ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, July 12, 2011

Jussa amwambia Sitta Zanzibar haitaki kubebwa

Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta
Chama cha Wananchi (CUF) kimezidi kuelekeza makombora kwa viongozi wandamizi serikalini wanaopinga kuwepo kwa serikali tatu katika sura ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Ijumaa iliyopita, wakati anajibu hoja za Wabunge waliochangia hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais mjini Dodoma, Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, alisema kufufua serikali ya Tanganyika ni sawa na kutengeneza mpinzani wa Zanzibar.

Sitta ambaye alikuwa Kaimu Kiongozi wa shughuli za serikali Bungeni, pia alisema Muungano wa serikali mbili una manufaa zaidi kwa upande wa Zanzibar, ambao unabebwa kutokana na uwezo wake mdogo wa kuchangia gharama za huduma, kama vile za umeme na uanachama katika Muungano.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara huko Bububu, mjini hapa, Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Ismail Jussa Ladhu, alisema kupingwa kwa Muungano wenye sura ya serikali tatu kutonatokana na hofu ya muda mrefu ya Tanzania Bara kupoteza fursa ya kunufaika, kiuchumi kupitia mgongo wa Zanzibar.
Jussa alisema Muungano wenye sura mbili unainufaisha zaidi Tanzania Bara kutokana na mfuko wa serikali ya Muungano ambao uendeshaji wake unakosa uwiano katika suala la mgawanyo wa fedha kati ya pande hizo mbili za Muungano.
Vifungu vinavyoongoza matumizi ya fedha kutokana na mfumo huo, vinapaswa kueleza kiasi gani ni kwa ajili ya Tanganyika na kipi kinaenda Zanzibar… matumizi ya mfuko hayana maslahi kwa Zanzibar,” alisema Jussa.
Alisema Zanzibar haiwezi kufurahia sura ya Muungano wa serikali mbili kwa sababu inanyonywa na Tanzania Bara na ndio maana viongozi, kama Waziri Sitta na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, hawataki serikali tatu.
Ukiwa na serikali mbili, mapato yote ya serikali ya Muungano yanabaki Tanzania Bara, zikiwa tatu yatakwenda kwa serikali ya Muungano, ya Tanganyika na ya Zanzibar kwa uwiano unaoeleweka,” alisema Jussa.
Alisema maelezo ya Waziri Sitta dhidi ya Zanzibar ndani ya Bunge la Muungano ya kutumia vitu na huduma za umeme kwa wananchi wa pande hizi mbili, ni ishara ya nia mbaya ya Tanzania bara kwa Zanzibar.
Sitta asitulaghai kwamba chini ya muundo wa serikali tatu, Tanganyika ingechoka kuibeba Zanzibar na Muungano ungevunjika, Zanzibar hatupewi bure umeme, tunanunua, sawa na Kenya na Uganda wanavyouziana huduma hiyo,” alisema.
Alisema ujenzi wa miundombinu ya umeme unaotumika visiwani kutoka Ras Kilomoni uligharamiwa na serikali ya Zanzibar. “Badala ya kutusimangwa, Zanzibar tulipaswa kulipwa faida kwa kuwekeza katika umeme huo.”
Katika kauli yake Bungeni Dodoma, Waziri Sitta pia alisema Muungano wa serikali mbili ulipata baraka zote za Mwalimu Nyerere na Mzee Abeid Karume na kwamba katika hatua fulani, Rais huyo wa kwanza wa Zanzibar aliwahi hata kupendekeza kuundwa kwa serikali moja.
Juu ya mchakato Katiba mpya, Jussa alisema Serikali ya Mapinduzi yenye muundo wa Umoja wa Kitaifa, imesimama imara kuhakikisha muswada wa mapitio ya Katiba mpya unapelekwa bungeni ukiwa umelinda maslahi yote ya wananchi wa Zanzibar yaliyomo katika Muungano.
CHANZO: NIPASHE

No comments: