ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, May 23, 2012

Mzindakaya ailipua kamati ya Lembeli


Mbunge mstaafu wa Kwela, Dk Chrisant Mzindakaya, akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam, jana. Picha na Rafael Lubava
Raymond Kaminyoge
MWANASIASA maarufu na Mbunge mstaafu wa Kwela (CCM), Dk Chrisant Mzindakaya, ameiponda Kamati ya Bunge ya Maliasili, Ardhi na Mazingira, kuwa inaingilia kazi za Serikali katika ugawaji vitalu vya uwindaji.

Dk Mzindakaya alisema mapendekezo yaliyotolewa na kamati hiyo kwenye kikao kilichopita na baadaye kupitishwa kama maazimio, kuwa zoezi la ugawaji vitalu vya uwindaji utangazwe upya kwa kuzingatia sheria ya ununuzi wa umma ni kinyume na sheria.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Dk Mzindakaya alisema sheria namba 5 ya mwaka 2009, inaeleza wazi uwiano wa ugawaji vitalu ambao asilimia 85 ni wazalendo na asilimia 15 ni wageni.
“Baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo wanataka kampuni zaidi za kigeni zipate vitalu vya uwindaji iwapo ugawaji huo utarudiwa wakati sheria inaeleza wazi,” alisema Dk Mzindakaya.

Alisema wajumbe hao wa kamati mchana wanatetea wazalendo kupewa upendeleo, wakati huohuo wanataka kuzipendelea kampuni za kigeni ili zipate vitalu zaidi.

Lakini, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Maliasili, Ardhi na Utalii, James Lembeli na makamu wake, Abdulkarim Shaha, walipopigiwa simu kwa nyakati tofauti kuzungumzia suala hilo hawakupatikana.
Dk Mzindakaya alisema kampuni kubwa za kigeni zinahangaika huku na kule kuhakikisha zinapewa fursa kubwa ya kupata vitalu zaidi ya asilimia 15 iliyopo katika sheria.

Alisema Bunge halina mamlaka ya kutengua uamuzi wa waziri pale anapotekeleza sheria: “Vitalu vimekwishagawiwa kwa wazalendo walio wengi uamuzi wa waziri usitenguliwe.”  
 
Uwindaji wa kitalii upigwe marufuku
Dk Mzindakaya alishauri Serikali itunge sheria kuzuia uwindaji wa kitalii kwa kuwa eneo hilo ndilo kichaka cha walarushwa na kwamba, iboreshe vyanzo vingine vya mapato kama utalii wa picha.

“Lawama nyingi zinazotokea kwenye Wizara ya Maliasili na Utalii ni kutokana na biashara ya uwindaji wa kitalii, tuzuie kwa kuwa haliongezi pato kubwa la Serikali,” alisema.

Alisema Kenya ni miongoni mwa nchi ambazo zimezuia uwindaji wa kitalii na wanaingiza mapato kwa utalii wa picha.Dk Mzindakaya alisema athari za uwindaji wa kitalii ni kubwa zikiwamo kuuawa kwa wanyama.



Mwananchi

No comments: