.
"Sasa hili jambo itabidi liamuliwe kwa maandamano kwa kuwa wananchi wanataka kujua nini kifanyike,"alisema Lissu.
Lissu naye alisema kuwa Watanzania wakae tayari kwa hukumu ya Richmond kwa kuwa tayari wameshaishtaki Tanesco.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Bashiru Ally alisema kuwa hivi sasa kuna matatizo makubwa ambayo yanahitaji kufanyiwa kazi na kwamba suala la Dowans ni la kisiasa zaidi.
"Inashangaza, wasomi wanavyokimbilia bungeni ili kutengeneza rushwa kubwa badala ya kuendeleza nchi. Dowans haitatusaidia kutokana na kutoangalia umuhimu wake,"alisema Ally.
Alisema kuwa sakata la 'Goldenberg' la Kenya ni sawa na Dowans jambo linalofanya wananchi waamini kuwa ni wakati wa Serikali kula.
"Siyo suala la sheria ni suala la siasa. Siasa mbaya ndizo zilizotuingiza hapa, tusimamie haya ya kulipwa yasitokee,"alisema Bashiru. "Masikini hatabiriki hivyo tusicheze nao,"aliongeza Bashiru.
Naye Dk Mushumbusi Kibogoyo alisema kuwa ni lazima wananchi waelewe nini kifanyike kuhusu Dowans iwapo ilipwe au isilipwe.
"Kama tukitaka watu waingie mitaani, lazima tujue tumewaandaa vipi na hali ilivyo kama Dowans ilipwe au isilipwe,"alisema Dk Kibogoyo
No comments:
Post a Comment