ANGALIA LIVE NEWS

Monday, February 28, 2011

Watanzania wadandia ndege ya Kenya nchini Libya

Click here for full size photo!Felix Mwagara na mashirika
WATANZANIA waliokwama nchini Libya, wamelazimika kupanda ndege ya Kenya iliyokuwa imebeba zaidi ya raia 100 wa nchi za maziwa makuu, waliondoka katika nchi hiyo yenye machafuko.
 
Habari zilisema raia hao, walisafirishwa Jumamosi iliyopita kwa ndege ya Shirika la Ndege la Kenya, iliyokuwa imezuiwa kutua katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Tripoli.

Badala yake, ndege hiyo ilitua katika Uwanja wa ndege wa Cairo, nchini Misri.
 

Hata hivyo baada ya mvutano, serikali ya Kanali Muammar Gaddafi anayekabiliwa na shinikizo la kumtaka aondoke madarakani, ilitoa idhini kwa ndege hiyo kutua katika Uwanja wa Tripoli. 

Habari zilizopatikana jana kutoka Kenya, zilisema tayari raia hao wa nchi za mazaiwa makuu, walishatoka nchini humo na walitarajiwa kutua Nairobi, jana usiku 

Habari hizo zilisema ndege hiyo yenye uwezo wa kubeba abiria 191, imebeba pia raia wa Uganda, Rwanda, Burundi, Lesotho, Zimbabwe na Afrika Kusini. 

Kwa mujibu wa Ofisa wa Mawasiliano wa Shirika la Ndege la Kenya, Chris Karanja, balozi za nchi hizo ziliwaomba kuwasafirishia raia wao na kwamba kwa kuzingatia ujirani mwema shirika, limetekeleza ombi hilo.
"Balozi nyingi zilituomba tuwasafirishe raia wao, na tumefanya hivyo kutokana na undugu tuliokuwa nao,"alisema Karanja.

Habari zaidi zilisema  maelfu ya raia wa kigeni wanaendelea kuondoka nchini Libya, ili kusalimisha maisha yao.

Serikali ya China, imetumia meli za kukodi ili zitumike katika kuwahamisha raia wake 3,000 hadi katika kisiwa cha Crete, nchini Ugiriki. 

Wakati huo huo, meli moja ya kivita ya Uingereza iliyowabeba mamia kadhaa ya raia wa  nchi 20,imewasili Malta. 

Taarifa ya mwandishi wa Reuters ambaye ni miongoni mwa waandishi habari walioalikwa na mtoto wa Gaddafi, alisema maelfu ya raia wa kigeni wanakimbilia uwanja wa ndege wa Tripoli, katika jitihada za kuondoka nchini humo.

Maelfu ya raia wa Misri pia wanaendelea kukimbia nchi hiyo ya jirani, kupitia mpaka wa magharibi.

India inasema imetuma ndege mbili na meli idadi kama hiyo, kuwahamisha raia wake 18,000 kutoka Libya. 

Meli mbili za jeshi la majini la Uturuki, zimeondoka katika mji wa Benghazi, zikiwa zimebeba watu 1,700 kutoka nchi 11.

Huko Dhaka jamaa za Wabangladeshi 60,000 waliokwama Libya wameishutumu Serikali ya Bangladesh kwa kupuuza kilio chao.


CHANZO:MWANANCHI

No comments: