Na Mohamed Hamad, Babati
KATIBU wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Bonga wilayani Babati, Manyara, Issa Mohamed (Kadogoo) amekatwa na kitu chenye ncha kali kwenye makalio yake na mtu ambaye hakufahamika jina mapema kwenye tukio lililodaiwa kuwa ni fumanizi.
Tukio hilo lilitokea Februari 21, mwaka huu katika Kijiji cha Bonga, eneo la Orng’adida wilayani hapa wakati katibu huyo alipodaiwa kumshika ugoni mtu huyo na mwanamke mmoja aliyefahamika kwa jina moja la Pili ambaye alidaiwa kuwa na uhusiano naye wa kimapenzi.
Shuhuda wa sakata hilo aliyeomba hifadhi ya jina lake, akizungumza na gazeti hili alisema baada ya katibu huyo kumwona Pili akiwa na mwanaume saa 4.30 usiku, alifuatilia hadi walipoingia kwenye shamba moja la mahindi kijijini hapo.
Alisema wakati katibu huyo akiwa na rafiki yake aliyefahamika kwa jina la Hamisi Masera , walifanya jitihada za kuwafuatilia hadi walipofanikiwa kuwafuma. Baada ya kuwakuta, walianza kumpiga vibao kijana huyo waliyemkuta akiwa amevua nguo, huku wakimtaka avae.
“Katibu huyo alimcharaza vibao kama vinne hivi huku akimhoji na kumtaka avae nguo. Jamaa yule alikuwa na maneno ya kejeli kila alipokuwa anapigwa na akawa anataka aongezwe kipigo. Baada ya kumaliza kuvaa nguo, alichomoa kisu chake na kumrarua katibu sehemu za makalio,” alisema shuhuda huyo
Baada ya kukata makalio alipiga mayowe kuomba msaada kwa jamii iliyokuwa katika maeneo hayo na walipofika walimkuta katibu huyo na rafiki yake ambaye naye katika jitihada za kumwokoa alichomwa kisu kifuani na mkononi. Wote walikutwa wamelala chini.
Habari zinasema wananchi hao waliwatafutia usafiri usiku huo kwenda Hospitali ya Mrara, Babati kwa matibabu ambapo katibu huyo alilazimika kushonwa nyuzi 25 kwenye makalio yake.
Aidha, Masera ambaye alichomwa kisu kifuani na kujeruhiwa sehemu za mkono wa kulia, naye alipata matibabu hospitalini hapo ambapo imeelezwa kuwa wote tayari waliruhusiwa baada ya hali zao kuwa za kuridhisha.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Parmena Sumary amekiri kutokea tukio hilo na kwamba mtuhumiwa anatafutwa na polisi.
CHANZO:GLOBAL PUBLISHERS
No comments:
Post a Comment