Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro kwa kushirikiana na maafisa biashara imefanikiwa kukamata mifuko 2029 ya sukari yenye uzito wa kilogramu 50 kila mmoja iliyokuwa inatoroshewa Kenya.
Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro, Absalom Mwakyoma, alithibitisha kukamatwa kwa shehena hiyo kati ya Septemba 21 na 26, mwaka huu katika wilaya za
Moshi Vijijini na Rombo.
Alisema polisi pia walivunja ghala moja eneo la Himo na kufanikiwa kukamata mifuko 729 ya sukari, ambapo hadi sasa muhusika wa ghala hilo hajajitokeza huku baadhi wa wamiliki wa magari yaliyokamatwa wakishindwa kujitokeza.
Mwakyoma alisema sukari mifuko 230 ilikutwa katika gari lenye namba za usajili T 960 AAV, mifuko 320 kwenye gari lenye namba za usajili T 508 AXY, mifuko 240 kwenye gari lenye namba za usajili T 698 AXY yote aina ya Fuso.
Alisema katika Wilaya ya Rombo magari matatu yalikamatwa yakiwa na shehena ya sukari, ambayo yalikamatwa Septemba 21, mwaka huu katika msako uliofanyika kwa siku nzima na kwamba sukari hiyo inasadikiwa ilikuwa inasafirishwa kwenda nje ya nchi.
Alisema katika zoezi hilo magari yenye namba za usajili T 284 AFZ aina ya Fuso, mali ya Emmanuel Kisamo ikiwa na mifuko 330, T916 AHQ aina ya Fuso ikiwa na mifuko 100 na yenye namba za usajili T 719 AAQ aina ya fuso ilikutwa na mifuko 80, mali ya Damas Raymond, mkazi wa Dar es Salaam.
“Magari yote yapo kituo cha polisi Rombo na Himo yakisubiri maofisa wa Mamlaka ya Mapato na maafisa biashara wa wilaya hizo kuona kama taratibu, kanuni na sheria za kuletwa sukari zilifutwa,” alisema.
Kamanda Mwakyoma alisema msako huo ni mwendelezo wa kila siku na kwamba kwa wale ambao magari yao yamekamatwa ni vyema wakajitokeza sasa, vinginevyo Polisi itatoa kibali cha kuyafikisha mahakamani ili
iweze kuuzwa kwa wananchi kwani sukari ni mali inayotakiwa kuhifadhiwa
kwa usalama zaidi.
Wiki iliyopita, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, akiwa katika ziara yake mkoani Mara, alisema kama polisi watashindwa kazi ya kuzuia sukari kutoroshewa nje ya nchi, serikali itaamua kutumia Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kudhibiti vitendo vya utoroshaji wa sukari hiyo kwenda nje ya nchi.
Pinda, alisema kuwa baadhi ya askari polisi wamekuwa wakishirikiana na wafanyabiashara kusafirisha sukari kwenda nje na kwamba hiyo ndiyo sababu inayochangia kushamiri kwa tatizo hilo.
Siku moja baada ya Pinda kutoa kauli hiyo, Jeshi la Polisi lilitoa taarifa likisema kuwa halijashindwa kufanya kazi hiyo isipokuwa halikuwa na taarifa za kutosha kuhusiana na vitendo hivyo.
Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Robert Manumba, alisema kuwa kutokana na hali hiyo, polisi wameanzisha opereshani ya wiki mbili kuwasaka wanaotoroshea sukari nje.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment