Askari wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya, G 2795, PC Meshack (28), ameuawa kwa kupigwa na kitu chenye ncha kali na watu wasiofahamika.
Kamanda wa Polisi mkoani Mbeya, Advocate Nyombi, alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 5:15 usiku katika maeneo ya Mabatini jijini Mbeya.
Kamanda Nyombi alisema watu wanane wanatiliwa shaka kuhusika katika tukio hilo, lakini hadi jana hakuna mtuhumiwa aliyekamatwa.
Alisema marehemu alifariki dunia njiani wakati akipelekwa katika Hospitali ya Rufaa Mbeya kwa matibabu.
Kamanda Nyombi alisema askari huyo alivamiwa na watu hao wakati akirejea nyumbani kwake ingawa hakueleza mahali alipokuwa akitokea.
Alisema askari Meshack alikuwa ni fundi wa magari ya jeshi hilo na kuongeza kuwa mwili wake umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mbeya.
Katika tukio lingine lililotokea maeneo ya Forest ya Zamani lililopo jijini Mbeya, Mhasibu wa Hospitali ya Rufaa Mbeya, Moses Mwazembe (35), alivamiwa na watu wasiofahamika, waliojitambulisha kuwa ni sungusungu wakati akirejea nyumbani.
Kwa mujibu wa Kamanda Nyombi, watu hao walimpiga na kumpora fedha ambazo kiasi chake hakikufahamika pamoja na simu yake ya mkononi.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment