ANGALIA LIVE NEWS

Monday, March 12, 2012

Raia wa Uholanzi amzaba vibao mwalimu mbele ya wanafunzi

Raia mmoja wa Uholanzi, Marise Koch, amemfanyia kitendo cha udhalilishaji Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Marera iliyopo kata ya Rhotia Wilayani Karatu mkoani Arusha kwa kumpiga vibao mbele ya wanafunzi na walimu wenzake.
Taarifa ambazo NIPASHE imezipata na kuthibitishwa na viongozi wa Idara ya Elimu Wilaya ya Karatu na Jeshi la Polisi, zinasema kutokana na udhalilishaji huo, raia huyo wa Uholanzi ameshafunguliwa jalada lenye namba KRT/RB/835/2012 katika kituo cha polisi Karatu kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Marera, Emmanuel Ginwe, alisema alipigwa vibao viwili na Koch baada ya kuwakuta walimu wa shule hiyo wakipanga ratiba ya shule.
Ginwe alisema tukio hilo lililotokea Februari 14, 2012 majira 4:30 asubuhi ambapo Koch ambaye anafadhili shule hiyo kwa kukarabati majengo ya shule, ofisi, nyumba za walimu na kompyuta ndogo za wanafunzi kufanyia michezo na kujifunzia kuandika alifika shule hapo kutembelea kama kawaida.
Alisema baada ya kufika shuleni hapo, alikuta walimu wakipanga ratiba ya shule na kuanza kuhoji kwanini walimu hawajaingia madarasani kufundisha wanafunzi ambapo alijibiwa kuwa wamepewa maelekezo ya kuandaa ratiba ya shule na baada ya kumaliza kazi hiyo wataingia madarasani kufundisha.
Hata hivyo majibu ya walimu hao hayakumridhisha Koch na kuamua kwenda ofisini kwa Mwalimu Mkuu na kuanza kumfokea kwamba yeye anafadhili vitu vingi, lakini kumbe walimu hawafundishi na kuanza kukusanya kompyuta zake ndogo kwa lengo la kuzichukua.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo hata hivyo alimsihi asichukue kompyuta hizo, lakini alikataa na alipoona anazuiliwa, alipiga vibao mwalimu huyo huku akiendelea kuzikusanya komputa  na kumnasa tena vibao tena mwalimu mkuu na kuchukua kompyuta zake 70 kati ya 93 zilizokuwepo na kuondoka zake.
 “Nimedhalilishwa sana mbele ya walimu, wanafunzi na mke wangu ambaye ni mwalimu, namshukru Mungu wakati ananipiga vibao japo ni mwanamke sikuweza kujibu mapigo,” alisemwa Ginwe.
Katibu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) wilaya ya Karatu, Peter Simwanza, alisema kitendo hicho ni cha kiudhalilishaji.
CHANZO: NIPASHE

5 comments:

Aliweiwei Machibya said...

Kweli ni uzalilishaji na ni kinyume na haki za binadamu.

Fredrick said...

Mtu anatoa mapesa yake anasaidia mahali kwa manufaa ya Watu wenyewe, Atahitaji sana kuona uwajibikaji na kujituma ili kupata moyo wa kuendelea kusaidia.
Hapa Mwalimu huyu kwa manufaa ya watoto wote wa shule hiyo waliokuwa wananufaika na ufadhili huo unatakiwa kukiri kuwepo kwa uzembe uliokidhiri!!! Hivi wajameni ratiba ya shule inaandaliwa na walimu wote wa shule kiasi cha kuvunja ratiba ya kufundisha????? Hata mimi ni Teacher bwana!!

Fredrick said...

Watanzania walio wengi na mungu atusaidie, tunapenda mambo makubwa na mazuri bila kuyafanyia kazi wala kuwajibika ipasavyo, huku tukilalamika tu mambo yanapokwenda kinyume na matarajio ya kula bata bila jasho.
Sasa huyu Mwalimu mpaka kupigwa vibao ni kwamba alikuwa anamzuia mfadhili kuchukua kompyuta zake!!! Mimi najiuliza, alikuwa anazuia za nini wakati hawaingii madarasani kufundisha, wangezitumia vipi? Huyo Mama mfadhili arudi kule shule akachukue zile zingine zilizobaki maana amechukua 70 kati ya 93 apeleke kwa wanaohitaji na watkao zitumia kiukweli, Anawajenge hata nyumba za nini watu wasioingia madarasani bwana??? Eti walimu wote wa shule tunaanda ratiba ya shule, "HUU NI UGONJWA"

Anonymous said...

Nafikiri vibao viwili havitoshi, alitakiwa apigwe kumi. Namkumbuka Mnali kule mahali flani Bukoba miaka miwili mitatu iliyopita.

Anonymous said...

Watanzania tumekuwa tukifanyia mchezo misaada tunayopewa kwa kudhani kuwa wazungu wana hela nyingi au kuna sehemu wanachota hela kuja kutusaidia.
Ila ukweli ni kwamba wanajinyima na wanafanya kwa moyo na kwa kujituma sana na wakija kuona kuwa jitihada zao hazithaminiwi na hakuna matunda ya kazi zao huwa wanachukia sana.
Na hapa najua hawa walimu watakuwa wamemkera tu maana watanzania nao tunajijua wenyewe.