ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, March 1, 2011

Usiri watanda kambi za Simba, Yanga

Kocha wa Simba Patrick Phiri
Jessca Nangawe na Clara Alphonce
SIKU  nne kabla ya mchezo wa Ligi Kuu  Tanzania Bara baina ya watani wa jadi, Simba na Yanga, usiri kuhusu kambi za timu hizo mbili ndio umetawala.

Kwa nyakati tofauti jana, uongozi wa klabu hizo  ulieleza kuwa maandalizi yao  yatakuwa ya siri zaidi, ingawa imethibitishwa kuwa   Simba tayari wamekwenda Zanzibar na Yanga wataweka kambi yao Bagamoyo.

Kwa upande wake,Mwananchi iliarifiwa jana  kuwa  wachezaji wa Simba waliondoka jana alasiri kuelekea Zanzibar kwa ajili ya kuweka kambi yao kujiandaa na mchezo dhidi ya  watani zao, Yanga pamoja na maandalizi ya mechi ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya TP Mazembe.

Katibu Mkuu wa  klabu hiyo, Evodius Mtawala aliiambia  Mwananchi kuwa  timu yao iliondoka jana mchana  kwa ajili ya kwenda visiwani humo kujiandaa vyema na mchezo huo pamoja na maandalizi ya mchezo wao wa kimataifa  dhidi ya  Mazembe kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) badaye mwezi huu.

Alisema timu  imeondoka na wachezaji karibu wote isipokuwa wale ambao ni majeruhi na mara baada ya pambano lao na Yanga wataanza mikakati ya kukabiliana na Mazembe, Machi 20.

"Timu yetu inaondoka leo (jana) mchana na benchi zima la ufundi ambapo kama mnavyofahamu sisi tuna kazi kubwa mbili  zilizoko mbele yetu, moja ikiwa kuhakikisha tunalipa kisasi kwa Yanga waliotufunga kule mjini Mwanza katika mzunguko wa kwanza.

Pili ,  ni  kujiandaa na mchezo wa kimataifa ambao kwa sasa  tunaupa umuhimu mkubwa dhidi ya Mazembe,"alisema Mtawala.

Naye makamu mwenyekiti wa klabu hiyo, Godfrey Nyange 'Kaburu' alithibitisha kuondoka kwa timu hiyo  jana mchana kwa boti  kwenda visiwani humo kwa ajili ya kuweka kambi kujiandaa na mchezo huo wa Jumamosi.

Alisema kuwa wachezaji wote waliondoka wakiwa chini ya kocha Patrick Phiri na benchi la ufundi   na watarejea Dar es Salaam Ijumaa tayari kwa mchezo huo.

Phiri  kwa upande wake alisema kuwa atazitumia dakika za mwanzo za mchezo huo Jumamosi kufanya mashambulizi ya mapema ili waweze kuichanganya safu ya ulinzi ya Yanga na kupata bao la mapema.

Kwa upande wao, Yanga  ambao jana walikuwa wakicheza na Ruvu Shooting  mjini Morogoro hawakuwa wazi watakaa wapi kwa mazoezi hayo.

Wao waligoma kueleza wazi wapi wataweka kambi yao huku katibu mkuu wao,  Celestin Mwesingwa akisema kuwa mpaka jana walikuwa hawajui kambi hiyo wataweka wapi watajua baada ya kumalizika kwa mechi ya jana.

Hata hivyo, habari zilizopatikana jana zilieleza kuwa timu hiyo itakwenda  Bagamoyo kama ilivyoripotiwa awali.


CHANZO:MWANANCHI

No comments: