ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, March 11, 2012

Azam yajikong’otea Yanga

Mwamuzi Israel Nkongo akikwepa konde la beki wa timu ya Yanga, Stephano Mwasika (wa nne kulia), wakati wa mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Azam iliyofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jana. Wengine ni wachezaji wa Yanga waliokuwa wakimzuia Mwasika, ambapo kutoka kulia ni Shadrack Nsajigwa , Omega Seme na Nurdin Bakari. Kwa mbali Nadir Haroub ‘Cannavaro’ naye akizuiwa na Hamis Kiiza asimvae mwamuzi. Azam ilishinda mabao 3-1. (Picha na Fadhili Akida).


MAMBO jana yalikuwa magumu kwa Yanga ya Dar es Salaam baada ya kukubali kipigo cha mabao 3-1 kutoka kwa Azam katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara. 

Azam ilikuwa ya kwanza kupata bao lililofungwa na John Bocco dakika ya tatu ya mchezo huo, baada ya kumnyang’anya mpira beki wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro na kumfunga kirahisi kipa Shaaban Kado. 


Baada ya bao hilo timu hizo ziliendelea kushambuliana kwa zamu, huku umaliziaji ukiwa mbovu kwa pande zote mbili katika mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. 

Dakika ya 13 Yanga ilipata pigo baada ya kiungo wake, Haruna Niyonzima ‘Fabregas’ ambaye ni mchezaji wa kimataifa wa Rwanda, kutolewa nje kwa kadi nyekundu, baada ya kumtolea lugha chafu mwamuzi wa mchezo huo, Israel Nkongo. 

Niyonzima awali alioneshwa kadi ya njano kwa mchezo mbaya, hivyo baada ya tukio hilo alioneshwa kadi ya pili ya njano iliyoambatana na nyekundu. 

Hatua hiyo ya Niyonzima kutolewa nje ilizua kizaazaa kwenye mchezo huo, ambapo wachezaji wa Yanga walimvamia mwamuzi Nkongo na kuanza kumfukuza uwanjani, wakiongozwa na Stephano Mwasika na Cannavaro. 

Baada ya vurugu hizo zilizochukua karibu dakika sita kutulia, mwamuzi alimuonesha kadi nyekundu Cannavaro na kuzusha tena mtafaruku mkubwa, kabla ya hali kutulia na mchezo kuendelea. 

Kwa kiasi kikubwa mapengo ya wachezaji hao yaliiathiri Yanga na kuonekana kuzidiwa kwa kiasi kikubwa kutokana na kucheza wachezaji nane ndani huku kipa akiwa wa tisa, wakati wenzao wakiwa kumi ndani na kipa akiwa wa 11. 

Kocha wa Yanga, Kostadin Papic baada ya kuona hali hiyo alimpumzisha mshambuliaji Davies Mwape na kumuingiza beki Chacha Marwa, kisha dakika chache baadaye aliingia kiungo Godfrey Bonny badala ya Shamte Ally. 

Mabadiliko hayo kwa kiasi kikubwa yaliisaidia Yanga kuweza kumiliki mpira, ingawa upungufu wao uwanjani ulikuwa tatizo kubwa. 

Kazi nzuri iliyofanywa na beki Shadrack Nsajigwa, iliipatia Yanga bao la kusawazisha dakika ya 34 mfungaji akiwa Hamisi Kiiza. 

Azam ambayo kwa matokeo hayo imeshika usukani wa ligi baada ya kufikisha pointi 41 na kuchupa kutoka nafasi ya pili, ikiiacha Simba nafsi ya pili ikiwa na pointi 40, ilipata bao la pili dakika ya 54 mfungaji akiwa Balou Kipre kwa shuti la mbali lililowagonga mabeki na kumpoteza kipa Kado. 

Dakika ya 76 Bocco aliipatia Azam bao la tatu akiunganisha vyema kazi nzuri ya Salum Abubakari. 

Kutokana na matokeo hayo Yanga bado ipo nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 37. 

Hata hivyo Azam imezizidi Simba na Yanga michezo miwili. Mchezo wa kwanza baina ya timu hizo Azam ilishinda bao 1-0, ambapo zilipokutana kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi Januari mwaka huu, Yanga ilifungwa mabao 2-0. 

Akizungumza baada ya mchezo huo, Papic alisema kutolewa kwa Niyonzima na Cannavaro kuliwaathiri na kwamba vijana wake walijitahidi kucheza vizuri, lakini hatua ya kucheza pungufu ndiyo imewamaliza. 

Wakati huohuo, ligi hiyo inatarajiwa kuendelea leo kwa mchezo kati ya Simba na Toto Africans Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

No comments: