ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, March 1, 2011

Lowassa ashauri mishahara ya wafanyakazi ipande

Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa
Mussa Juma, Arusha

WAZIRI Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa, ameishauri Serikali kuunda tume ya kurekebisha mishahara ya watumishi wa umma ili iendane na hali ya maisha ya sasa.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Arusha jana, Lowassa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, alisema uchumi wa dunia sasa umeyumba na hivyo kusababisha vitu vingi kupanda bei. 

Kwa mujibu wa Lowaasa, kuendelea kuwalipa wafanyakazi mishahara kwa viwango vya sasa ni kuwapunguzia ari ya kutekeleza wajibu wao kwa umma.

Lowassa alitoa kauli hiyo muda mfupi baada ya kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), akitokea jijini Dar es Salaam.

Lowassa na Uchumi
Jana Lowassa ambaye katika mkutano huo alijikita zaidi kuzungumzia machafuko ya kidini yaliyotokea jimboni kwake Monduli katika mji wa Mto wa Mbu, ni muhimu sasa, wafanyakazi wa umma wakapata mishahara itakayokidhi gharama za maisha.

“Hali ya uchumi duniani sio nzuri na inasababisha vitu vingi  kupanda  bei kama  mafuta na nafaka hali ambayo imetokea nchi zilizoendelea na hivyo kuathiri hadi nchi  nyingine ikiwapo Tanzania,”alisema Lowassa.

Alisema machafuko yanayoendelea nchini Libya na kulipuliwa kwa visima nchini Iraq yamesababisha kupanda kwa kiasi kikubwa kwa bei ya mafuta katika soko la dunia.

Lowassa aliendelea kueleza kuwa kama Serikali ikiunda tume ya kupitia upya mishahara ya wafanyakazi, inapaswa kushirikisha viongozi wa vyama vya wafanyakazi, wataalamu wa uchumi na wadau wengine.

“Licha ya kuunda tume pia  Serikali nashauri  wataalam wa uchumi kutazama Bajeti ya Serikali ili kuona vitu gani vinaweza kupunguzwa bila kuathiri utendaji wa Serikali,”alisema Lowassa.

Lowassa pia alizungumzia mfumko wa bei wa vitu mbalimbali ikiwamo sukari na kueleza kuwa yote hayo yanasababishwa na kuyumba kwa uchumi wa dunia na sio tatizo la Tanzania pekee.

Vurugu za kidini
Akizungumzia vurugu za kidini zilizoibuka Mto wa Mbu hivi karibuni na kusababisha watu 12 kujeruhiwa na mali kadhaa kuharibiwa, Lowassa aliwataka wakazi wa mji huo kutulia na kuendeleza uhusiano mwema baina yao .

“Pale Mto wa Mbu kuna makabila zaidi ya 120  na muda mrefu wanakaa kwa amani hivyo kwa tukio hili naomba maelewano yaendelee kuwepo,”alisema Lowassa.

Lowassa pia aliviomba vyombo vya habari kuwa makini na migogoro ya kidini ili visije vikachochea hasa kwa kusema dini fulani ni sahihi na nyingine sio sahihi.

Katika siku za hivi karibuni vyama vya wafanyakazi vimekuwa vikiomba Serikali kupandisha mishahara hasa kutokana na kupanda wa gharama za maisha, ikiwepo bei za vyakula, usafiri na mahitaji mengine.


Msimamo wa Tucta
Kauli ya kiongozi huyo, Mbunge wa Monduli (CCM), imekuja wakati kukiwa na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (Tucta), likiendelea kuibana Serikali kuhusu suala la maslahi ya wafanyakazi.

Uhusiano baina ya Tucta na Serikali ya Awamu ya Nne umezorota kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa kutokana na kile kinachodaiwa na wafanyakazi kuwa ni Serikali kutotekeleza ahadi za kuboresha maslahi yao kwa muda mrefu.

Desemba 8, mwaka jana, Tucta baada ya kimya cha muda mrefu, walitangaza rasmi kuanza tena kwa mgogoro baina yao na Serikali wakiishinikiza iongeze mishahara ya wafanyakazi kuanzia Januari mwaka huu.

Ombi la wafanyakazi kupitia Tucta ni kutaka kima cha chini cha mshahara kuongezwa hadi kufikia Sh315,000/- kwa mwezi, kiwango ambacho Rais Jakaya Kikwete alishasema "hakiwezekani" na kwamba Serikali haina uwezo wa kulipa fedha nyingi kiasi hicho.

Katibu Mkuu wa Shirikisho hilo, Nocolaus Mgaya, ndiye amekuwa kinara wa wafanyakazi nchini katika kudai maslahi bora zaidi, hali ambayo ilisababisha Rais  Kikwete Mei 4, 2010 'kuwatisha', pale walipotaka kuandaa mgomo wa nchi nzima uliokuwa ufanyike Mei 5, mwaka huo.

Mvutano huo ulisababisha wafanyakazi kupitia Tucta kutangaza msimamo kwamba wasingempa kura mgombea yeyote wa kiti cha urais “asiyejali masilahi yao au yule aliyezikataa kura zao”.
Hata hivyo, baadaye wakati akizindua kampeini za kitaifa za CCM akiwania kurejea tena Ikulu, Agosti 21, 2010 katika Viwanja vya Jangwani, Kikwete alisema Serikali ilikuwa imepandisha mishahara ingawa si kwa kiwango cha walichotaka Tucta.

Msimamo wa Tucta ni kwamba kima cha chini cha mishahara ya wafanyakazi kilichoongezwa kutoka Sh 104,000 hadi Sh 135,000 kwa mwezini kidogo na kwamba hakuna uwiano mzuri baina ya watumishi wa kada za chini na wale wa ngazi za juu kama makatibu wakuu wa wizara na wakurugenzi wa vitengo mbalimbali serikalini.


CHANZO:MWANANCHI 

No comments: