1st March 2011
Yanga ililazimika kusubiri hadi dakika 13 kabla ya mechi kumalizika ili kupata goli walilolihitaji sana katika ushindi wa 1-0 dhidi ya Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Jamhuri, mjini Morogoro jana.
Alikuwa ni mshambuliaji Jerryson Tegete aliyefunga goli hilo likiwa ni lake la saba katika ligi kuu ya bara msimu huu lililotosha kuirejesha Yanga kileleni mwa msimamo.
Kwa ushindi huo Yanga imefikisha pointi 38, moja zaidi ya Simba iliyo katika nafasi ya pili ambayo hata hivyo ina mechi moja mkononi. Azam FC iko katika nafasi ya tatu kwa pointi 35.
Tegete alifunga kwa kichwa katika dakika ya 77 akiuwahi mpira wa kona uliopigwa na kiungo Kiggi Makassi katika mechi ambayo kipa wa Yanga Mghana, Yaw Berko kwa mara nyingine alikuwa shujaa akiokoa hatari za mara kwa mara langoni mwake.
Wenyeji hawakuonyesha kutishika na jina la wapinzani wao na wakawashambulia kila ilipowezekana lakini safu ya ulinzi ya Yanga ilikuwa makini na hadi mapumziko matokeo yalibaki kuwa 0-0.
Kipindi cha pili kilianza kwa mashambulizi ya pande zote lakini baada ya wenyeji kuwaandama Yanga kwa muda mrefu walijikuta wakifungwa goli dakika 13 kabla ya mchezo kumalizika na kukosa japo sare katika mechi hiyo ambayo kiungo wa zamani wa timu ya taifa, Athumani Idd 'Chuji' alirejea kikosini baada ya kuwa nje ya uwanja kutokana na kuwa majeruhi.
Kocha wa Shooting, Charles Boniface Mkwassa, ambaye ni nyota wa zamani wa Yanga, alisema baada ya mechi hiyo kwamba hana maoni kuhusu mchezo huo, lakini alielezea kutoridhishwa na viwango vya waamuzi wa Tanzania. Refa Thomas Mkombozi kutoka Kilimanjaro, ndiye aliyekuwa mwamuzi wa mechi hiyo.
Kocha wa Yanga, Sam Timbe alisema amefurahi kwamba wameibuka na ushindi lakini wachezaji wake hawakucheza vile anavyotaka na kwamba inaonekana kwamba bado hawajamuelewa.
Hata hivyo, Timbe alisema atarekebisha matatizo yaliyojitokeza katika mechi hiyo na nyingine kabla ya mechi yao ijayo dhidi ya watani zao wa jadi Simba itakayofanyika Jumamosi kwenye uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
JKT Ruvu watakuwa wenyeji wa timu ya mkiani ya AFC ya Arusha katika mechi pekee ya leo ya ligi hiyo wakati Azam watakuwa na fursa nyingine ya kurejea kileleni kesho wakati watakapowakaribisha 'vibonde' wengine wa ligi Majimaji ya Songea kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
Vikosi katika mechi ya jana vilikuwa; Ruvu Shooting: Mahmoud Mbulu, Michael Pius, Oscar Mkulula, George Hosei, Hamis Yakuti, Jumanne Juma, Rafael Keyala, Hassan Dilunga, Martin Mlolele, Revocatus Mariwa na Ayub Kitala.
Yanga: Yaw Berko, Shadrack Nsajigwa, Stephano Mwasika, Chacha Marwa, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Ernest Boakye/ Ibrahim Job, Nsa Job, Athuman Idd 'Chuji', Davis Mwape/ Idd Mbaga, Jerryson Tegete na Kiggi Makassy.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment