Advertisements

Friday, June 10, 2011

Motema Pembe waficha ujio wao

Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange `Kaburu`
Wapinzani wa Simba, timu ya DC Motema Pembe kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, inatarajiwa kuwasili nchini leo kimya kimya kwa ajili ya mechi yao ya kwanza ya Kombe la Shirikisho ambayo itachezwa keshokutwa kuanzia saa 9:30 alasiri kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange 'Kaburu', alisema kuwa wapinzani wao hao hawajatuma taarifa rasmi kwa maandishi lakini wamefahamu ujio wao huo kutokana na kupokea taarifa kutoka kwa wadau wa klabu hiyo wanaoishi Kinshasa.
Kaburu alisema kuwa mapokezi ya wageni hao yamekamilika na wanafanya hivyo ili kuepuka malalamiko yoyote ambayo yanaweza kutolewa na wapinzani hao.
"Hawajatuambia rasmi kama kanuni zinavyoeleza, lakini sisi tuko tayari kwa kila jambo kuhusiana na mechi hiyo itakayochezwa Jumapili alasiri," alisema Kaburu.
Alisema waamuzi wa mchezo huo kutoka Nigeria, Auwalu Barau, Babaa Abel, Wokoma Solomon na Amao Opeyeni pamoja na Kamishna wa mchezo huo, Feisal El Hakim wa Sudan watawasili leo jioni.
Alisema pia tiketi za mchezo huo zitaanza kuuzwa leo asubuhi katika vituo mbalimbali jijini Dar es Salaam na wanawaomba mashabiki wa soka nchini kujitokeza nchini kuwashangilia kwa sababu Simba inawakilisha nchi kwenye mashindano hayo ya kimataifa.
Aliongeza kwamba baada ya kumaliza mechi hiyo ya Jumapili, wachezaji wa Simba wataendelea na mazoezi na wataondoka nchini Juni 16 kuelekea Kinshasa tayari kwa mchezo wa marudiano ambayo utachezwa kati ya Juni 17 na 19 jijini humo.
Alisema kwamba pia wawakilishi hao pekee wa nchi kwenye mashindano ya kimataifa mara baada ya kumaliza mechi hizo mbili wataendelea kujifua na kusubiri michuano ya Kombe la Kagame ambayo itafanyika jijini kuanzia Juni 25 kwa kushirikisha klabu zaidi ya 12 za ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati pamoja na timu nyingine mbili zitakazoalikwa.
Wakati huo huo, Simba itamkosa kiungo wake, Jerry Santo, katika mchezo wa keshokutwa kutokana na kuwa na kadi mbili za njano pamoja na beki, Meshack Abel, ambaye ni majeruhi.
Simba ikifanikiwa kuitoa DC Motema Pembe itakuwa imefuzu kwa hatua ya nane bora ya mashindano hayo ya kila mwaka.
CHANZO: NIPASHE

No comments: