Waandishi Wetu, Singida, Dar
JESHI la Polisi mkoani Singida, limemkamata na kumfikisha katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Singida, Mkurugenzi wa Sera na Utafiti wa Chadema, Waitara Mwita kwa tuhuma za kutoa lugha ya matusi dhidi ya Mbunge wa Iramba Magharibi (CCM), katika mkutano ambao ulisababisha mauaji ya Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wa Kata ya Ndago, Yohana Mpinga (30).
Waitara alikamatwa juzi asubuhi muda mfupi baada ya kumaliza kutoa tamko la chama hicho kutohusika na mauaji ya kijana huyo na mchana wake alipandishwa kizimbani, huku vijana wengine sita, wakituhumiwa kwa mauaji ya Mpinga.
Awali, Mwanasheria wa Serikali, Seif Ahmed alidai mbele ya Hakimu wa mahakama hiyo, Ruth Masssamu kuwa mnamo Julai 14, mwaka huu saa 10:00 alasiri huko katika Kijiji cha Nguvumali, Kata ya Ndago wilayani Iramba, mshtakiwa bila uhalali, alimtusi Mbunge Mwigulu kuwa ni malaya, mzinzi na mpumbavu, huku akijua kuwa kitendo hicho ni kinyume cha sheria.
Seif alisema mshtakiwa bila uhalali, alitenda kosa hilo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Nguvumali kwa lengo la viongozi wa Chadema kuzungumza na wananchi.
Hata hivyo, Waitara alikana kutenda kosa hilo na yupo nje kwa dhamana hadi Julai 30, mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa tena.
Mbali na Waitara, vijana hao sita wakazi wa Kijiji cha Nguvumali wamefikishwa mahakamani hapo wakituhumiwa kuhusika katika mauaji ya Mpinga.
Mwanasheria wa Serikali Mwandamizi, Neema Mwanda aliwataja washtakiwa hao kuwa ni Manase Daudi (40), William Elia (33), Frank Stanley (20), Charles Leonard (36), Tito Nintwa na Fillipo Edward (30).
Alidai mbele ya Hakimu Massamu, kuwa mnamo Julai 14, mwaka huu saa 10:00 alasiri huko katika Kijiji cha Nguvumali, washtakiwa wote kwa pamoja bila uhalali, walimpiga kwa kutumia fimbo na mawe mwenyekiti huyo wa UVCCM na kusababisha kifo chake.
Washtakiwa hao hawakutakiwa kujibu lolote kwa vile mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji na wamepelekwa rumande hadi Julai 30, mwaka huu kesi yao itakapotajwa tena.
Wadau walaani
Vyama vya siasa nchini vimetakiwa kufanya shughuli za kisiasa bila ya vurugu ili kupunguza matukio ya hatari ambayo yanahatarisha amani kwa wananchi wasio na hatia.
Akizungumza Dar es Salaam jana, CCM Tawi la Vyuo Vikuu, Assenga Abubakari alisema siasa zinazoendelea nchini hazina mwelekeo mzuri.
“Tunapoelekea kama nchi sipo. Nchi haiwezi kufikia siasa ya kupiga propaganda mpaka watu wengine wanapoteza maisha, sisi kama wanafunzi wa vyuo vikuu tunawataka wanasiasa wabadilike waanze kufanya siasa safi,” alisema Abubakari.
Makinda akemea
ugaidi bungeni
Spika wa Bunge, Anne Makinda jana alilazimika kutumia dakika kadhaa kukemea kile alichosema kuwa ni vitendo vya ugaidi miongoni mwa wabunge.
Makinda aliwataka wabunge waache tabia za kigaidi walizozianzisha kwa kutumiana ujumbe wa vitisho kwa kuwa hiyo ni “tabia mbaya na inaliaibisha Bunge.”
Alisema wabunge wanalindwa kwa Sheria ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, hivyo mtu akisema chochote bungeni kinatakiwa kuishia hapohapo na siyo kujengeana uhasama na kuanza kupeana vitisho.
Makinda alitoa maelezo hayo kutokana na ombi lililotolewa na Nchemba kwa kutumia Kanuni ya 47 akitaka kutoa hoja maalumu ya kujadiliwa kwa dharura vurugu zilizotokea jimboni kwake na kusababisha kifo cha mtu mmoja.
Spika Makinda alisema suala hilo haliwezi kujadiliwa kwani ameelezwa kuwa polisi wanafanya uchunguzi wa kina.
Alisema ni muhimu wabunge wakaacha tabia mbaya kwa kuwa wameanzisha tabia za kigaidi. Alisema wabunge wote ambao wamekuwa wakituma ujumbe wa vitisho namba zao anazo na kwamba zitawasilishwa polisi kwa ajili ya uchunguzi.
Awali, Nchemba alisema kutokana na vurugu hizo ambazo zimesababisha kifo cha msaidizi wake, amekuwa akipokea vitisho vya ujumbe wa simu kutoka kwa wabunge wa Chadema.
Nchemba alitaka kuwataja wabunge hao na kusoma ujumbe ambao ametumiwa lakini Spika Makinda alimzuia kwa kumweleza kuwa polisi wanalifanyia uchunguzi suala hilo.
“Mheshimiwa Spika ningependa nisome meseji za vitisho ambazo nimetumiwa na wabunge wa Chadema kutokana na vurugu zilizotokea Singida,” alisema Nchemba.
Habari hii imendaliwa na Boniface Meena, Dodoma, Gasper Andrew, Aziza Masoud na Zaina Malongo
Mwananchi
No comments:
Post a Comment