ANGALIA LIVE NEWS

Friday, January 6, 2012

Hamad Rashid: Mimi bado ni mbunge

Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohammed akionyesha waandishi wa habari baadhi ya kadi za wananchama wa Cuf alizodai zimerudishwa na wanachama walipopinga uwamuzi wa Baraza Kuu la Uongozi la Cuf wakuwavua uwanachama yeye na wenzake watatu , jijini Dar es Salaam jana. Picha na Edwin Mjwahuzi
Waandishi Wetu
MBUNGE wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed, amepinga uamuzi wa Baraza Kuu la Uongozi la Chama Cha Wananchi (CUF) kumvua uanachama, akisema ni batili na umekiuka amri ya Mahakama.

Wakati Hamad akitoa tamko hilo, Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, John Tendwa amekilipua CUF, akisema uamuzi wake wa kumfukuza uanachama Hamad, haukuzingatia maslahi ya wapiga kura wa Jimbo la Wawi, bali matakwa ya wachache ndani ya chama hicho.
 
Licha ya kuwepo zuio la mahakama, juzi Baraza Kuu la Uongozi la CUF, lilimvua uanachama Hamad Rashid na washirika wake watatu ambao ni  Mjumbe wa Baraza Kuu (Tanga), Doyo Hassan Doyo, Mjumbe wa Baraza Kuu (Pemba), Shoka Khamis Juma na Juma Saanane ambaye ni Mjumbe wa Baraza Kuu Unguja.

Hatua hiyo ilimfanya Hamad kuitisha mkutano na waandishi wa habari jana na kutoa tamko kuhusu uamuzi huo ambao aliuita kuwa ni batili kutokana na kukiuka amri ya Mahakama kuzuia mkutano.

Alisema muda mfupi kabla ya tangazo la kufukuzwa kwao uanachama, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ilitoa amri ya kuzuia kuendelea kwa kikao cha Baraza kuu, lakini baraza hilo lilikaidi na kuwafukuza.

Mbunge huyo alisema: “Niliwaomba wanipe muda wa kujitetea kama wao walivyochukua muda wa kunihukumu, wakakataa. Kikao kile kilikuwa na watu wazito kama Waziri wa Sheria wa Zanzibar, Jussa, Taslima na Makamu wa Rais wa Zanzibar, wote wakiwa wanasheria, lakini wameshindwa kufuata sheria.”

Hamad Rashid alihoji, “Kiongozi wa Serikali kama Maalim Seif anakataa kutii amri halali ya mahakama? Akija kuwa rais itakuwaje? Nimeogopa sana?”

Hata hivyo, Hamad na wenzake walisema wataendelea kupigania haki yao ndani ya CUF mpaka ipatikane.
"Tunaheshimu uamuzi wa Mahakama. Kwa amri hiyo uamuzi wa Baraza Kuu ni batili. Bado sisi ni wanachama halali..., bado mimi ni mbunge na tuna mashiko ya kuendelea kufanya kazi za chama,” alisisitiza.
Alisema, “Jana (juzi) nilipata simu zaidi ya 15 za wanachama kutoka mikoani akiwemo aliyekuwa mbunge wa Chadema Jimbo la Tarime, Charles Mwera wakiniunga mkono."

"Wana CUF mikoani wametangaza kutuunga mkono. Mwanza wameandaa maandamano, Tanga wamesema hadi leo jioni watakusanya kadi 2,000 kwa Dar es Salaam Temeke wameshakusanya kadi 600 na mikoa mingine mingi”. Alisema hukumu dhidi yao ilikuwa imeshaandaliwa hata kabla ya kusikilizwa na kwamba hata Kamati ya Nidhamu iliyowahoji haikuwa halali kikatiba.

“Tumefanya mabadiliko ya Katiba ya chama mara mbili. Kifungu cha 81 cha Katiba ya chama kinaitaka Kamati ya Katiba iidhinishwe na Baraza Kuu, lakini wajumbe wote wa kamati ile wanakaimu nafasi zao. Makamu mwenyekiti wa chama huyo huyo ndiyo aliyeongoza kikao cha Kamati ya Nidhamu na huyo huyo ndiye aliyeongoza Baraza Kuu kutuhukumu,” alisema.

Alisema  Baraza Kuu halikutenda haki ya kusikiliza kila upande na kuongeza: “Kwa kuzingatia ‘natural justice’, Baraza Kuu limepoteza uwezo wa kusikiliza na halina sifa ya kutenda haki. Baraza hilo lenye wanasheria wengi, lakini halikutupa nafasi ya kutusikiliza.”

Tuhuma dhidi yake
Kuhusu tuhuma alizopewa kabla ya kufukuzwa, alisema  Kitabu chake cha ‘Yaliyojiri’ alichokitunga mwishoni mwa mwaka jana ndicho kimesababisha yote.Katika kitabu hicho, Hamad  ameweka barua aliyowaandikia viongozi wa chama hicho akiwaeleza mwenendo mbaya wa chama hicho.

Hata hivyo, Hamad Rashid alisema uongozi wa chama hicho akiwemo mwenyekiti  Profesa Ibrahim Lipumba, walimwonya asiendelee kukisambaza kitabu hicho naye akaacha.

“Hivyo nimehukumiwa kwa kutoa kitabu hicho wakati tayari nilishaacha kukisambaza. Fedha iliyotumika kutufukuza ingetosha kabisa kugharimia matawi mikoani. Waulizeni nguvu waliyotumia kwenda Mwanza, kuzunguka Zanzibar, Lindi na Mtwara yote kuwaambia kuwa eti Hamad ni msaliti” alisema na kuongeza:,
“Mimi kama nimetumia fedha basi ni Sh 500,000 tu, 250,000 kuimarisha tawi la Kosovo na nyingine tawi la Chechnya. Fedha za walipa kodi na michango ya wabunge yote imetumika kunishitaki mimi niliyejitolea kusema ukweli.”

Kauli ya Tendwa
Kwa upande wake Tendwa, alisema uamuzi huo wa kumfukuza Hamad Rashid ambaye ni mbunge wala kujali maslahi ya wapiga kura wa Wawi bali maslahi ya chama.

Tendwa alisema hayo jana Ikulu jijini Dar es Salaam alipokuwa akijibu maswali ya waandishi wa habari baada ya kuhudhuria hafla ya kuwaapisha viongozi wapya wa Tume ya Taifa ya  Uchaguzi (NEC).

Alisema ni muhimu vyama vikaweka maslahi ya wapiga kura mbele kwa kuwa, ndiyo wanaomchagua mwakilishi wao na si chama kinachowachagulia.

"Tunaweza tukabadilisha mifumo ya uchaguzi, chama kinapomfukuza mbunge ni lazima kimfikirie mpigakura atakuwa katika hali gani na pia suala la gharama lazima lifikiriwe,"alisema Tendwa.

Msajili huyo mwenye dhamana na ustawi wa vyama vya siasa nchini, alisema ni muhimu mpigakura akapewa nafasi ya kufanya uamuzi huo kama anavyofanya wakati anapomchagua mbunge wake.

"Busara inahitajika katika kufanya uamuzi huu ili isiwe ni tabia na desturi ambayo tunajiwekea,"alisema Tendwa.

Mwenyekiti wa UDP na mbunge wa Bariadi Mashariki, John Cheyo alisema walichofanya CUF ni kukiuka sheria mama ya nchi ambayo ni Katiba.

Alisema kwa mujibu wa Katiba, mbunge atakaa katika kiti chake kwa miaka mitano na utaratibu wa kumwondoa ni katika Uchaguzi Mkuu.

"Katika nchi tuna sheria mama ambayo inatamka rais atatawala miaka mitano ukimwondoa hapo katikati unatafuta matatizo  hivyo kwa mbunge,"alisema Cheyo.

Alisema kitendo kilichofanya na CUF na NCCR ni kutafuta matatizo nchini na vurugu badala ya kujenga demokrasia.

CUF: Hatuendeshwi na Mahakama

Kwa upande wa uongozi wa CUF umetetea uamuzi wake wa kuwafukuza  wanachama wake wanne na kuwaonya wengine 10, huku kikisema kimezingatia katiba yake.

Chama hicho pia  kimekanusha madai ya kupokea amri ya mahakama ya kuzuia mkutano huo, uliomalizika juzi kwa kuwafukuza wanachama wanne na kuwavua nyadhifa za uenyekiti na wanachama wanne.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Bara, Julius Mtatiro alisema: “CUF hatujapokea pingamizi la Mahakama  kuzuia mkutano wa Baraza  Kuu na  kama amri hiyo ingekuwa sahihi kama tungeletewa juzi, (Jumatatu) na si siku ya mkutano.”

Mtatiro alisema kimsingi, mahakama haina uwezo wa kuzuia mkutano wa chama cha siasa kama ulikwishaanza kwa kuwa chama hakiongozwi na mahakama.

“Mahakama yoyote haina uwezo wa kuzuia mkutano wa chama cha siasa uliokwishaanza, chama hakiongozwi na mahakama bali kila chama kinaongozwa na  katiba za vyama vyao ambazo zinatambuliwa na  Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alisema Mtatiro.

Katika mkutano huo, CUF  kilitangaza kuwavua uenyekiti wanachama wake wanne katika Wilaya za  Ilala, Temeke jijini Dar es Salaam na Nachingwea Mkoa wa Lindi.
Waliovuliwa nyadhifa zao za uongozi ni waliokuwa wenyeviti katika Wilaya za Ilala, Don Waziri, na katibu wake Masaga Masaga, Temeke, Mohamed Albadawi na mwenyekiti wa Nachingwea, Haji Nanjase.

Mtatiro alisema baraza lilipokea majina ya watuhumiwa 14 akiwamo Hamad Rashid na baada ya kuwahoji lilijiridhisha kwamba 12 kati yao walivunja katiba ya chama.

Alifafanua kwamba, wajumbe wanne akiwamo Hamad Rashid  wamefukuzwa uanachama na kuanzia sasa  si mbunge kupitia chama hicho.

“Kuanzia sasa Hamad  Rashid si mwakilishi wa wananchi wa Wawi kupitia CUF, akitaka kuendelea kuwa Mbunge anapaswa kuwa mwakilishi kupitia mahakamani,”alisema Mtatiro.
Mwanasheria

Kwa upande wake ofisa mwandamizi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Harod Sungusia alisema tabia ya  vyama vya siasa kuwafukuza uanachama wanachama wake, inatokana na matokeo ya mmomonyoko wa utawala wa sheria.
Sungusia  alisema hayo jana jijini Dar es Salaam alipokuwa akitoa maoni kuhusu chama cha CUF kumfukuza uanachama mbunge huyo wa Wawi.

Alisema  vyama vya siasa vimekuwa vikifanya uamuzi kwa kujali maslai yao binafsi, ndio maana vimekuwa vikileta  msuguano ndani vya vyama na kusababisha wengine kufukuzwa.

“Kama wabunge wanatumia vizuri  chombo chao cha kutunga sheria, wanaweza kuondoa matatizo haya kwa kutunga sheria ambazo zitawasaidia wananchi pamoja na kuwapa miongozo mizuri katika kazi zao ndani ya Bunge na nje ya Bunge,” alisema Sungusia.

Imeandikwa na Boniface Meena, Elias Msuya, Aziza Masoud, Aidan Mhando na Geofrey Nyang'oro wa Mwananchi

No comments: