Maafisa wa kimataifa wameelezea wasiwasi kuhusu zaidi ya watu 200, 000 ambao wamejikuta katikati ya mapigano makali katika miji ya Sirte na Bani Walid nchini Libya.
NATO imesema wapiganaji wanaomtii Kanali Muammar Gaddafi wanajificha katika maeneo ya raia, na kuwaweka watu hao katika hatari kubwa.
Msemaji wa NATO kanali Roland Lavoie amesema katika miji hiyo ambayo bado iko chini ya wapiganaji wanaomtii Gaddafi, inakabiliwa na uhaba wa maji ya kunywa, chakula na dawa.
Wapiganaji kutoka Baraza la Mpito la Taifa la Libya wamezidi kushambulia miji hiyo miwili.
Hayo ni maeneo makuu mawili ya mwisho ambayo bado yako chini ya udhibiti wa wafuasi wa Gaddafi.
Baraza la Mpito la Taifa, NTC, linasema ni suala tu la wakati kabla ya miji hiyo kutwaaliwa na majeshi yake.
Lakini Kanali Lavoie amesema wafuasi wa Gaddafi wanakataa kushindwa, akisema "Ikiwa hatua ya mwisho, wanajificha katika maeneo ya raia."
Kanali Lavoie na Kamati ya Kimataifa ya Chama cha Msalaba wameonya kuwa hali inayowakabili wananchi hao inazidi kuwa ya hatari.
Kama kuna mashaka yoyote kama majeshi yanayomtii Gaddafi katika mji wa Sirte wangeonyesha upinzani mkali dhidi ya majeshi ya Baraza la Mpito la Taifa, basi hali hii ndiyo inayodhihirisha mashaka hayo.
Tuko katika barabara ya pwani ambayo inaingia katika mji wa Sirte kutoka kaskazini, katika jumba ambalo majeshi ya zamani ya waasi wameketi nyuma ya ukuta, wakijificha kutokana na mapigano makali ikiwa ni umbali wa karibu kilomita moja mbele yetu. Mapema, kulikuwa na vifaru vya kijeshi na makombora yakirushwa katika kuelekea mji wa Sirte.
Ni vigumu kufahamu kuhusu idadi halisi ya wafuasi wa Gaddafi wanaopigana katika mji wa Sirte, lakini uhakika ni kwamba kuna wapiganaji wa kuvizia na wanarusha makombora. Mapigano haya yanaingia katika mitaa, hali inayowatia watu wasiwasi, hususan kwa raia waliobakia katika mji huo.
Raia wameendelea kuukimbia mji wa Sirte, wakati inaripotiwa kuwa ukosefu wa maji safi ya kunywa kunatishia kuzuka kwa magonjwa ya mlipuko.
"Hakuna chakula, hakuna umeme.here's no food, no electricity. Tulikuwa tunakula mikate tu," mkazi wa Sirte Saraj al-Tuweish ameliambia Shirika la Habari la Ufaransa, AFP wakati akiondoka katika mji huo jana.
"kwa siku kumi nilikuwa najaribu kuondoka na kila wakati wanajeshi walikuwa wakiturejesha. Mapema leo asubuhi tulitumia barabara mbaya na kuweza kutoroka."
Mashuhuda katika mji wa Sirte wanaelezea kuwepo hali ya ghasia wakati wapiganaji wa NTC wakijaribu kusonga mbele kuingia katika mji wa Sirte.
Walijikuta katika mapigano makali kutoka kwa wapiganaji watiifu wa Gaddafi, na vituo vya televisheni vinavyounga mkono NTC wameripoti kuwa askari wao waliuawa katika mapigano hayo.
Inafikiriwa kuwa Kanali Gaddafi bado yuko nchini Libya - huenda katika mji wa Bani Walid au Sirte.
Lakini watu wake wa karibu tayari wameikimbia nchi hiyo.
Binti yake Aisha alitorokea Algeria wiki kadhaa zilizopita, na ameonekana katika televisheni ya kituo cha Arrai TV nchini Syria akiwaambia watazamaji kuwa baba yake ana afya njema na anapigana bega kwa bega na majeshi yake.
Hata hivyo maafisa wa Algeria, walimwaambia Jumanne, wiki hii kuacha kujiingiza katika siasa.
Jumanne, Arrai TV ilionyesha picha ambazo kituo hicho kinasema zilipigwa tarehe 20 Septemba wakati mtoto wa kiume wa Kanali Gaddafi Saif al-Islam akiongoza askari.
Saif al-Islam, ambaye aliwahi kusemwa kuwa angemrithi baba yake, bado anajificha na kwa wiki kadhaa hajaonekana hadharani.
No comments:
Post a Comment