Yapata kipigo Mapinduzi Cup
Huku wakiwa na kumbukumbu ya kuwashuhudia watani zao wa jadi, Yanga wakiumbuka pia kwa kulala bao 1-0 katika mechi yao ya ufunguzi ya Kundi B dhidi ya Mafunzo juzi usiku, Simba walitarajiwa kupata ushindi na kuwapa mashabiki wao jeuri ya kuwatambia ‘Wanajangwani’.
Hata hivyo, ni wao waliojikuta wakigeuziwa kibao mbele ya maelfu ya mashabiki waliofika uwanjani baada ya kutanguliwa kwa mabao 2-0 kutokana na magoli yaliyofungwa na Ali Othman Mmanga katika dakika ya 55 na Ali Bakari aliyeongeza la pili kwa kichwa katika dakika ya 65.
Kona ya Ramadhani Singano ilisababisha piga nikupige langoni mwa Jamhuri na beki Shomari Kapombe akafunga kwa shuti lililomshinda kipa Jafar Said wa Jamhuri na kutinga wavuni katika dakika ya 74.
Awali, timu zote zilikuwa zikishambuliana kwa zamu. Jamhuri waliongeza kasi baada ya kuanza kwa kipindi cha pili na kujipatia bao la utangulizi baada ya beki wa Simba Kevin Yondani kushindwa kuumiliki mpira ulioonekana ‘rahisi’ na Mmanga akawaadhibu kwa kumvisha kanzu maridadi kipa Ali Mustafa ‘Bartez’ kabla ya kuutumbukiza mpira wavuni.
Makosa mengine ya beki Juma Nyoso ndani ya dakika moja tangu aingie uwanjani kuchukua nafasi ya Victor Costa yalitumiwa vyema Bakari kwa kuifungia Jamhuri bao la pikli katika dakika ya 65.
Baada ya bao hilo, Simba walicharuka kutaka kusawazisha kupitia kwa washambuliaji wao wa kimataifa, Felix Sunzu kutoka Zambia na Gervais Kago wa Jamhuri ya Afrika ya Kati. Hata hivyo, mabeki wa Jamhuri walisimama imara na hata alipoingia Haruna Moshi ‘Boban’ katika kipindi cha pili, bado Simba walishindwa kubadili matokeo.
Mgeni rasmi katika mechi hiyo iliyochezeshwa na refa Ali Juma Kombo alikuwa ni Waziri wa Ardhi, Makazi, Maji na Nishati wa Serikali ya Mpainduzi ya Zanzibar, Ali Juma Shamhuna.
Katika mechi iliyotanguliwa kuchezwa mchana jana, Miembeni United walishinda kwa bao 1-0 dhidi ya ‘maafande’ KMKM, mfungaji akiwa ni Issa Othamn katika dakika ya 36.
Mashindano hayo yanaendelea tena leo wakati Yanga itakaposhuka dimbani kucheza dhidi ya Kikwajuni na Mfaunzo wakiwavaa Azam ambao walianza vyema juzi kwa kushinda 3-1 dhidi ya Kikwajuni.
Vikosi:
Simba: Ali Mustafa, Nassor Masoud, Shomari Kapombe, Kelvin Yondani,Victor Costa/Juma Nyosso (dk.64), Jamal Mkude, Edward Christopher, Abdallah Seseme, Felix Sunzu, Gervais Kago, Ramadhani Singano
Jamhuri: Jafar Said, Salum Suleiman, Mrisho Ahmad, Mfaume Shaaban, Hussein Omar, Juma Othman, Bakari Khamis, Suleiman Nuhu, Ali Othman, Ali Salum,
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment