ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, May 23, 2012

Waziri Wasira azomewa


 Ni wapigakura wa jimboni kwake
  Akerwa na Wenje kuzoa wanachama
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wasira
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wasira, amejikuta katika wakati mgumu kwa kuzomewa na kuulizwa maswali magumu na wananchi wa jimbo lake wakati akihutubia mkutano wa hadhara katika viwanja vya stendi ya zamani mjini Bunda, mkoani Mara.

Waziri Wasira ambaye pia ni Mbunge wa Bunda alikumbwa na zomeazomea hiyo pale alipoanza kumponda Mbunge wa Nyamagana (Chadema), Ezekia Wenje, kwamba ana shaka na uraia wake na kwamba huenda ni raia wa nchi jirani, ambaye hata hivyo, hakuitaja.

Wananchi waliendelea kumzomea Wasira alipoviponda vyombo vya habari kuandika habari kwamba CCM Bunda yapata pigo, baada ya aliyekuwa mgombea ubunge kwenye kura za maoni za chama hicho mwaka 2005 na 2010, Jeremiah Maganja, kukihama na kujiunga na Chadema.



Alisema kuwa pia habari zilizoandikwa kwamba wanachama wengi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Arusha, wamehamia Chadema siyo za kweli, kwa kile alichoeleza kuwa yeye ni mlezi wa mkoa huo.

Alisema kwamba anaijua vizuri Arusha, ambapo alisema wanachama waliohamia Chadema ni watatu tu, akiwemo aliyekuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Mkoa wa Arusha, James Millya, na kuongeza kuwa vyombo vya habari mara nyingine vinapotosha habari.

Hata hivyo, Wasira alisema mtu kuhama chama siyo kosa na kutamba hata yeye aliwahi kuhamia upinzani (NCCR-Mageuzi) na kwamba akiwa huko aligombea ubunge na Waziri Mkuu mstaafu, Joseph Warioba, na kumbwaga.

“Kuhama chama siyo kosa hata mimi niliwahi kuhama na katika kugombea ubunge nilimbwaga mtu mzito Jaji mstaafu Joseph Sinde Warioba, lakini baadaye nilirudi CCM,” alisema.

Aliendelea kuviponda vyombo vya habari  kwamba habari hiyo haikuwa sahihi kwa sababu, Maganja hakuwa na nguvu ndani ya CCM, kauli iliyowafanya wananchi kumzomea tena wakidai hiyo siyo hoja.

Zomeazomea iliendelea baada ya Wasira kuhoji kwamba Wenje alikwenda kuhutubia Bunda akiwa kama nani, kwa sababu hilo siyo jimbo lake.

“Hivi mimi nauliza Wenje alikuja kuhutubia hapa akiwa kama nani....maana hili siyo jimbo lake?” alihoji Wassira na kabla hajaendelea kutetea hoja yake hiyo, alikumbwa na zomeazomea nyingine kutoka kundi la wananchi wengi wakiwa ni vijana huku wakimuonyesha alama ya vidole viwili.

“Mheshimiwa waziri kumuongelea Wenje kwamba siyo raia na pia alikuja kuhutubia hapa kama nani hiyo siyo hoja, wewe ukiwa mbunge hauoni kwamba unaleta makundi ndani ya jamii...wewe twambie mambo ambayo tangu tukuchague umeyafanya na unaendelea kuyafanya kwa ajili ya kutuletea maendeleo, siyo kumuongelea Wenje hapa,” alisema kijana mmoja msomi wa chuo kikuu, Joash Kunaga.

Godfrey Nyamusenda, ambaye kitaaluma ni mwanasheria, aliuliza swali akisema kwamba sasa hivi hapa nchini wananchi wamekosa uzalendo kutokana na vitendo vya ufisadi vinavyofanywa na baadhi ya watendaji wa serikali na kuhoji serikali inachukua hatua gani kurejesha uzalendo.

Katika mkutano huo wananchi waliibua hoja ya kukosa maji safi na salama ambapo mwananchi mmoja alihoji kama Wasira naye anakunywa maji hayo.

Waziri Wasira alisema kuwa hata yeye pia anakunywa maji hayo, na baada ya kujibu hivyo akakumbana na zomeazomea nyingine.

“Hata kama mkizomea ukweli ndiyo huo, sasa mnazomea hooooooo nini sasa,” alisema Waziri Wasira akionyesha kukasirishwa na zomeazomea hiyo.

Pia Waziri Wasira alisema kero ya maji itaisha kabisa baada ya kukamilika kwa mradi mkubwa wa maji ya bomba kutoka katika ziwa Victoria unaotekelezwa na serikali kwa ufadhili wa Benki ya Dunia. Alisema uko katika hatua ya pili ambayo ni ya uchimbaji wa mtaro, kwa ajili ya kutandaza mabomba.

Kero nyingine walizozitaja wananchi hao ni pamoja na manunuzi mabaya katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, ambapo mwenyekiti mmoja wa kitongoji katika mji mdogo wa Bunda, Maximillian Bwire, alitoa kielelezo cha waraka mmoja uliyokuwa unaonyesha utengenezaji wa milango tisa katika Shule ya Sekondari Nyiendo umegharimu Sh. 6,440,000.

Kadhalika Wasira alielezwa kuwa mkuu wa zamani wilaya ya Bunda, Chiku Ghallawa, alichukua eneo la Shule ya Msingi Balili na kuwekeza majengo ya hoteli bila kuchukuliwa hatua licha ya wananchi kulalamika mara kwa mara.

Naye Mzee Korogo Korogo alisema kero nyingine ni wazee kutokupata huduma za matibabu bure kwenye vituo vya afya na hospitalini, hivyo wamekuwa wakilazimika kununua dawa madukani, pindi wanapougua licha ya sera ya serikali inayosema kwamba wazee watibiwe bure.

Wananchi hao walisema kuwa kero nyingine ni ahadi za Rais kutokutekelezwa kwa wakati, ikiwemo ahadi ya barabara za mjini Bunda kuwekwa lami na barabara ya Bunda-Kisorya hadi Ukerewe kujengwa kwa kiwango cha lami.

Akijibu kero hizo, Wasira alisema sera ya serikali ni wazee kupata huduma za matibabu bure na kwamba siyo wazee wote bali wale ambao hawana uwezo. Kuhusu ahadi za Rais, alisema zinaendelea kutekelezwa na nyingine zitatekelezwa ndani ya kipindi cha uongozi wake.

KIMBUNGA CHA CHADEMA BALAA


Wanachama wa CCM zaidi ya 400, wakiwepo mabalozi 16 na wajumbe wa serikali za vijiji wa Kata ya Mbulumbulu, wilayani Karatu, Mkoa wa Arusha, juzi walijiondoa katika chama hicho na kujiunga na Chadema.

Kata ya Mbulumbulu ni moja kati ngome chache za CCM, katika Wilaya ya Karatu ambayo halmashauri yake inaongozwa na Chadema. Diwani na viongozi wengi wa serikali za vijiji wanatoka CCM.

Wanachama hao walitangaza uamuzi huo katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Kambi ya Simba na kuongozwa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Lazaro Massay, Mbunge wa  Karatu, Mchungaji Israel Natse na Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Karatu, Moshi Darabe.

Katika mkutano huo ambao ni sehemu ya mikutano ya Chadema iliyopewa jina la “vua gamba vaa gwanda”, mamia ya wana-CCM hao walisema waliamua kukihama chama tawala kutokana na kupinga utendaji mbovu wa watendaji wa serikali za vijiji katika kata hiyo ambao walidai kuwa umekuwa ukiungwa mkono na viongozi wa serikali na CCM katika wilaya hiyo.

Massay ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya  Karatu, alisema hakuna sababu ya wakazi wa kata hiyo kuendelea kug’ang’ania kuwa CCM wakati wanakabiliwa na matatizo mengi yanayosababishwa na uongozi mbaya.

“Jamani nyie wenzangu wa Kambi ya Simba, ondokeni huko CCM, njooni Chadema tukae pamoja kama kata nyingine, matatizo yenu mengi ambayo mmetueleza yanatokana na uongozi mbaya mliouchagua,” alisema Massay.

Alisema viongozi wa kijiji hicho wamekuwa kikwazo kutokana na kuvuruga miradi ya maendeleo, ikiwepo miradi ya maji na afya.

“Sisi tumepata malalamiko yenu na tutatuma timu ya wataalam kuja kupitia mahesabu ya kijiji hiki cha Kambi ya Simba na maeneo mengine,” alisema Massay.

Naye Mchungaji Natse alisema Halmashauri ya Karatu itahakikisha inawashughulikia watendaji wote wa kata hiyo ambao wanatuhumiwa kwa ubadhirifu.

“Hapa kwenu kuna matatizo mengi sana, ambayo yanachangiwa na hawa viongozi wa CCM kubebana, sasa tunasema ni mwisho, kama tulivyofanya bungeni naomba mfanye na hapa tuwaondoe viongozi hawa,” alisema Mchungaji Natse.

Aliwataka wakazi wa kata hiyo kushirikiana kwa pamoja bila kujali itikadi zao na kujitokeza kuchangia miradi yao ya maendeleo na pia kutoa maoni juu ya mabadiliko ya Katiba mpya.

Imeandikwa na Mwandishi wetu Bunda na Cynthia Mwilolezi, Arusha.
CHANZO: NIPASHE

No comments: