ANGALIA LIVE NEWS

Monday, January 2, 2012

Magufuli achafua hali ya hewa Dar

Waziri wa ujenzi Dk John Magufuli
BAADA YA KUWAAMBIA WAKAZI KIGAMBONI WAKISHINDWA KULIPA NAULI MPYA ZA VIVUKO WAPIGE MBIZI
Ramadhan Semtawa
WAZIRI wa Ujenzi, Dk John Magufuli amechafua hali ya hewa na kuingia kwenye mgogoro na wakazi wa Kigamboni, Dar es Salaam baada ya kuwaeleza kuwa ni lazima walipe nauli mpya za vivuko vya Mv Kigamboni na Alina na kama watashindwa, wapige mbizi baharini kuvuka.

Kauli hiyo ya Dk Magufuli imekuja siku mbili baada ya wizara hiyo kutangaza viwango vipya vya nauli mnamo Desemba 29, mwaka jana ambavyo vimepanda kwa asilimia 100 na vilianza kutumika jana Januari Mosi nchi nzima.

Baada ya kutangazwa kwa viwango hivyo vipya vya nauli, wakazi wengi wa Kigamboni walipinga kutokana na kile wanachosema hawakushirikishwa na ndipo jana asubuhi, Dk Magufuli alipoamua kufanya ziara ya ghafla katika vivuko hivyo na kusisitiza kwamba viwango hivyo lazima vilipwe.

Katika ziara hiyo, vyanzo vya kuaminika vilisema Dk  Magufuli alipofika eneo hilo la Kivukoni, alitoa msimamo huo na ndipo wananchi waliokuwa wakimsikiliza walipoanza kumzomea na kukatisha hotuba yake mara kwa mara.

Vyanzo hivyo viliongeza kwamba, kitendo hicho cha zomeazomea, kilimkera Dk Magufuli ambaye pamoja na mambo mengine, alisisitiza nauli hizo lazima zilipwe na mtu asiyetaka ni vyema akapiga mbizi kwa kuogelea kutoka Kigamboni hadi ng'ambo ya pili au apite Kongowe kuingia katika katikati ya jiji.

Msemaji: Waziri amechukizwa
Akizungumzia tukio hilo, Msemaji Mkuu wa wizara hiyo, Martin Ntemo alisema Waziri Magufuli hakufurahishwa na kitendo cha baadhi ya watu kumzomea wakati alipokuwa akizungumza... “Amechukizwa na baadhi ya watu kuzomea wakati alipokuwa akizungumza. Alichokuwa akisisitiza ni kwamba nauli mpya lazima ilipwe lakini wapo waliokuwa hawataki kuelewa wakawa wanapinga.”

Alisema kuna watu walikuwa wamepangwa kufanya mgomo kupinga nauli mpya kitendo ambacho pia kilimkera waziri alipokuwa kwenye ziara hiyo.

Magufuli na waandishi

Baada ya kuzomewa Kigamboni, Dk Magufuli alifanya mkutano na waandishi wa habari na kusisitiza kwamba, “Kuanzia Januari, Mosi, mwaka huu Wizara ya Ujenzi kupitia Wakala wa Ufundi na Umeme (Temesa), imeongeza viwango vya nauli katika vivuko vyote vya Serikali nchini.”

Alisema kwa muda wa miaka 14 iliyopita Kivuko cha Kigamboni kimekuwa kikitoza nauli ya Sh100 kwa mtu mmoja, wakati vivuko vingine vyote nchini, vimepandisha nauli zaidi ya mara mbili tangu mwaka 1997 kuendana na gharama za uendeshaji.

“'Kwa mfano, Kivuko cha Pangani ambako umbali wa uvushaji hauzidi ule wa Magogoni kilikuwa kinatoza Sh 200 na hali ya uchumi kwa wananchi ni ya chini kuliko Dar es Salaam. Kivuko cha Kilombero kilikuwa kikitoza Sh200 ikilinganishwa na Sh100 zilizokuwa zikitozwa hapa Magogoni.” 

Dk Magufuli alitaja sababu zilizochangia kupandisha nauli hizo kwamba ni pamoja na ongezeko la mishahara ya watumishi serikalini kwa zaidi ya asilimia 100, ongezeko alilosema la zaidi ya asilimia 400 la bei ya mafuta ya dizeli na mafuta ya kulainishia mitambo ambayo hutumika kuendeshea vivuko hivyo. 
 
Alitaja sababu nyingine kwamba ni pamoja na: “Ongezeko la bei za vipuri na kodi zake linalowiana na kushuka kwa thamani ya shilingi na ongezeko la bei kwa jumla.”

Alisema upandishaji wa nauli hizo ulifanywa kwa kuzingatia taratibu za kisheria na hatimaye kutangazwa kwenye Gazeti la Serikali toleo Na. 367 la Novemba 4, mwaka jana kwa mujibu wa sheria za uendeshaji wa vivuko vya Serikali.

“Sura 173 Kifungu cha 11(b), mwenye mamlaka ya kupanga nauli za vivuko vya Serikali ni Waziri mwenye dhamana na vivuko vya Serikali. Hata hivyo, kabla ya kufikia uamuzi huu, kumekuwa na jitihada za aina mbalimbali katika kuimarisha mapato ya vivuko. Machi, 2009, Wakala wa Ufundi na Umeme wakishirikiana na  
Jeshi la Polisi pamoja na Askari kutoka Kikosi cha Wanamaji waliendesha zoezi la kudhibiti mapato ya Kivuko.”

Alisema hilo liliwahi kufanywa na na Kampuni ya udalali ya Yono Auction Mart mnamo Aprili 17 hadi 20, mwaka jana kwa makubaliano na Temesa. “Zoezi hilo liliendeshwa tena Septemba 16 hadi 20, 2010 na 
Wizara kwa ushirikiano na Jeshi la Polisi.”

Alisema Julai, 2011, Temesa iliamua kubadili wakata tiketi na kuajiri wengine akisisitiza kuwa Serikali imechukua hatua mbalimbali kupambana na matukio ya watumishi wasio waaminifu. Hatua nyingine ni ile ya Temesa  kuondoa askari wa kuajiriwa na badala yake kuingia mikataba na kampuni za ulinzi.

“Kwa sasa katika Kivuko cha Magogoni, Kampuni ya ulinzi ya Suma JKT ndiyo inayotumika kufanya kazi hiyo,” alisema.

Alisema juhudi hizo zimesaidia kuongeza mapato kwa siku kutoka Sh5.5 milioni mwaka 2009 hadi Sh9 milioni kwa sasa katika Kivuko cha Magogoni na kusisitiza kwamba wizara itaendeleza hatua hizi kwa lengo la kubana uvujaji wa mapato na matumizi yasiyo ya lazima kwa vivuko vyote. 

Magufuli alisema kwa utaratibu, watumiaji wote wa huduma za vivuko wanatakiwa walipie huduma hiyo na kuongeza: “Tunaomba utaratibu huu uzingatiwe isipokuwa kwa wanafunzi waliovaa sare za shule. Tunasisitiza watumiaji wa vivuko waheshimu sheria na taratibu zote za vivuko kwa ajili ya usalama wao na ufanisi wa huduma.”


Mbunge achukizwa

Kwa upande wake Mbunge wa Kigamboni, Dk Faustine Ndugulile alikiri kusikia maneno ya Magufuli ambayo hayakuwafurahisha wapiga kura wake na kuahidi kuendelea kufuatilia kujua undani hasa wa kauli hizo. 

Dk Ndugulile alifafanua kwamba baada ya tangazo hilo la ongezeko la nauli, aliwasiliana na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadiki na taarifa alizonazo ni kwamba nauli hizo zimesitishwa.

Alifafanua kwamba baada ya kuwasiliana na waziri mkuu, jibu alilopata jana saa 1: 00 usiku ni kwamba mpango huo wa kupandisha nauli umesitishwa hadi hapo itakapoamuliwa vinginevyo.

Dk Ndugulile alisema sababu zilizomfanya yeye na wananchi kupinga nyongeza hiyo ya nauli ni Serikali kushindwa kueleza wazi vigezo vilivyotumika na kushindwa kuwashirikisha wananchi wa maeneo husika. Alitoa mfano wa Bajaji ambao alisema ni usafiri wa wanyonge uliokuwa ukitozwa Sh300 lakini kwa viwango hivyo vipya, itavushwa kwa Sh1,300 huku baiskeli ya miguu mitatu inayotumiwa na wanyonge pia kuchukulia bidhaa kutoka Kariakoo ikiongezewa nauli kutoka Sh200 hadi Sh1,800 na gari ndogo sasa zinatakiwa kulipa Sh1,500 badala ya Sh800.

“Sasa angalia hivyo vigezo, utaona mwananchi wa kawaida amezidi kuumizwa. Leo hii tayari bei za bidhaa zinazoletwa Kigamboni kutoka sokoni kama Kariakoo kwa kutumia maguta zimepanda. Mtu mwenye gari anapadishiwa bei chini ya mwenye guta, vigezo gani hivi? Baada ya kuona hivyo, niliwasiliana na Waziri Mkuu Ijumaa (Desemba 30, mwaka jana) na jana Mkuu wa Mkoa akanipa jibu kwamba Waziri Mkuu kasema nauli hizo zisipandishwe kwanza. Kwa hiyo mimi na wananchi wangu tunajua hivyo,” alisema na kuongeza:

“Hili ni jambo la ajabu sana. Yaani Waziri Mkuu anasema hivi halafu waziri wake anafanya vingine! Uko wapi sasa utendaji kazi wa pamoja wa Serikali?”


Baadhi ya wananchi wamelaani kauli hiyo za Dk Magufuli wakisema haikupaswa kutolewa na waziri ambaye ana dhamana ya kuhakikisha matatizo ya wananchi yanatatuliwa. Mmoja wa wakazi wa Kigamboni aliyejitambulisha kwa jina la Hamis Bwamkuu alisema: “Waziri anatoa kauli za kejeli namna hii! Ametusikitisha sana na kwa kweli tunamuomba Rais Jakaya Kikwete amchukulie hatua za kinidhamu.”

Pia wananchi hao wamemshutumu Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Dk Hurbet Mrango na Temesa kwa kushindwa kuwashirikisha na pia kumshauri vibaya waziri katika jambo hilo. 

"Katibu Mkuu ndiye mtendaji na Temesa wao ndiyo wakala lakini hawakumwambia kwamba wananchi hawakujua na hata mbunge wetu. Kwa hiyo hawa ni sehemu ya tatizo na hii si mara ya kwanza.”


Mwananchi

No comments: