Ni furaha kuwa na amani ya kudumu na mwenzi wako. Inauma pale migogoro inaposumbua uhusiano. Si jambo jema kutumia muda mwingi kutatua migogoro badala ya kupanga maendeleo ya kimaisha na kuboresha penzi. Inafurahisha ukiwa na moyo tulivu na linapokereketa huzaa maumivu ya hisia.
Yote kwa yote, ni vema mtu anapoamua kuingia kwenye uhusiano wa kimapenzi awe amejiandaa kupenda, kuheshimu, kulinda, kunyenyekea na kadhalika. Kama hajajiweka tayari kwa vitu hivyo, asithubutu kumcheza shere mwenzie. Mapenzi yanabeba uhai wa mtu, hayajakufika tulia au uliza usimuliwe.
Nimekuwa nikitaka kila mtu ajue hili kwamba wewe unaweza kuwa mtu tu duniani. Ukijitazama thamani yako ni ndogo, usipokuwepo ni familia yako tu ndiyo inayoweza kubaini upungufu. Dunia haitotetereka kwa namna yoyote ile. Ukitembea ni mwepesi na unapigwa vikumbo na wanaojiona wana mbavu nene kuliko wewe.
Pamoja na yote hayo, ndani ya ulimwengu wa kimapenzi wewe ni dunia ya mwenzi wako. Vivutio vyote unavyoviona ulimwenguni haviwezi kumpa amani ikiwa wewe hujataka. Tabasamu lako kwake hujenga utulivu wa moyo wake na kuona siku za kuishi zimeongezeka, kwahiyo ni vema kuheshimu.
Hakuna linalouma moyo kama mtu kuachana na aliyempenda. Moyo husafiri kilometa nyingi kwa kuwaza. Hakukosea aliyesema sikitiko la mahaba linashinda msiba. Lakini yote hayo yanaweza kuepukika na kukaa mstari ulionyooka endapo mawasiliano yatabeba umuhimu unaotosheleza na kusimama kwenye nguzo zake kuu.
MAWASILIANO: Ni nguzo kuu ya uhusiano. Ikiimarishwa huchochea amani ya kudumu lakini kinyume chake ni kichocheo cha wapenzi kuachana. Ni vizuri kujifunza lugha inayoweza kukufanya uelewane na mwenzako. Sauti yako ukiwa mtaani itofautiane na ile ambayo unaitumia chumbani.
Pengine una kawaida ya kutoa majibu ya mkato unapokuwa unazungumza na rafiki zako, lakini tabia hiyo hutakiwi kuizoea pale unapokuwa na mwenzio chumbani. Ikiwa umezoea kuwaita wenzako: “Wewe!” Mwenzi wako hutakiwi kumwita hivyo.
Ni elimu ambayo kila mtu anatakiwa kuwa nayo kwamba kutofautisha maeneo ni jambo la busara. Kwamba sura yako iwe nyingine unapokutana na watu wa mitaani, itofautiane unapokuwa na wazazi, vivyo hivyo pale ambapo upo sehemu ‘spesho’ na mwenzi wako.
Lazima uwe unabadilika kama kinyonga. Ukiwa kazini mbele ya watu unaowaongoza unazungumza kwa sauti ya amri, lakini hiyo hupaswi kuitumia unapokuwa na wazazi wako. Unaongea kwa sauti kali ya kuamrisha mbele ya baba yako, hiyo adabu umefundishwa wapi?
Kuna lugha ya kuzungumza ukiwa na mwenzi wako. Ni mwiko kutoa sauti ya kuamrisha. Ni vizuri kumnyenyekea lakini si katika kiwango ambacho kitakufanya uonekane una kasoro za kisaikolojia. Tawile kwa kila linalosemwa na mpenzi wako hairuhusiwi, unatakiwa kuweka mbele hisia zako.
Upole kupitiliza hauna maana kwamba wewe ni mpenzi sahihi. Eti, utaonekana una nidhamu na unamsikiliza vizuri mwenzio, la hasha! Utatambulika kuwa mtu hai kulingana na jinsi akili yako inavyofanya kazi. Namna hisia zako zinavyoonesha uhai unapoguswa na matukio mbalimbali ndivyo na ubinadamu wako unavyosomeka.
Unahoji mambo kwa sauti yenye ujazo wa kutosha, unachukia pale unapoona mambo hayajaenda sawa, unaumia pale unapotendwa na unafurahi mipango inapokuwa chanya. Hii ndiyo mantiki ya kukutaka uwe na akili hai. Itashangaza umepata habari kwamba mwenzi wako yupo gesti na mpenzi mwingine halafu utabasamu.
Sumu hatari inayosababisha mmomonyoko wa ndoa au uhusiano wa kimapenzi kwa watu wengi ni kushindwa kujipanga kimaeneo. Ratiba za ofisini kuingiza nyumbani. Marafiki kuathiri taratibu za mapenzi yenu, ingawa kila kitu kina umuhimu wake kulingana na wakati husika.
Umeudhiwa na wafanyakazi wenzako kazini, unatakiwa kuweka hekima mbele. Unarudi nyumbani ukiwa na imani kwamba huko utakutana na mwenzi wako na ndiye mfariji wako. Kichwa kizito, basi mueleze mwenzio ajue kinachokusibu kuliko kumpa majibu ya mkato. Itakuharibia badala ya kukusaidia
Ninachosisitiza hapa ni kuwa uhusiano wa aina yoyote unadumishwa na mawasiliano.
Ninachosisitiza hapa ni kuwa uhusiano wa aina yoyote unadumishwa na mawasiliano.
Lugha yako mbele ya mwenzi wako ina nafasi kubwa ya kukufanya uendelee kufurahia penzi lake. Kinyume chake unaweza kujikuta ni kero kwake. Atakuvumilia mwisho atachoka kwa sababu hujui kubembeleza, unapenda kuamrisha.
www.globalpublishers.info
No comments:
Post a Comment