Wapeleka pingamizi lake Tume ya Uchaguzi
Wasema kwasababu amesafishwa kimakosa
Benjamin Mkapa atua Arusha, kunguruma leo
Wasema kwasababu amesafishwa kimakosa
Benjamin Mkapa atua Arusha, kunguruma leo
Msimamizi huyo, alisema kuwa ameamua kuyatupilia mbali baada ya kuridhika kuwa hayana msingi wala mashiko ya kisheria na kusisitiza kuwa wagombea wote wako huru kugombea ubunge na kuendelea na kampeni ambazo zitafikia kilele Machi 31, mwaka huu.
“Mimi nimepitia sheria na mimi mwenyewe ni mwanasheria na nimesaidiana na mwanasheria mwenzangu,” alisema Kagenzi na kuongeza: “Nimeona mapingamizi haya hayana mashiko ya kisheria na nimeyatupa.”
Kagenzi alipotakiwa kueleza kwa undani kwa sababu zipi hazikuwa za msingi, alijibu kwa ufupi kuwa waulizwe viongozi wa vyama kwa kuwa ameeleza sababu za kufanya hivyo na kuvipatia vyama.
Mgombea wa Chadema, Nasarri alimwekea pingamizi Sumari kugombea kwa madai kuwa siyo raia wa Tanzania kwa kuwa alizaliwa Thika, Kenya mwaka 1976 na kwamba hana fomu ya kuukana uraia wa Kenya.
Pia Chama cha Wakulima (AFP) kilimwekea pingamizi Sumari kupinga uraia wake na kwamba wadhamini wake wana utata.
Nacho Chama cha United People’s Democratic (UPDP) kilimwekea pingamizi Nassari kwamba aliandika maelezo yake kwa ufupi na bila kueleza kazi anayoifanya.
NASSARI ALIA NA SUMARI
Akizungumzia maamuzi ya mapingamizi hayo kutupwa Nassari alisema kuwa hawajaridhishwa na sababu za kutupwa kwa pingamizi dhidi ya Sumari.
Alisema wamegundua kuwa uamuzi wa Kagenzi una mapungufu ya kisheria na wameamua kukata rufani NEC.
“Sisi tunakata rufaa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ili tupate ufafanuzi zaidi kama mtu huyu alizaliwa nchi ya Kenya, na hajakana uraia wake na tuna nyaraka za siri zinazoonyesha kuwa si raia na zinaonyesha alipozaliwa, sasa anapewaje haki ya kugombea Tanzania?” alihoji Nassari.
Nassari alisema kuwa wao kama chama hawajaridhishwa kabisa na uamuzi huo, hivyo wanafanya taratibu za kupata fomu kutoka kwa msimamizi wa uchaguzi kwa ajili ya kukata rufaa NEC.
Meneja wa kampeni, Vicent Nyerere, alithibitisha baadaye jioni kuwa walifanikiwa kukata rufani NEC. Mwisho wa kukata rufani ilikuwa jana saa 11:00 jioni.
MKAPA KUNGURUMA LEO
Wakati Rais na Mwenyekiti Mstaafu wa CCM, Benjamin Mkapa akitarajiwa kuzindua kampeni za kumnadi Sumari leo, chama hicho kimetangaza rasmi kuvunjwa kwa makundi yote yaliyoibuka wakati wa mchakato wa kura za maoni.
Kimesema baada ya kuvunjwa kwa makundi hayo na kuwa kitu kimoja, watalitetea Jimbo la Arumeru Mashariki katika uchaguzi mdogo utakaofanyika Aprili Mosi, mwaka huu kuziba pengo lililoachwa na aliyekuwa mbunge wake, Marehemu Jaremiah Sumari. Katibu wa CCM mkoani Arusha, Mary Chatanda, alitangaza kuvunjwa kwa makundi hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na uzinduzi wa kampeni za chama hicho zitakazozinduliwa leo.
“Ni kawaida wakati wa kura za maoni kuwepo kwa makundi, lakini baada ya kumpata mgombea wetu, wote tumerudi na tunatetea maslahi ya chama chetu katika uchaguzi,” alisema Chatanda.
Ingawa Chatanda hakuyataja makundi hayo, wakati wa mchakato wa kura za maoni yaliibuka makundi mawili moja likiwa la wafuasi wa Sumari na lingine la William Sarakikya.
Sumari na Sarakikya walichuana katika uchaguzi wa duru ya pili na Sumari kuibuka na ushindi. Awamu ya kwanza ambayo Sumari aliongoza wagombea wote sita waliochukua fomu walishindwa kufikisha nusu ya kura na Kamati Kuu (CC) ya CCM kuamuru urudiwe na kuwapambanisha Sioi na Sarakikya.
Chatanda alithibitisha kuwa Mkapa aliwasili jana jijini Arusha kwa ajili ya kuzindua kampeni hizo.
Alisema pia tayari mjumbe wa CC ambaye pia ni mlezi wa CCM Mkoa wa
Arusha, Steven Wasira na Katibu Mkuu wa CCM, Willson Mukama wamewasili jijini Arusha kwa ajili ya uzinduzi huo.
Chatanda alibainisha kuwa watazindua kampeni zao kwa viongozi wa kitaifa na mkoa kutembelea wanachama wao katika kata mbalimbali za jimbo hilo.
“Tunafanya uzinduzi wetu wa kipekee, viongozi watawatembela wanachama wetu katika kata mbalimbali kabla ya uzinduzi rasmi ambao utafanyika jioni,” alisema Chatanda.
Alisema uzinduzi huo utatanguliwa na maandamano makubwa yatakayoanzia nyumbani kwa mgombea katika eneo la Akheri na kuelekea katika mji mdogo wa User River katika uwanja wa Ngaresero.
Aidha, Chatanda alieleza kuwa katika maandamano hayo kutakuwepo na watumbuizaji wa matarumbeta, vikundi vya sanaa na ngoma, kikiwemo kikundi cha uhamasishaji cha CCM cha Tanzania One Theatre (TOT).
“Sisi hatutafanya kama wenzetu, tutakuwa na wanachama wetu wa jimbo na wapenzi wetu kutoka katika eneo hilo na wala hatutatumia helikopta kwani huwafanya watu kujitokeza kuishangaa tu na zaidi mbinu zote hizo
walizikopi kutoka CCM,” alisema Chatanda akikisema Chadema ambacho juzi kilizindua kampeni zake kwa kishindo, ikiwa ni pamoja na kutumia helikopta.
Alitamba kuwa CCM ni dume la mbegu bora na kwamba ni lazima wataibuka kidedea katika uchaguzi huo unaobashiriwa kuwa na ushindani mkali.
Alisistiza kuwa chama hicho kitaendesha kampeni kwa njia za kistaarabu zisozokuwa na matusi wala lugha za kashfa.
KAMPENI ZA CHADEMA SOKONI
Nassari jana alitembelea katika soko la Usa River na kupokewa kwa vigelegele na shangwe kubwa, huku wakimtaka kuwatatulia kero za maji machafu ya chooni yanayotoka kwenye nyumba za jirani na eneo hilo.
Wafanyabaishara hao walisema wanateseka sana na harufu mbaya ya kinyesi hicho pamoja na kutozwa ushuru mkubwa kwa bidhaa zao bila kujali kuwa wanalipa kwa siku.
Aidha walisema soko hilo halina maji safi kwa ajili ya kuoshea mboga na maji ya kunywa na kwamba wanalazimika kupanga bidhaa zao chini kutokana na kutokuwepo kwa meza.
Akijibu hoja hizo, Nassari alisema kitu kikubwa anaomba kura zao ili aingie bungeni na kuwatatulia tatizo la maji na changamoto zote zinazosababishwa na uongozi mbaya wa halmashauri.
“Nitadaiana na Halmashauri kutatua tatizo kubwa la maji sokoni hapa, naomba tu kura zenu jamani akina mama,” alisema Nassari. Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba, alisema wanawashukuru wafuasi wa chama hicho kwa kuwachangia katika uzinduzi wa kampeni Sh. milioni saba, kati yake Sh. milioni 2.2 zilichangwa uwanjani na Sh. milioni 5.7 zilichangwa kupitia simu walizotoa.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment